Serikali imepanga kutumia zaidi ya Sh bilioni 92 mwaka ujao wa fedha kuimarisha sekta ya uvuvi nchini ili kuhakikisha fursa zinazopatikana kwenye sekta hiyo zinachangia kikamilifu maendeleo ya nchi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha na Mipango, kiasi kikubwa cha fedha hizo zitakuwa za ndani zitakazotokana na kodi za Watanzania kwenye bajeti ijayo ambayo utekelezaji wake utaanza Julai mosi mwaka huu.
Takwimu kwenye mpango mkakati wa serikali kuiboresha sekta hiyo ya uvuvi zinaonyesha kuwa asilimia 82.4 ya fedha hizo ambazo ni Sh bilioni 92.13 zitatumika kulifufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO).
Maeneo mengine yaliyopewa kipaumbele kwenye mchakato huo ni ujenzi wa bandari ya uvuvi, uimarishaji wa miundombinu ya mialo na masoko ya uvuvi pamoja na kuanzisha kanda maalumu za ufugaji samaki na kutengeneza kanzidata ya viumbe maji.
Uwekezaji katika kuiendeleza sekta ya uvuvi pia utaelekezwa kwenye ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya ufugaji wa viumbe maji na kuimarisha ulinzi wa rasilimali za uvuvi na mazingira yake.
Sekta ya uvuvi ni moja ya maeneo yaliyoainishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21 kusaidia ujenzi wa misingi ya uchumi wa viwanda. Kwa sasa mchango wake kwenye pato la taifa ni mdogo ikilinganishwa na rasilimali zilizopo hasa katika bahari kuu.
Akizungumza mwishoni mwa mwaka jana wakati wa kupokea msaada wa Sh bilioni 4.2 kutoka Japan kwa ajili ya kufufua TAFICO, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, alisema uboreshaji wa shughuli za uvuvi utasaidia kuvutia Watanzania zaidi kujihusisha katika sekta hiyo kama chanzo cha ajira na kipato.
“Shughuli za uvuvi zilichangia asilimia 1.7 katika Pato la Taifa mwaka 2018, ambayo inadhihirisha umuhimu wa uvuvi katika uchumi, hivyo msaada uliotolewa utachangia jitihada za serikali katika kufikia Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, Malengo Endelevu ya mwaka 2030 na Ajenda ya Maendeleo ya Afrika ya mwaka 2063,” anasema Doto.
“Kiwango cha ukuaji kwa shughuli ndogo za kiuchumi za uvuvi kilifikia asilimia 9.2 mwaka 2018 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 8.4 mwaka 2017, ambapo kiwango kikubwa cha ukuaji kilitokana na utunzaji mzuri wa mazalia ya samaki yakiwemo mabwawa ya watu binafsi sambamba na kuongezeka kwa mahitaji katika soko la ndani na nje,” aliongeza.
Wakati akizindua menejimenti ya kusimamia utaratibu wa kufufua TAFICO miaka miwili iliyopita, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, alisema eneo la uvuvi wa bahari kuu tu likisimamiwa vizuri lina uwezo wa kuiingizia serikali Sh bilioni 352 kwa mwaka.
Mpina alisema kwa muda mrefu uvuvi wa bahari kuu hapa nchini umekuwa ukifanywa na meli za kigeni na kulikosesha taifa mapato makubwa, jukumu ambalo sasa litafanywa na TAFICO mpya. Kiwango ambacho kimekuwa kinakusanywa kama mapato yanayotokana na uvuvi wa bahari kuu ni wastani wa Sh bilioni 3.2 kwa mwaka, kiasi ambacho ni kidogo ikilinganishwa na fursa kubwa iliyopo kwenye eneo hilo.
Kwa mujibu wa Waziri Mpina, hatua ya kulizindua Shirika la TAFICO ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 Ibara ya 27(c) iliyoelekeza serikali kufufua shirika hilo na kununua meli tano za uvuvi zenye uwezo wa kuvua samaki bahari kuu na kuzalisha ajira zaidi ya 15,000 kwa mwaka.
Katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21 ambao ni wa mwisho katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano Awamu ya Pili (FYDP II), serikali inasema kuwa Sh milioni 700 fedha za ndani zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha usanifu wa kina na kuanza awamu ya kwanza ya ujenzi wa bandari ya uvuvi.
“Shughuli zilizopangwa kufufua Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO) ni pamoja na ununuzi wa meli mbili za uvuvi kwa ajili ya uvuvi kwenye Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu na meli moja ya mizigo ambapo Sh bilioni 75.93 fedha za ndani zimetengwa,” Wizara ya Fedha na Mipango inasema kwenye muhtasari wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21.
“Sh bilioni 4.2 fedha za nje zimetengwa kwa ajili ya kununua meli moja ya uvuvi kwenye maji ya ndani; mtambo wa kuzalisha barafu; ghala la ubaridi na gari maalumu la kuhifadhia samaki.”
Chapisho hilo la Wizara ya Fedha pia linasema Sh bilioni 2 fedha za ndani zimetengwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa mialo sita ambayo ni Kanyenze mkoani Mwanza, Nyamkazi (Kagera), Kirando (Rukwa), Nyamisati (Pwani), Shangani (Mtwara) na Masoko Pwani (Lindi).
Kwenye mwaka ujao wa fedha, serikali imepanga kutumia Sh milioni 500 kwa ajili ujenzi wa soko la samaki la Mbamba Bay lililopo Ziwa Nyasa mkoani Ruvuma. Mpango mwingine mkubwa katika kuiongezea tija sekta ya uvuvi ni ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya ufugaji wa viumbe maji.
“Shughuli zitakazotekelezwa ni: ujenzi wa vituo viwili vya Rubambagwe (zamani Nyamirembe), Kingolwira – Morogoro, kuanzishwa kwa mashamba darasa manne katika halmashauri nne na ukarabati wa vituo vya Ruhila – Songea, Mwamapuli – Tabora, na Nyegedi – Lindi, ambapo Sh bilioni 2.6 fedha za ndani zimetengwa.”
Wizara ya Fedha inasema Sh bilioni moja zitahitajika na kutumiwa katika mwaka wa fedha wa 2020/21 kuimarisha na kuendeleza ulinzi wa rasilimali za uvuvi na mazingira.
Shughuli zitakazotekelezwa katika eneo hili ni kuimarisha vituo vya doria kwa kuvipatia vitendea kazi na kutoa mafunzo kwa maofisa uvuvi, polisi, mahakimu na vikundi shirikishi vya ulinzi wa rasilimali za uvuvi (BMUs). Pia kutakuwepo kuwezesha uendeshaji wa doria kwa maeneo ya maji na nchi kavu pamoja na mipakani; na kufanya sensa ya uvuvi katika maziwa.
Maboresho ya sekta ya uvuvi yanazingatiwa na kutekelezwa pia chini ya awamu ya pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Nchini (ASDP – II). Mambo muhimu yatakayozingatiwa hapa ni pamoja na kuanzisha kanda za ufugaji wa samaki na kujenga kanzidata za ukuzaji viumbe maji.
“Sh bilioni 1.5 fedha za ndani zimetengwa kwa ajili ya: kuanzisha kanda za ufugaji wa samaki kwenye vizimba katika maziwa ya Nyasa na Tanganyika kwa kutambua maeneo na kufanya tathmini ya mazingira na kuandaa mpango wa
usimamizi wa mazingira,” Wizara ya Fedha inasema na kuongeza:
“Kuanzisha kanzidata ya ukuzaji viumbe maji itakayojumuisha taarifa za wakuzaji viumbe maji, watoa huduma na taarifa za masoko, na kujenga mfumo wa kielektroniki kupata taarifa za masoko ya mazao ya uvuvi; na kununua na kusambaza magari matano na pikipiki 10 ili kuboresha utoaji wa huduma za ugani katika vituo vitano vya kuendeleza ukuzaji viumbe maji.”
Juhudi za serikali kuindeleza sekta ya uvuvi pia itanufaika na Mradi wa Kikanda wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish) ambapo Sh bilioni 5.2 fedha za nje zinatarajiwa kupatikana kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Shughuli hizo ni pamoja na ujenzi wa jengo la utawala la Mamlaka ya Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu katika Kisiwa cha Mafia; ukarabati wa Soko la Kimataifa la Samaki la Feri jijini Dar es Salaam; ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Ukuzaji Viumbe Maji; na ujenzi wa ofisi za vikundi vya ulinzi shirikishi wa rasilimali za uvuvi vitakavyojengwa Mkinga, Pangani, Lindi na Bagamoyo.