Ndoto ya kuunganisha kwa lami Tanzania, Burundi, DRC kupitia ‘central corridor’ yaiva

Mtandao wa barabara kuu na barabara za mikoa nchini Tanzania unaosimamiwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) una jumla ya kilomita 36,258 zinazojumuisha kilomita 12,176 za barabara kuu na kilomita 24,082 za barabara za mikoa. 

Miongoni  mwa malengo makuu ya Sekta ya Ujenzi ni kujenga barabara kuu ili kufungua fursa za maendeleo na kiuchumi pamoja na kuhakikisha miji yote mikuu na mikoa inaunganishwa kwa barabara za lami. 

Katika kuhakikisha lengo hili linatimia, hivi karibuni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, alisaini mikataba yenye thamani ya Sh bilioni 585 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kabingo – Kasulu – Manyovu mkoani Kigoma yenye urefu wa kilomita 260. 

Akizungumza mara baada ya kusainiwa kwa mikataba hiyo mkoani humo, Mhandisi Kamwelwe amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 36.  

“Leo tupo hapa tukiwa na furaha kubwa kushuhudia tukio hili muhimu na la kihistoria katika mkoa huu, kusainiwa kwa mikataba hii ni kutimia kwa ndoto na ahadi ya Rais Dk. John Magufuli ya kuifungua Kigoma kiuchumi na kijamii kwa kuiunganisha kitaifa na kimataifa kutokana na barabara hii kuunganisha nchi jirani za Burundi, Rwanda na DRC – Congo,” anasema Mhandisi Kamwelwe.

Waziri Kamwelwe ametaja kampuni zilizopata zabuni kutekeleza mradi huo kuwa ni Zhejing Communication Construction Group Company Ltd (ZCCC), Sinohydro Corporation Ltd, Stecol Corporation na China Henan International Corporation (CHICO) ambapo utekelezaji wa mradi huo umegawanywa sehemu nne.

“Mradi huu utatekelezwa na makandarasi hawa kwa sehemu nne, sehemu ya kwanza itahusisha ujenzi wa barabara kuanzia Kasulu junction – Manyovu na viunganishi vya barabara za Kasulu mjini (Km 68.25), sehemu ya pili itakuwa ni Kanyani – Kidyama – Mvugwe (Km 70.5), ya tatu ni Mvugwe – Njia Panda ya Nduta (Km 59.35) na ya mwisho ni Nduta junction – Kabingo junction (Km 62.5),” anafafanua Mhandisi Kamwelwe.

Aidha, Mhandisi Kamwelwe amewataka makandarasi waliopata zabuni ya ujenzi wa barabara hiyo kuhakikisha wanatekeleza ujenzi wake kwa mujibu wa mikataba na kuwasisitiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kuhakikisha wanawasimimia makandarasi hao ili kupata barabara yenye kiwango sawa na thamani ya fedha itakayotumika.

Waziri Kamwelwe, ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kuboresha miundombunu ya barabara katika uwanda wa magharibi ili kuifungua Kigoma kitaifa na kimataifa.

“Serikali hii hailali,  inafanya kazi usiku na mchana, miradi ya ujenzi wa barabara kama ya Chaya – Nyahua (km 85.4),  Chagu – Kazilambwa (km 36) na Kaliua – Urambo (km 28)  inaendelea kujengwa na inatarajiwa kukamilika Oktoba  mwaka huu,” anabainisha Kamwelwe. 

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale, amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutarahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kati ya mkoa huo na mikoa ya jirani pamoja na nchi za Rwanda, Burundi na DRC – Congo katika ushoroba wa kati. 

Ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo utaenda sambamba na uboreshwaji wa huduma za afya pamoja na elimu kwa kujenga shule, zahanati pamoja na ununuzi wa magari manne ya wagonjwa ambazo zitasaidia katika kuleta maendeleo mkoani humo.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali mstaafu, Emmanuel Maganga, amesema kuwa ujio wa mradi huo mkoani kwake utasababisha uzalishaji wa ajira kwa vijana na kuimarika kwa huduma za usafiri na usafirishaji.

Mbali na utiaji saini wa ujenzi wa barabara hii katika mkoa huo, serikali imepanga kutekeleza miradi mingine kama uimarishaji wa Uwanja wa Ndege wa Kigoma kwa kuhusisha ujenzi wa jengo jipya la abiria pamoja na kujenga uzio katika eneo lote la uwanja, pamoja na kuweka taa za kuongozea ndege. 

Halikadhalika serikali katika mkoa huu itajenga mradi wa Bandari Kavu ya Katosho ambayo inatarajiwa kuhudumia mizigo ya nchi za DRC, Burundi na Rwanda. 

Miradi mingine ni ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Uvinza itakayounganisha Msongati – Gitega nchini Burundi kwenda Uvira hadi Kindu nchini DRC, ambapo mazungumzo ya utekelezaji wa mradi huu yanaendelea kati ya Tanzania, Burundi na DRC.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.