Wananchi wilayani Mkuranga wameutupia lawama uongozi wa Kiwanda cha Nondo cha Lodhia wakidai kunyanyasa wafanyakazi na kutokuwa na ushirikiano kwa jamii inayokizunguka.

Wakizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Subira Mgalu, hivi karibuni, wananchi ambao miongoni mwao ni wafanyakazi wa kiwanda hicho, wamedai kuwapo pamoja na mambo mengine, mapunjo ya mishahara na mikataba mibovu ya kazi.

“Wawekezaji hawana msaada kwa wafanyakazi, wakidai haki zao hufukuzwa kabisa kazini na kunyimwa stahiki zao,” anasema mkazi wa Kijiji cha Mpera, Rashidi Liundi, akielekeza lawama kwa uongozi wa Kiwanda cha Lodhia, miongoni mwa viwanda kadhaa vilivyopo wilayani Mkuranga.

Liundi amemwambia naibu waziri huyo pamoja na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini alioambatana nao kuwa mbali na unyanyasaji wa Lodhia, watumishi wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) wilayani humo nao wamekuwa kikwazo kingine cha maendeleo kwa wananchi.

Anatoa mfano wa suala la kuchangia huduma za nguzo za umeme, akisema awali wananchi waliahidiwa na Waziri wa Nishati na Madini alipowatembelea kuwa wangewekewa umeme wa REA majumbani mwao kwa Sh 27,000 tu bila kulipia gharama za nguzo.

Amesema wananchi waliokwenda ofisi za Tanesco wilayani humo walikutana na wafanyakazi aliodai kuwa si waaminifu waliowatoza fedha kulipia nguzo kwa gharama kubwa kiasi cha wengine kusita kujaza fomu za kuomba umeme.

Akijibu hoja hizo, Subira aliahidi kushugulikia suala la malipo ya nguzo haraka mara atakapokuwa na ushahidi wa kutosha wa kuwapo waliotozwa fedha.

“Serikali inafanya kazi kubwa kuhakikisha kila mwananchi vijijini anapata huduma ya umeme kwa gharama nafuu kama ilivyoahidi na si vinginevyo,” amesema.

Subira amewataka wananchi kuwa wavumilivu, akisisitiza kuwa mradi huo utafika katika kila kijiji nchini awamu kwa awamu, ambapo kwa wilaya hiyo, hadi kufikia mwaka 2021 vijiji 81 vitakuwa na umeme na kubaki vijiji 30 tu.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Vedasto Mathew, amewataka wawekezaji kuwa karibu na jamii.

“Mwekezaji anapaswa kujishughulisha na shuguuli za kijamii kwa kujenga vitu vyenye faida kama shule na hospitali wananchi wanufaike na kuwapo kwake,” anasema Mathew.

Mathew anasema katika ziara hiyo, kamati imeridhishwa na miradi mbalimbali kikiwamo kiwanda cha nondo kinachomilikiwa na Lodhia Group kikiwa moja kati ya viwanda 50 vitakavyonufaika na gesi asilia na kupunguza gharama za uendeshaji na uzalishaji.

“Tutaishauri serikali kusukuma matumizi ya gesi katika viwanda kama Lodhia na vingine ili kuviwezesha kuzalisha bidhaa na kuuza nje ya nchi huku zikipungua bei kwa wananchi,” anasema.

Mmiliki wa Kiwanda cha Lodhia, Harun Lodhia, anasema ujio wa gesi umeshusha gharama za uzalishaji kwa kiasi fulani na zitashuka zaidi baada ya kukamisha ubadilishaji wa mitambo yote itumie gesi.

Ameahidi kuwa karibu na jamii na kufanya kazi kwa manufaa ya wananchi, akiwa tayari ametoa ajira kwa watu 1,300.