Ndugu Rais, Baba Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania, Emmaus Mwamakula, malango yake yabarikiwe. Huyu ni kiongozi mkuu wa dini katika nchi yetu ambaye bila kujali kama atahusishwa na makundi fulani fulani, amesimama hadharani na kuitetea haki.





p.p1 {margin: 0.0px 0.0px 0.0px 0.0px; font: 10.0px ‘Myriad Pro’}
Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania, Emmaus Mwamakula (kushoto) akimjulia hali Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, aliyekuwa amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan baada ya kuumizwa katika vurugu zilizotokea katika Gereza la Segerea hivi karibuni.

Tunao viongozi wengi wa dini wa madhehebu mbalimbali katika nchi yetu lakini ni wangapi wamesimama hadharani kuisemea haki? Haki inaponyimwa katika nchi yoyote, magumu na machungu hata vifo huwaandama waja wa Mwenyezi Mungu.

Amelikiri lile neno lililoandikwa: “Mjapoteswa kwa ajili ya haki mna heri, msiogope kutisha kwao, kwa kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki na masikio yake husikia maombi yao, bali uso wake Bwana ni juu ya watenda dhambi, hukumu yao ni Jehenamu.”

Nchini mwetu imeingia hofu ya ugonjwa mbaya ambao wataalamu wamekiri walikuwa hawaufahamu. Wananchi sasa hawajui kipya hapa ni nini. Ni ugonjwa wenyewe au ni ufahamu kuwa sasa tumejua kuwa huo ni ugonjwa? Kama ulikuwa haujulikani, utasemaje kuwa ulikuwa haupo? Hofu mpya imechanganyikana na hofu iliyokuwapo.

Maandiko yanasema, haki haiombwi! Watu hudai haki yao. Palipo na dhuluma ya haki, amani haikai. Vurugu, machafuko na ghasia za kumwaga damu ndivyo hutamalaki.

Viongozi wema popote duniani huwaepusha wananchi wao na nchi zao kwa uwezo wao wote zisiingie katika ghasia za kumwaga damu. Hawa ni wale wanaoamini katika maridhiano. Katika maridhiano ndiyo kuna umoja, mshikamano na upendo wa kweli. Maridhiano ni kwa viongozi kuwasikiliza wale wanaowaongoza na wale wanaoongozwa kuwasikiliza viongozi wao. Hii ndiyo busara na hekima vinavyoitawala amani ya kweli.

Ubabe na mabavu ni kati ya vitu vilivyokosa busara na hekima. Kiongozi bora havikumbatii. Vinapopatiwa kipaumbele na baadhi ya viongozi wenye shingo ngumu huwapelekea magumu na machungu wananchi maskini na wanyonge kwa kipindi chote cha uwepo wa madarakani.

Kiongozi bora ni yule wa mfano wa Mfalme Suleimani. Mfalme Suleiman alibahatika kutakiwa na Mwenyezi Mungu aombe chochote naye angepatiwa.  Mfalme Suleimani aliomba hekima! Katika maendeleo ya kweli hakuna kuchelewa wala kucheleweshwa. Nchi kubwa na tajiri kabisa duniani kama Marekani, Uingereza, Urusi na nyingine bado zinaendelea kujiletea maendeleo. Tunakimbilia wapi tulikoambiwa sisi huko ndiko ukomo wa maendeleo hata tuwe na haraka?

Maendeleo ni juu ya jamii yetu na si vinginevyo. Jamii yetu ni dini mbalimbali. Jamii yetu ni makabila mbalimbali. Jamii yetu ni tamaduni mbalimbali. Na jamii yetu ni vikundi mbalimbali vikiwamo vyama vya siasa. Bila kuzingatiwa haya, hayo si maendeleo. Ng’oa hata milima, yote hayo yatabaki ni kubangaiza tu.

Nchi iliyokosa maridhiano kati ya wananchi na viongozi wao ni sawa na nchi iliyoingiliwa na ugonjwa mbaya unaoua. Ugonjwa hatari unapoingia katika nchi viongozi wema husimama na kutoa maelekezo kwa wananchi wao jinsi ya kujikinga wasipate maambukizi ya ugonjwa huo.

Tumewasikia viongozi wetu sasa, wakilisisitiza hilo mara kadhaa sasa. Siku zote wananchi ni wasikivu. Nao wanaofuata maelekezo ya viongozi wao hubaki salama.

Lakini kifo ni kifo tu, kiwe kwa mkuki au kiwe kwa upanga. Kifo cha ugonjwa huu ni kifo sawa na kifo cha ugonjwa mwingine. Hivyo busara ni kuzuia vifo vyote bila kubagua ugonjwa. Wanapotokea watu katika nchi wanaoteka na kuwatesa raia hata kuwaua bila kuguswa na sheria za nchi, huo ni ugonjwa hatari sana. Viongozi walio wema walipaswa kusimama kama walivyosimama kwa ugonjwa huu wa sasa na kutoa tahadhari kwa wananchi jinsi ya kujikinga na huu ugonjwa unaojulikana kama  watu wasiojulikana.

Juhudi kubwa zinaonekana kufanywa na viongozi wetu wa serikali kwa kuwasisitizia wananchi kunawa mikono kwa maji yanayotiririka mara kwa mara. Wanakatazwa kusalimiana kwa kushikana mikono. Wakikohoa wajizuie kwa viwiko vyao.

Wananchi wameshuhudia jitihada kubwa zinazofanywa na serikali yao katika kuhakikisha inadhibiti maambukizi kuenea, hivyo kupunguza idadi ya vifo vingi vinavyoweza kutokea. Shule na vyuo vimefungwa. Mikusanyiko mikubwa ya watu imepigwa marufuku. Michezo hata ligi kuu imesimamishwa. Na jitihada nyingine nyingi zinazofanywa na serikali yetu.

Wanachojiuliza wananchi wetu, ni kwanini nguvu kubwa kwa ugonjwa mmoja tu? Mbona hakuna tahadhari yoyote inayotolewa kwa wananchi jinsi ya kujikinga na ugonjwa huu hatari wa watu wasiojulikana? Wanaodhurika na kuuawa na ugonjwa huu ni wananchi walewale wana wa nchi hii.

Yaonekana ugonjwa wa watu wasiojulikana nao hauna tiba wala kinga. Isipotolewa kauli thabiti wako watu wanaweza wakaziita juhudi hizi za kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huu mpya ni maigizo. Wakasema hakuna mwenye uchungu wa kweli kwa vifo na mateso wanayoyapata wananchi wa nchi hii, iwe kwa ugonjwa huu au kwa ugonjwa wa watu wasiojulikana.

Tumwombe Mwenyezi Mungu anaporidhia kutupatia kupona ugonjwa huu basi atuponye pia na ugonjwa huu wa watu wasiojulikana ambao uligundulika katika nchi yetu mara tu baada ya kuingia kwa Awamu ya Tano. Hizi mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mafuriko yake  yasombe na hivi virusi vya ugonjwa wa watu wasiojulikana.

Wako wanaolalama wakidai machungu katika nchi yamepita kiwango cha uvumilivu. Mioyo yao imepondekapondeka nao wamekata tamaa. Wanasema wako tayari kwa kifo chema kutetea haki.

Tumehadithiwa kuwa Mashahidi wa Uganda walipowekwa katika tanuri la moto, waliimba kumtukuza Mungu mpaka walipoteketea kabisa! Zamani wachawi walichomwa moto. Siku hizi ndio wanawaombea wengine maisha marefu.  

Marehemu mama yangu aliniambia mchawi anahuzunika sana kuona  mwanadamu anakufa mwenyewe kwa amri ya Mungu. Alisema mchawi wa kweli hataki mtu ajifie. Anataka abaki ili amuue yeye. Hivi ndivyo alivyo yeyote anayekataa maridhiano. Mpaka aue yeye!

Baba Askofu Emmaus Mwamakula anasema: “Mimi kama askofu, ninaishauri serikali iunde tume huru ya uchunguzi ili kubaini ukweli kuhusu nini hasa kilitokea siku ile, kwa kuwa kuna hisia kuhusu uvunjwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji wa kijinsia katika tukio lile, hasa kwa kuwa kuna madai kuwa wanawake walikabiliwa visivyo na askari wa kiume.” Katika nchi ya maridhiano, upendo hutawala, si unyama.