Mpenzi msomaji, ungana nami katika safu hii ufahamu maana ya mirathi.
Mirathi ni mali iliyoachwa na mtu aliyefariki dunia kwa ajili ya kurithishwa warithi wake halali. Sheria imeweka taratibu maalumu zinazoongoza ukusanyaji, uangalizi, usimamizi, ugawaji na umiliki wa mali hizo pamoja na kulipa madeni aliyoacha wakati wa uhai wake au gharama zilizotokana na mazishi yake.
Mirathi hufunguliwa mahakamani kutokana na namna alivyoishi muhusika; mathalani, iwapo aliishi akifuata dini ya Kiislamu, mirathi yake hufunguliwa Mahakama ya Mwanzo au Mahakama Kuu na itagawiwa kufuata sheria za Kiislamu.
Iwapo alikuwa Mkristo, mirathi itafuata Sheria ya Serikali na itafunguliwa katika mahakama husika. Kwa aliyekuwa mpagani au alifuata mila na desturi zinazoruhusu wanawake wengi, mirathi itafunguliwa katika Mahakama ya Mwanzo au Mahakama Kuu kwa kuzingatia kiasi cha mali iliyoachwa.
Baadhi ya wajane wametendewa vibaya na ndugu au marafiki wa walioaga dunia kwa kunyang’anywa mali hata kabla ya mirathi kufunguliwa.
Kisheria hairuhusiwi mali za mtu aliyefariki dunia kutumiwa na yeyote bila kibali cha mahakama hata kama marehemu alikuwa na biashara ya bidhaa zinazoharibika haraka, ni mahakama ndiyo itaruhusu matumizi yake kwa faida ya wategemezi wake.
Imekuwa ni kawaida kwa baadhi ya ndugu wa marehemu bila aibu kung’ang’ania mali bila kujua kuwa hawana uhalali kisheria, na wakati mwingine kumuondoa mjane kwa madai kuwa hana haki ya kuishi katika nyumba ya ndugu yao au kumiliki mali zilizoachwa.
Sheria haijampa mtu yeyote, awe mke au ndugu wa marehemu ruhusa ya kuanza kutumia mali kwa faida ya warithi kabla ya kufungua mirathi au kupata kibali kutoka mahakamani.
Ieleweke wazi kuwa mahakama ndiyo yenye mamlaka ya kugawa mali hizo na si wazee wa ukoo kama utamaduni uliojengeka katika baadhi ya jamii zenye mila kandamizi.
Taratibu za kufungua mirathi ikiwa hakuna wosia
Kawaida ikitokea kifo, taarifa ya kifo itolewe na kusajiliwa kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ndani ya siku 30.
Kikao cha wana ukoo kifanyike kumchagua au kumteua msimamizi wa mirathi na uamuzi huo uwekwe katika dondoo za maandishi.
Msimamizi aliyeteuliwa na wana ukoo apeleke maombi ya kupata barua/hati ya usimamizi wa mirathi mahakamani akiambatanisha:
• Cheti cha kifo.
• Dondoo za kikao cha wana ukoo kilichomteua kuwa msimamizi.
Mahakama itatoa taarifa kwa kubandika katika ukuta wa mahakama au gazetini juu ya maombi ya usimamizi wa mirathi na kutoa muda wa siku 90 kuruhusu yeyote kutoa pingamizi kama ana sababu za kufanya hivyo. Kama hakuna pingamizi basi mahakama itatoa barua ya usimamizi wa mirathi kwa mwombaji. Msimamizi wa mirathi hugawa mali ndani ya miezi sita na hatimaye kurejesha mahakamani nakala ya fomu inayoonyesha jinsi mgawo ulivyofanyika na kutiwa sahihi na kila mrithi. Kisha mahakama itafunga jalada.
Barua ya kuomba usimamizi wa mirathi lazima itaje kwanza familia ya marehemu na anwani zao na ndugu waliokuwa wakimtegemea; idadi na aina ya mali iliyoachwa; juhudi zilizofanyika kuhakikisha kwamba hakuna wosia ulioachwa na maelezo kuhusu maskani yake.
Hata hivyo, endapo kunahitajika kufungua mirathi, ni vizuri kwenda mahakamani kupata fomu maalumu ya kujaza.
Mtu anaweza kufungua mirathi katika Mahakama ya Mwanzo, Wilaya au ya Hakimu Mkazi.
Maombi ya usimamizi wa mirathi lazima yaeleze bayana juu ya kiasi na aina ya mali iliyoachwa na marehemu; majina na anwani za warithi; sehemu atokayo marehemu na mahali mali zilipo (hii ni muhimu kwani husaidia kuamua ni mahakama gani stahiki inaweza kupokea maombi ya ufunguzi wa mirathi).