Mtu adilifu anatengeneza kitu iwe kwa kuunda, kurekebisha kilichoharibika au kisichofaa kwa matumizi, ili kifae.
Mtu dhalimu anavunja, anaharibu au anashusha hadhi ya kitu kilichotengenezwa. Anabomoa.
Watu wawili hawa kila mmoja ana uhuru wa kuwaza, kutoa mawazo yake kufanya au kutofanya kitu au jambo kutokana na fikra zake au za wenzake. Katika utaratibu huu anajiwekea kanuni au sheria ya kutawala mwenendo wa maisha yake.
Katika utaratibu huu anaweza kuchukua tabia ya kutengeneza au kubomoa. Tengeneza na bomoa ni matendo mawili yasiyokwenda pamoja. Tengeneza inaleta maendeleo na bomoa inaharibu maendeleo. Daima watu waungwana wanataka maendeleo na mabadiliko katika maisha yao.
Maelezo haya hebu yapeleke na kuyatafakari katika kaya yako, ukoo wako, kabila lako na taifa lako; bila kuacha jumuiya yako ya mchezo, siasa au dini. Je, yupo au hayupo mtu adilifu au mtu dhalimu? Akili kichwani mwako. Mwanadamu anapaswa kuyatambua na kuyakabili mazingira yake.
Taifa letu hivi sasa limekumbwa na mabishano ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ndani na nje kwa sababu waadilifu hawakubaliki kwa wadhalimu. Nao wadhalimu hawatakiwi mbele ya waadilifu. Ukiwauliza kila mmoja atakuambia ana
uhuru wa kusema na kufanya.
Unasema nini? Unatenda nini? Unachosema na unachotenda kinatengeneza au kinabomoa? Kufikiri unatengeneza kumbe unabomoa, unavunja nia na malengo ya watu katika kujiletea maendeleo ya taifa lenu. Mwili unatengenezwa na chakula, ambapo nyumba inajengwa na matofali na taifa linajengwa na watu.
Wala usidhani kufanya hivi unakomoa, hapana. Inakubidi kufikiri kwa makini kwanza matokeo ya kutengeneza na kubomoa, kabla ya kusema na kutenda. Hekima hii ikitawala akili yako utatengeneza mambo mema.
Taifa letu hivi sasa limekumbwa na mabishano yenye hoja, maswali na majibu kuhusu misimamo ya kiitikadi ya vyama vya siasa, maendeleo ya kiuchumi ya nchi na ustawi wa jamii kati ya chama kinachoshikilia dola na vyama vinavyogombea kushika dola hapo baadaye penye majaliwa.
Kushika dola kidemokrasia ni kupata ridhaa ya umma wa wananchi; si wananchi wachache, ingawaje wachache hawa wanayo haki ya kusikilizwa mawazo yao. Si uhuru wa mawazo ya kutusi, kutisha na kukejeli.
Wanapofanya hivi hawatengenezi, ila wanabomoa misingi ya umoja, haki na usawa.
Misingi hii ya umoja, haki, usawa na mshikamano ndiyo inayoleta na kujenga utaifa, maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Taifa linapata kuwa imara katika uchumi, ustawi wa jamii, usalama na amani. Wananchi wanakuwa nao huru na kufurahia maendeleo yaliyopatikana.
Huu si wakati wa kuzozana, kushindana kwa hila za ugomvi, chuki na unafiki, ni hatari kisiasa. Havitajenga bali vitabomoa. Ni wakati wa kufanya kazi, kulinda nchi yetu na kudhibiti mali zetu za taifa. Tukumbuke na kuzingatia, siasa ni maisha katika taifa lolote asili yake ni demokrasia.
Bado ninarudia kusema, hatuwezi kuwa na Bunge huru, Mahakama huru, asasi huru za kiraia, tume huru ya uchaguzi na vyombo vya habari huru iwapo Watanzania wanaotaka hivyo katika vyama vya siasa, viongozi wa kijamii na wanaharakati hawapo huru katika mioyo yao.
Natambua ukweli, moyo wa mwanadamu una sifa nyingi, ikiwemo ya kupenda kitu au jambo kutokana na uzuri wake au ubora wake, na kufuatiwa na tamaa ya kupata hamu ya kutengeneza kitu au jambo. Lakini katika hili la taifa, tujaze mioyo yetu masilahi ya nchi kwanza.
Tusiuendekeze moyo utakavyo, kwa sababu una tamaa ya kufanya mazuri na mabaya ili kukidhi haja zake. Haja ya umma wa Watanzania ni maendeleo ya taifa si kubomoa maendeleo yaliyopatikana. Tutafakari.