Toleo lililopita tuliishia katika aya isemayo: Akaichukua na kuipokea kisha akaiweka sikioni: “Haloo!’’ Sauti akaifahamu kuwa ni ya profesa mwenzake. “Mbona sikuoni, hauko kwenye baraza mwaka huu?’’ Profesa baada ya kusikia hivyo akashituka: “Kwani kuna baraza la mitihani gani hapo?’’ aliuliza profesa, maana alikuwa hajui kilichokuwa kikiendelea. Sasa endelea…

“Juma lijalo tunaanza mitihani ya majaribio, tuko kwenye kupanga na kuandaa.” Profesa aliulizia kuhusu jina la Noel. “Niangalizie jina la kijana mmoja anaitwa Noel, anatoka nchini Tanzania, amepangiwa kwa profesa gani?’’ Kumbe profesa huyo huyo ndiye aliyekuwa akisimamia kitivo cha Habari na Mawasiliano, akakumbuka jina hilo ni kama aliliona katika orodha ya majina yake.

“Jina hilo kama ninalo!’’ alisema huku akiangalia katika kompyuta yake. “Kwani unasimamia watu wa kitivo gani?’’ Profesa mwenzake akamjibu: “Kitivo cha Habari na Mawasiliano.’’ Aliposema hivyo profesa akajua ni kweli jina la Noel liko kwa profesa huyo. 

“Kuna kijana anatoka Afrika anaitwa Noel, ninajua utakuwa unamsimamia, naomba umpe ushirikiano mzuri.’’ Waliongea mambo machache kidogo kisha wakakata simu na profesa akarudi kulala kwa kuwa alikuwa na usingizi mzito.

Noel alikuwa amelala usingizi mzito akiota ndoto akijiona akiwa sehemu ambayo haifahamu. Akitazama nyuma anaona watu wenye rangi sawa na ya kwake, pembeni anaona mahema makubwa watu wakiwa wanatoka ndani ya hayo mahema wakionekana wenye huzuni, waliokosa tumaini, wakiwa wamekonda, wengine wakiwa wameambatana na watoto wao wakitoka katika yale mahema. 

Akatokea mtu mbele yake Noel akamwambia: “Twende upande wa kule ukawaone,’’ alisema mtu yule ambaye naye pia alikuwa ana asili ya Afrika kwa muonekano. Noel akaona akiambatana naye wakafika sehemu wakakuta watu wakiwa wamekaa chini nyuso zao zikionekana kukosa tumaini.

“Dah! Sasa kwa nini wako hapa?’’ aliuliza Noel, kisha yule Mwafrika mwenzake akamjibu: “Maisha ya Afrika yamewashinda, ukitoa taarifa hakikisha unagusa pia maisha halisi ya watu wa Afrika’’ aliongea kwa kumsisitiza. “Sitaacha hata kitu kimoja,’’ alisema. Noel akashituka kutoka usingizini, akainuka kutoka kitandani, akafikiria juu ya kile alichokiona ndotoni mwake. Hakujua ilikuwa ni ndoto iliyokuwa ikitafsiri nini. Kwa kuwa usingizi ulikuwa umemtawala alirudi kulala.

Asubuhi yenye tumaini kwa Noel

Baridi ikiwa imeshika hatamu katika mji wa Moscow. Noel aliwahi kuamka, alikuwa mezani akiumiza akili yake juu ya kitabu alichokuwa akiandika. Akawa katika hali ya kufikiria isivyokuwa kawaida.

“Dah! Halafu sijasali leo,’’ alikumbuka Noel kisha akafungamanisha mikono yake na kufumba macho tayari kwa kusali. Noel japokuwa alikuwa si mtu wa kuonyesha mbele za watu kwamba anasali sana, lakini alikuwa ni mtu aliyekuwa na imani thabiti ya kujitegemeza kwa Muumba wake. 

Akaanza kusali kimoyo moyo bila kutoa sauti, wakati alipokuwa akisali Meninda naye alikuwa chumbani kwake akibeba funguo zake za gari ili kuelekea kazini. Mariana naye siku hiyo alikuwa ana kipindi asubuhi chuoni.

Profesa yeye alikuwa ameamka lakini alikuwa bafuni akioga. Mariana alipokuwa chumbani ahadi yake ya kuondoka na Noel ili kwenda kumtambulisha kwa mhadhiri mwenzake bado haikufutika akilini mwake.

“Nikitoka hapa ninywe chai tuondoke na Noel,’’ alikuwa akiongea mwenyewe huku akipanga vitabu vyake vya kufundishia na kuweka katika begi lake, Noel alikuwa amezama katika uhalisia wa maombi.

“Eeeh Mwenyezi Mungu nakuomba uilinde familia yangu, najua niko mbali nayo lakini wewe Bwana hautawapungikia kwa jambo lolote,’’ alikuwa ametulia akiwa anaomba. Alipokuwa akihitimisha maombi mara Mariana naye akawa amefika sebuleni, alipoangaza macho yake mezani, akamkuta Noel akiwa amekaa, daftari lake likiwa mbele akiwa anaandika. “Noel unawahi kuamka lakini ndivyo ilivyo kwa watu wenye mwelekeo wa maisha yao huwa wako makini kuamka mapema,’’ alisema Mariana akiwa mwenye tabasamu.

Profesa naye akawa amemaliza kuoga na kujiandaa, Meninda akatoka sebuleni kisha akawakuta Noel pamoja na Mariana ndugu yake. Alijua walikuwa wakiongea kuhusu uandishi. “Mariana unaondoka na Noel au?’’ aliuliza kabla ya yote Meninda.

“Ndiyo, nilipanga tangu jana, leo tutaondoka wote,’’ Meninda alikuwa si mtu wa kuongea sana kama ilivyokuwa kwa Mariana. “Sawa, Noel mimi ninakwenda kazini,’’ aliongea Meninda akiwa mwenye haraka. “Sawa dada Meninda uwe na kazi njema.’’ 

Mariana alipokuwa akiongea na Meninda, Noel alijua moja kwa moja ataondoka na Mariana. “Noel ngoja tunywe chai kwanza halafu tutaondoka.’’ Noel akamkubalia huku akiwa anaandika kitabu chake. Mariana akaondoka na kwenda moja kwa moja jikoni.

Noel akiwa anaandika alikumbuka alivyokuwa akihangaika katika harakati zake za uandishi alikutana na binti aliyekuwa akisoma chuo cha biashara jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania kiitwacho College of Business Education. Binti huyo alikuwa akisoma ugavi na manunuzi katika ngazi ya cheti.

Akakumbuka alivyokutana naye alivyomwangalia kwa macho ya dharau na maneno machafu, hii ilikuwa baada ya Noel kumwambia yeye ni mwandishi. “Wewe mwandishi gani? Huoni waandishi wengine wanapendeza?’’ alizungumza binti yule kwa madoido na kujikweza kwingi.