Siku chache baada ya Gazeti la JAMHURI kuchapisha habari za uchunguzi kuhusu ulegelege wa Mamlaka ya Vitambulisho Tanzania (NIDA) kushindwa kufanya kazi ya kutoa vitambulisho vya uraia inavyotakiwa kutokana na kuharibika kwa mitambo na hujuma za baadhi ya watumishi, Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, amelisambaratisha kundi lililounda mtandao wa hujuma ndani ya mamlaka hiyo.

Mambo mengi yaliyokuwa yamekwama, ikiwamo stahiki za watumishi, mfumo wa kifamilia kuamua watakalo kwa kuwaonea wafanyakazi, vitambulisho kutolewa kwa maelekezo na mengine ya aina hiyo, sasa yameanza kudhibitiwa, JAMHURI linathibitisha.

“Asante sana JAMHURI. NIDA ni taasisi muhimu kwa maendeleo ya taifa letu. Kwa masilahi ya familia moja au mbili, mamlaka hii ilikuwa inakufa. Mitambo ya kutengeneza vitambulisho imeharibika, haitengenezwi, wanafamilia wanaamua la kufanya ndani ya NIDA kama vile ni kikao cha harusi, wananchi hawapati vitambulisho, masilahi ya wafanyakazi yanapuuzwa, watu wanapaswa kusafiri kwenda kutatua matatizo mikoani wanakataliwa, lakini baada ya ninyi kuandika habari, tumeshangaa.

“Mkurugenzi wa (cheo kimehifadhiwa) alikuwa anatamba kila kona kuwa yeye ni Usalama wa Taifa. Akawa anasema hata wafanyakazi wafanye nini kauli yake ni ya mwisho, haiwezi kuhojiwa. Mke wake akawa anachapisha vitambulisho hadi kwa wageni wasio Watanzania anaagiza wapewe wakiwamo wale Waarabu saba ambao alitumia password (nywila) za wafanyakazi wenzake kuzalisha vitambulisho hivyo bila idhini ya watumishi husika.

“Sisi tunavyofahamu, Idara ya Usalama wa Taifa ni chombo nyeti. Kina heshima kubwa. Mtu hawezi kukitumia kuweka nchi rehani. Hata tulikuwa tunashangaa, huwa Usalama wa Taifa hawajitaji, sasa huyu ndugu akawa anajitaja, basi tukajua ni usalama feki, ila ilivyokuwa hachukuliwi hatua yoyote, tukajua labda ni kweli, ila tukasema kama ndivyo, basi usalama umeharibika. Unauza nchi, kumbe siyo bwana. Baada ya habari yenu, huyu mkurugenzi amehamishwa, amerudishwa Utumishi.

“Hata huyo mkewe aliyehamishiwa huko (jina la taasisi limehifadhiwa) waliposikia habari zake za kutoa vitambulisho kwa Waarabu, wamemshusha cheo kutoka Meneja Utumishi kuwa mtu wa mapokezi,” mtoa taarifa ameliambia JAMHURI.

JAMHURI limefuatilia habari hizi na kubaini kuwa wafanyakazi zaidi ya 10 wamehamishwa kutoka vitengo vya NIDA na kuhamishiwa mikoani, huku wengine wakiondolewa kabisa NIDA na kupelekwa katika idara nyingine za serikali.

Waziri Simbachawene amezungumza na JAMHURI kwa ufupi, akasema: “Mimi ninacholenga ni kuisafisha NIDA na kuona NIDA inatoa vitambulisho kwa Watanzania wasiteseke. Kuna kikundi kilijenga mfumo na kuuteka uongozi wa juu… ila hawa wote tunawadhibiti kwa masilahi mapana ya taifa letu.”

Mwandishi alipombana Waziri Simbachawene kwamba ilitokeaje uongozi wa NIDA ukashindwa kuwabana watumishi hao waliojijengea himaya hadi mifumo ikaharibika, alisema kwa ufupi: “Nimebaini yule mzee (Mkurugenzi Mkuu, Dk. Arnold Kihaule) hana shida. Alijikuta amebanwa na mtandao.”

Wiki iliyopita, wafanyakazi wa NIDA wameliambia JAMHURI kuwa Dk. Kihaule ametembelea kituo cha Kibaha ambako ni ‘jiko’ la kuzalisha vitambulisho akataka wamweleze matatizo yao.

“Kwa kweli asanteni JAMHURI, tulishangaa kuona Mkurugenzi Mkuu, Dk. Kihaule aliyekuwa anatupuuza akija hapa Kibaha na kutwambia tuseme matatizo yanayotukabili ayatatue. Saa chache baadaye watu wakaanza kupigiwa simu waende makao makuu wakachukue posho na barua za kusafiri kwenda mikoani kufanya kazi, suala tulilokwishalisahau. Yaani kwa jinsi walivyokuwa wanasema unaona mtumishi anabembelezwa kusafiri, tukasema hii ni kazi ya JAMHURI, hongereni,” amesema mtumishi mwingine.

Wiki tatu zilizopita Simbachawene aliwaita Dodoma viongozi wa NIDA akataka wampe maelezo ya kina juu ya malalamiko ya wafanyakazi na ununuzi wa mitambo ambayo haifanyi kazi hadi sasa.

Hatua hiyo ilikuja baada ya JAMHURI kuchapisha taarifa likionyesha kuwa NIDA wameamua kununua mashine mpya mbili za kuchapa vitambulisho kutoka Ujerumani, lakini kutokana na kupuuza ushauri wa wataalamu mashine hizo walizozinunua kwa Euro 3,304,650 (karibu Sh bilioni 8), pamoja na kuwa na uwezo mkubwa wa kila moja kuchapa vitambulisho 9,000 kwa saa haziwezi kufanya kazi kwa sasa.

Mkataba wa kununua mitambo hii miwili ulisainiwa Julai 22, 2019. Mkataba huu umesajiliwa kwa No. EA/061/2018-2019/HQ/G/01-LOT 3 wenye thamani ya Euro 3,304,650. Mwezi uliopita mmoja wa watumishi aliliambia JAMHURI: “Mkurugenzi Mkuu wa NIDA (Dk. Kihaule) aligoma kusikiliza ushauri wa wataalamu, matokeo yake sasa tumegota. Taarifa hii (JAMHURI linaonyeshwa taarifa ya kutisha) wameiandaa pale NIDA, lakini wanatumia hadi mablanketi kuhakikisha Rais (John) Magufuli haimfikii. Mashine zimefungwa tangu Novemba, 2019, lakini zimeshindwa kufanya kazi.

 “Mkurugenzi Mkuu wataalamu walimwambia kuwa kama tunanunua hizi mashine tunapaswa kununua na vifaa vyake, akakataa akasema zinunuliwe mashine vifaa vingine vitatumika hivi vinavyotumika katika mashine za zamani,” kimesema chanzo chetu.

Mashine hizo hazina vifaa vinavyohitajika. Kwanza, ni HSM ambacho kina neno siri (passwords) za kuendeshea mashine hizo. Pili, ni Compressor za kuendeshea mitambo hiyo; na tatu ni Servers kwa ajili ya kuhifadhi kumbukumbu za taarifa za Watanzania watakaotengenezewa vitambulisho.

Katika kikao hicho kilichofanyika Dodoma, inaelezwa kuwa uongozi wa NIDA ulidai kuwa mfumo wa kutengeneza vitambulisho umebadilika, hivyo nao iliwapasa kubadili teknolojia. Vigogo hao walimwambia Waziri Simbachawene wanafanya kila linalowezekana mitambo hiyo mipya ifanye kazi kabla ya mwisho wa Februari, mwaka huu, lakini hadi Machi 15, mwaka huu ilikuwa haijaanza kufanya kazi na wala hakuna dalili iwapo itafanya kazi ndani ya miezi mitatu ijayo.

Katika kikao hicho, Waziri Simbachawene aliwabana watendaji hao kuwa hata kama teknolojia wanayotumia imepitwa na wakati, inakuwaje wamenunua mashine ambazo hazijakamilika? “Amewaambia kwa mfano hicho kifaa cha HMS kinaweza kuwa kinasubiri vyombo vya usalama, sawa, lakini akawahoji hata compressor na severs zinasubiri nini? Hawakuwa na majibu… kwa kweli hakuwaficha, baada ya hapo akawaambia ni wazembe,” kimesema chanzo kingine.

Kwa vyovyote iwavyo, hatua ya kubadili teknolojia ya vitambulisho imetajwa kuwa italiongezea gharama kubwa taifa, kwani itabidi kuuacha mfumo wa zamani na kadi milioni 4.7 zilizopo itabidi ziharibiwe kama lilivyoandika gazeti hili hivi karibuni. 

Hadi sasa NIDA ina akiba ya kadi za vitambulisho zipatazo milioni 4.7 kwenye ghala. Baada ya Wataalamu kufunga mitambo hii, walionyeshwa kadi zilizopo, wakasema mitambo hii haitumii kadi hizo, inatumia aina nyingine.

Kadi hizi zimenunuliwa kati ya dola 2 na dola 2.5 au wastani wa Sh 5,000 kila kadi moja. Hii ina maana kuwa kadi 4,700,000 zilizopo kwa kuwa hazitatumika kwenye mashine hizi mpya itabidi zitupwe. Ukizidisha kadi hizo mara Sh 5,000 unaona serikali itakuwa imepata hasara ya Sh 23,500,000.

Hadi sasa NIDA wamesajili Watanzania milioni 21, na waliopatiwa vitambulisho ni milioni 5.9 tu, hivyo watu milioni 15.1 wanasubiri kupewa vitambulisho. Kuna kila dalili kuwa mfumo wa zamani ukiachwa ukaletwa mfumo mpya, basi itabidi hata watu milioni 5.9 waliokwisha kutengenezewa vitambulisho vya taifa nao itabidi wabadilishiwe vitambulisho, kwani utakuwa mgogoro mkubwa kuwa na vitambulisho vyenye mifumo miwili katika nchi moja.

Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha NIDA, Agnes Gerald Ngotolainyo, alipoulizwa na JAMHURI juu ya uhamisho wa wafanyakazi NIDA akiwamo mkurugenzi ‘kisiki’ aliyerejeshwa Utumishi, amesema: “Uhamisho katika Utumishi wa Umma unatekelezwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, na Taratibu za Utumishi wa Umma. Uhamisho umekuwa ukifanyika ndani ya taasisi ambapo mtumishi anaweza kuhamishwa kutoka kituo kimoja cha kazi hadi kingine. Mwenye mamlaka ya kuhamisha watumishi ndani ya taasisi ni Afisa Mtendaji Mkuu.

 “Pia, uhamisho ndani ya Utumishi wa Umma umekuwa ukifanyika kwa watumishi kuhamishwa kutoka taasisi moja hadi nyingine. Mwenye mamlaka ya kuhamisha watumishi kutoka taasisi moja hadi nyingine ni Katibu Mkuu Utumishi. Uhamisho huo huzingatia Kanuni ya 107(1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, Taratibu za Uendeshaji Utumishi wa Umma za mwaka 2003, Kanuni D.55 ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za mwaka 2009.”

Alipoulizwa kuhusu mitambo kutofanya kazi ilipofika mwishoni mwa Februari kama alivyokuwa ameuahidi umma Dk. Kihaule, akasema: “Uzalishaji wa vitambulisho unaendelea kwa kutumia mitambo iliyopo na vitambulisho vinaendelea kutolewa kwa wananchi. Aidha, ufungaji wa mitambo mipya unakamilishwa.”

Ingawa Ngotolainyo anatoa taarifa hiyo, taarifa za ndani zinasema kuna mkwamo. Mtoa taarifa anasema huenda ikachukua hadi miezi sita kuanzia sasa kupata mitambo hiyo, ila hata ikiweza kufanya kazi kuna mgogoro wa kisheria unaofukuta kati ya matumizi ya teknolojia ya zamani ya vitambulisho na hii inayodaiwa kutengenezwa na wahandisi wa ndani. 

Wafanyakazi wamemtaka Dk. Kihaule kuwa mkweli na kuuambia umma nini hasa kinachoendelea katika mfumo wa uzalishaji wa vitambulisho, kwani kuna hatari ya mfumo huu kufa kifo cha asili.