Zaidi ya wafanyabiashara 500 katika Soko la Buguruni katika Manispaa ya Ilala wamelikimbia soko hilo kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo kutokuwepo kwa usafiri wa uhakikika kwa wateja na miundombinu mibovu wakati wa mvua.
Akizungumza na JAMHURI hivi karibuni, Katibu wa soko hilo, Kambi Furahisha, amesema kuwa soko hilo lilikuwa na jumla ya wafanyabiashara 2,100, lakini idadi hiyo imepungua baada ya wengine kuondoka na kuhamia masoko mengine kutokana na changamoto zilizopo.
Kambi amesema kuwa changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA) kuondoa ruti za usafiri kutoka maeneo mbalimbali kuja sokoni hapo.
“Hii imesababisha wateja kupata shida ya usafiri kwa sababu hawawezi kufika sokoni kwa urahisi kama ilivyokuwa zamani. Wateja walipopungua baadhi ya wafanyabiashara wakalazimika kuondoka,” anaeleza.
Amesema wakati usafiri upo, watu wengi, wakiwemo wafanyabiashara wadogo wadogo walifika sokoni hapo kununua vitu kwa jumla na kuvisafirisha kupeleka kwenye magenge au masoko madogo madogo katika maeneo yao.
Amesema changamoto nyingine iliyowakimbiza wafanyabiashara ni ubovu wa miundombinu, hasa paa la soko ambalo linavuja wakati wa mvua.
“Ikinyesha mvua maji yanajaa ndani ya soko na hali inakuwa mbaya sana, wateja hawawezi kuja,” anasema.
Kwa upande mwingine, amesema wafanyabiashara nao hupata hasara, kwani bidhaa zao zinaoza kutokana na kujaa maji ndani ya soko.
Ameongeza kuwa wameshatoa taarifa kwa uongozi wa manispaa ambao waliahidi kushughulikia matatizo katika soko hilo lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika.
Abdallah Salum, mmoja wa wafanyabiashara katika soko hilo, amesema kabla LATRA hawajabadili ruti alikuwa akifanya mauzo ya Sh 100,000 kwa siku, lakini siku hizi huuza bidhaa za wastani wa Sh 30,000 tu kwa siku.