Daktari bingwa wa watoto katika Hospitali ya Regency jijini Dar es Salaam, Rahim Damji, ameanzisha mtandao wa kutoa ushauri na elimu ya afya ambao umewasaidia wazazi wengi kuokoa maisha ya watoto wao.
Akizungumza na JAMHURI hivi kaibuni, Dk. Damji, amesema mtandao huo umeshafikia miaka mitatu tangu uanzishwe na una washiriki zaidi ya 200.
Amesema lengo la mtandao huo ni kutoa bure elimu ya afya ya watoto. Mtandao huo unaundwa na watu mbalimbali lakini wengi wao ni wale waliowahi kutibiwa na daktari huyo.
Dk. Damji amedai kuwa ameamua kuanzisha mtandao huo ili kuwasaidia wazazi kukabiliana na changamoto za afya za watoto wao.
“Baadhi ya wazazi wamekuwa wakinipigia simu kutaka taarifa zaidi juu ya afya za watoto wao baada ya kuwatibu. Hilo limenisukuma kuanzisha mtandao huu ambao tunautumia kwa ajili ya kupeana taarifa za afya za watoto,” anafafanua.
Amedai baada ya kuona mahitaji makubwa ya wagonjwa kutaka ushauri hata nje ya kazi alishirikiana na muuguzi wake kuanzisha mtandao huo ambao umekuwa msaada mkubwa kwa wazazi.
“Tumeanzisha kundi la whatsapp ambako tunawasiliana na kupeana taarifa kuhusu matatizo ya watoto katika afya. Kundi hili linajumuisha wazazi ambao walikuja kutibiwa kwangu,” anasema.
Anasema kuwa pamoja na kutoa ushauri kwa wazazi wenye matatizo, pia mtandao huo hutumika kuendesha semina na mafunzo ya aina mbalimbali, ikiwamo lishe bora kwa watoto, jinsi ya kujikinga na maradhi kama pumu, namna ya kuishi na mtoto mwenye tatizo la pumu, kumkinga mtoto na magonjwa ya mlipuko ya kuharisha na kutapika, huduma ya kwanza kwa mtoto aliyepata ugonjwa wa dharura kama degedege, uzingatiaji wa chanjo, magonjwa ya mlipuo kama vile corona na magonjwa mengine ya watoto.
Mmoja wa wazazi walio katika mtandao huo, Jacqueline Crispin, amesema umewasaidia kina mama wengi kuweza kupambana na magonjwa mbalimbali ya watoto katika hatua za awali na kuwezesha watoto wao kupona haraka.
Amebainisha mathalani kuwa yeye mtoto wake alikuwa akisumbuliwa na magonjwa lakini baada ya kujiunga katika mtandao huo amekuwa akiokoa muda na fedha, kwani anaweza kushughulikia matatizo ya mwanaye bila kulazimika kwenda hospitali.
Muuguzi anayeratibu mtandao huo, Hilda Mapunda, anasema mtandao huo ulianza baada ya kuona kina mama wengi waliokuwa wakiwaleta watoto wao katika kitengo chao kuhitaji muda wa ziada kwa ajili ya ushauri wa daktari.