Na Mwandishi Wetu

Wanawake wajasiriamali zaidi ya 28,000 wamewezeshwa na serikali kupata mikopo yenye masharti nafuu kama sehemu ya kupambana na umaskini nchini na kuwashirikisha wananchi kikamilifu katika ujenzi wa taifa.

Wizara ya Fedha na Mipango ilisema wiki iliyopita kuwa mikopo hiyo yenye thamani ya karibu Sh bilioni 7.48 imetolewa mwaka huu wa fedha utakaokwisha tarehe 31, mwezi Juni.

Asilimia 52 ya fedha za mikopo hiyo zilitolewa kutoka mapato ya ndani ya halmashauri na kuwanufaisha wanawake wajasiriamali 14,295. Kiasi kilichobaki kilitolewa kupitia Benki ya Posta Tanzania (TPB) kupitia Dirisha la Wanawake kwa wakopaji 14,271.

“Serikali kupitia asilimia 4 ya mapato ya ndani imeendelea kutoa mafunzo na mikopo yenye masharti nafuu kwa wanawake wajasiriamali. Jumla ya Sh 3,890,123,401 zimetolewa kwa wanawake wajasiriamali 14,295 kutoka kwenye mapato ya ndani ya halmashauri,” Wizara ya Fedha na Mipango inasema kwenye taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2019/20.

“Serikali pia imeendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wanawake wajasiriamali kupitia Dirisha la Wanawake lililoanzishwa katika Benki ya Posta Tanzania (TPB) ambapo mikopo yenye thamani ya Sh 3,586,400,000 imetolewa kwa wanawake wajasiriamali 14,271,” taarifa inasema.

Wanufaika wengine wa mikopo hii inayolenga kuwasaidia wananchi kupambana na umaskini kupitia shughuli mbalimbali za maendeleo wamekuwa ni vijana kote nchini.

Serikali inasema katika mwaka huu wa fedha, mikopo yenye thamani ya Sh milioni 330.5 imetolewa kwa miradi 46 ya vikundi vya vijana katika halmashauri za wilaya 184 Tanzania Bara.

Katika kuwawezesha vijana pia serikali imeendelea na ufuatiliaji, tathmini na usimamizi wa SACCOS zinazowasaidia na kukamilisha mapitio ya Mwongozo Sanifu wa Stadi za Maisha kwa Vijana Walio Nje ya Mfumo wa Elimu.

Taarifa ya Wizara ya Fedha na Mipango pia inasema serikali imesajili wajasiriamali wadogo milioni 1.55 ambapo jumla ya Sh bilioni 31.02 zimepatikana. Mikoa iliyokuwa na idadi kubwa ya wajasiriamali waliosajiliwa ni pamoja na Dar es Salaam (asilimia 11.6), Arusha (asilimia 6.4), Mwanza (asilimia 5.3) na Mbeya (asilimia 5.2).

Wakati huo huo, taarifa hiyo inasema serikali imeendelea kutekeleza sera, mipango na mikakati mbalimbali ya kupunguza umaskini na kuboresha maisha ya Watanzania.

“Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi 2017/18, unaonyesha kuwa asilimia 8.0 ya watu wa Tanzania Bara wanaishi katika umaskini wa chakula ikilinganishwa na asilimia 9.7 mwaka 2011/12. Kwa mujibu wa utafiti huo, umaskini wa mahitaji ya msingi kwa mwaka 2017/18 ulikuwa asilimia 26.4 ikilinganishwa na asilimia 28.2 mwaka 2011/12,” taarifa inasema.

Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa asilimia 81 ya watu wenye umaskini wa mahitaji ya msingi wanaishi maeneo ya vijijini, wakati asilimia 16.1 wanaishi maeneo ya mijini na asilimia tatu katika Jiji la Dar es Salaam.