Wananchi makabwela wapika gongo wamezoea kuwakimbia polisi na viongozi wa dola. Si jambo la kawaida kwa wananchi wanaojihusisha na shughuli hiyo kuwa kwenye hali ya amani pindi wanapozingirwa na hao wakubwa ambao mara zote huwa pamoja na mgambo, polisi na maofisa wengine wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Lakini hivi karibuni mwiko huo umevunjwa. Tumeshuhudia tukio la aina yake. Wapika gongo kadhaa mkoani Mtwara walitembelewa na Mkuu wa Mkoa (RC) huo, Gelasius Byakanwa.
RC Byakanwa aliamua kwenda kiwandani kushuhudia namna gongo inavyotengenezwa. Awali, wananchi wale walionekana kuwa na wasiwasi, lakini RC huyo akawatoa wasiwasi. Akawauliza maswali kadhaa, na baadaye akaeeleza dhamira ya safari yake.
Akawahakikishia kuwa yupo pale si kuwakamata, bali kujionea namna wanavyotumia ujuzi wao kutengeneza pombe iliyopewa jina la ‘pombe haramu’. Kwake yeye, anaamini ile pombe si haramu, na kwamba uharamu huo ungejulikana tu endapo majibu ya maabara yangeonyesha hivyo. Akawaagiza wataalamu wa vipimo kuchukua sampuli ya gongo na kuipeleka kwenye maabara jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupata majibu ya kisayansi. Bila shaka lengo la mpango huo ni kupata ukweli wa yanayosemwa kuhusu gongo!
Uamuzi wa RC Byakanwa yawezekana ukawa umesukumwa na ukweli kwamba anakotoka kuna viwanda vingi vya gongo, ingawa yeye mwenyewe akiulizwa atasema ujuzi ulioko Kagera waliutoa mkoani Mara – hasa maeneo ya Musoma na Tarime. Wapo Watanzania wengi wenye nafasi kubwa kubwa katika jamii ambao masomo yao yaliwezeshwa kwa fedha zilizotokana na utengenezaji wa gongo.
Hoja yangu hailengi kukinzana na mitazamo ya kiimani kuhusu pombe. Pamoja na ukweli huo, pombe inaendelea kuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato kwa watu binafsi, kampuni na mataifa mbalimbali. Nimejaribu kudurusu baadhi ya vitabu vya historia kuona ni kwa namna gani baadhi ya vifaa au ujuzi wa Waafrika viliharamishwa.
Tunasoma kuwa ujio wa wakoloni katika Bara la Afrika ulikuwa na athari kubwa. Athari zake zingali zinaendelea hadi leo. Waafrika wenye ujuzi wa kutengeneza zana mbalimbali kama majembe, mapanga na kadhalika, ama walizuiwa, walikatwa mikono au waliuawa. Tunaambiwa walikuwapo Waafrika wengi waliokuwa na uwezo wa kutengeneza bunduki na silaha nyingine lakini walipigwa marufuku.
Kupigwa marufuku hakukuwa na maana nyingine isipokuwa kutoa mwanya kwa bidhaa za viwandani za wakoloni; lakini pia kuua vipaji vya Waafrika ambavyo kwa hakika vilikuwa zimefikia kiwango cha juu kabisa. Hadi leo kwenye orodha ya wavumbuzi, Waafrika wanashika nafasi ya juu.
Gongo inatengenezwa kisayansi. Ni ujuzi walioubuni Waafrika wenyewe katika kuhakikisha wanapata kinywaji chenye kuwafaa. Wakoloni kwa kutuaminisha kuwa kila linalofanywa na Mwafrika ni la kishenzi, wakaitangaza gongo kuwa ni pombe haramu.
Wakawazuia mababu na mabibi zetu kuitengeneza, kuisambaza na kuitumia. Wakaiharamisha kupitia kwenye sheria kandamizi. Kuanzia hapo ukawapo unyanyapaa kuanzia kwa watengenezaji hadi wanywaji wa pombe hiyo.
Licha ya kujitawala na kuwa taifa huru lenye watu huru, sheria hii kandamizi imeendelea kuwaumiza Waafrika. Wengi wameaminishwa kuwa gongo ni haramu, lakini Hennessy, Campari, Smirnoff, J&B na nyingine ni halali. Wataalamu wa hii pombe wameendelea kuwa katika kundi la wahalifu; jambo ambalo kwa kweli ni la uonezi.
Kuna hoja kwamba gongo ni hatari kwa sababu inaharibu afya za watumiaji. Ndiyo, pombe zinaumiza watumiaji. Hakuna pombe isiyokuwa na ‘side effect’ kwa mtumiaji. Hata bia ni hatari. Muhimu kwenye pombe ni kunywa kwa kiasi, lakini lililo muhimu ni kupata mlo kabla na baada ya kunywa.
Mazingira ya sasa ya utengenezaji wa pombe hii si rafiki kwa watengenezaji hadi kwa wanywaji. Kwenye vichaka kunakopikwa gongo hakutoi mwanya wa kuuzwa supu na viburudisho vingine. Watu wanakunywa pombe wakiwa ‘mguu sawa’ kuwakimbia mgambo, polisi na viongozi wa dola. Naamini nyama na viburudisho vingine vikiruhusiwa, wanywa gongo hawatadhoofu.
Hatua ya RC Byakanwa kupeleka sampuni kwa mkemia mkuu bila shaka itatuletea majibu ya kama ni kweli gongo ni pombe kali na hatari kuliko mamia kwa maelfu ya aina nyingine za pombe za viwandani.
Nampongeza RC kwa sababu amekuja na hoja ya kisomi ya kuondoa dhana iliyopewa taswira hasi na wakoloni kuwa gongo ni pombe haramu. Aina hii ya uamuzi iende hadi kwenye utengenezaji magobore na risasi. Haiwezekani tuwe na watu wetu wa kutengeneza vifaa hivi lakini tuendelee kuwapuuza huku tukiwafungulia kesi. Hawa ni wa kuwezeshwa tu.
Matumaini yangu ni kuwa majibu ya maabara ambayo tutayapata kutoka kwa RC Byakanwa yatakuwa chanya, na kwa maana hiyo huo utakuwa mwanzo wa kutunga sheria, kanuni na miongozo ya utengenezaji gongo nchini.
Hili si jambo la kuonea aibu, kwa sababu ni sayansi ya Kiafrika iliyopuuzwa kwa muda mrefu. Biashara hii ikiruhusiwa gongo itageuka kutoka kuwa laana na kuwa neema. Hongera RC Byakanwa.