Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tanzania Bara, Zitto Zuberi Kabwe, ametangaza rasmi nia yake ya kutaka kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), amesema anataka kuitumikia nchi hii akiwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano.

“Kwanza niseme wazi kabisa kuwa urais ninautaka… Ninaamini naweza kuwaongoza Watanzania wenzangu kuzikabili changamoto hizi,” anasema akimaanisha matatizo na mahitaji mbalimbali yanayoikabili Tanzania katika kipindi hiki na kijacho.

Tayari nia yake hiyo imewagusa na kuwakera kwa namna moja ama nyingine, viongozi wake wakuu akiwamo Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe; Katibu Mkuu wake, Dk. Wilbroad Slaa na hata mwasisi wa chama hicho, Mzee Edwin Mtei.

Wakati Mbowe ‘akiuma na kupuliza’ kwa kusema mbunge huyo ana haki ya kuonyesha nia yake kuhusu jambo hilo, lakini anahoji kuwa kwa nini aharakishe kiasi hicho kutangaza dhamira hiyo, Dk. Slaa anasema Chadema ndiyo itakayotoa uamuzi wa mwisho juu ya nani atagombea nafasi hiyo.

Anatamba kuwa yeye ndiye ‘kiongozi wa chama’ na kusema haoni jambo hilo kama linapaswa kujadiliwa sasa akidai “wakati wake haujafika”, kisha wote wakasema kilichopaswa kuzungumzwa ni uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki uliofanyika Jumapili ya juzi.

Zitto mwenyewe pia alilizungumzia mapema suala hilo alipotangaza nia yake ya kutaka kumrithi Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa kusema: “Naomba niseme kuwa pamoja na kutangaza nia hiyo, hivi sasa focus yetu ni uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki kwa kuwa ni lazima tulichukue jimbo hilo.”

Naam. Nampongeza rafiki yangu huyo kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kutangaza nia yake hiyo, jambo linaloshinda wengi wakiwamo wanasiasa wa siku nyingi, na kubaki wanasitasita kusema wakiogopa mashambulizi katika kile wanachokita ni ‘kuchafuliwa’.

Nilipokuwa darasa la kwanza wakati huo nikiwa na umri wa miaka minane, nilitangaza rasmi kwa wazazi wangu, walimu wangu na watoto wenzangu kwamba nikihitimu elimu yangu – tena wakati huo nikizungumzia darasa la saba tu – ilikuwa lazima nijiunge na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Watanzania (JWTZ), lengo ambalo wanaonifahamu vyema wanajua jinsi nilivyolitekeleza.

Nilikwenda jeshini nikiwa bado ni mdogo kiasi kwamba kila ninapopita mitaani na kombati zangu pale Dar es Salaam, wengi walikuwa wakinishangaa kuona ‘mtoto’ namna ile ni mwanajeshi, lakini hatimaye safari yangu ikanielekeza katika fani nyingine.

Nikiwa huko jeshini, nilipata mafunzo ya awali ya uandishi wa habari na kuwa mwandishi wa jarida la ULINZI, linalomilikiwa na JWTZ, lakini hatimaye nikaamua kuachana na jeshi ili nijikite zaidi katika fani hiyo katika upande wa kwanza, na pia nilitaka nipate fursa nzuri na kubwa ya kuongeza elimu katika upande mwingine.

Nilitaka niwe mwandishi wa habari maarufu zaidi nchini na ikiwezekana, kila anayesoma sana magazeti alijue jina langu hata kama hanifahamu sura, jambo ambalo nalo nikaweza kulitimiza vyema.

Nakumbuka namna watu walivyokuwa wakisongamana kuniangalia hususan maeneo ya Moshi, Arusha, Morogoro, Unguja na kila sehemu ninayokwenda, kipindi nilichokuwa ni mhariri wa gazeti la kila wiki la TAZAMA kuanzia mwaka 1994.

Nakumbuka watu walivyoshuka wakikimbia kutoka ghorofani katika ukumbi wa mikutano wa Zanzibar Hotel huko Unguja, baada ya kuambiwa kwamba nipo chini ninazungumza.

Kila mmoja alitaka aone nikoje ili anilinganishe na uzito wa maandishi ninayoandika na hasa katika safu yangu iliyoitwa ‘Kama ningekuwa mimi’, lakini walipofika chini pale mapokezi na kuambiwa “huyu ndiye Charles Charles”, wakabaki hawaamini macho yao!

Walitarajia kuwa ni jitu moja nene, refu na jeusi lenye macho makali, mekundu na sauti yake kali, sifa ambazo zote sikuwa nazo.

Nikiwa katika kilele hicho cha juu kabisa na kuasisi vitu vingi vinavyotumika hivi leo, katika fani hiyo ya uandishi wa habari, baadhi vikipigwa marufuku na Idara ya Habari (MAELEZO), na kupewa kila aina ya vitisho na baadhi ya maofisa wake, ghafla nikaingiwa na lengo jipya la kuwa mmoja kati ya viongozi wa kisiasa, jambo ambalo pia nimefanikiwa.

Nilitaka niwe kiongozi mwandamizi wa kisiasa, ili nipate nafasi nzuri ya kutoa kwa uhakika mchango wa mawazo na nguvu zangu kwa nchi yangu Tanzania, hivyo namshukuru Mungu kwa kunifikisha katika kila hatua ya maisha ninayotaka kwamba nifike.

Hayo ndiyo mafanikio kwa mtu anaponuia jambo na kuweka nia ya dhati kama anavyotaka kufanya Zitto mwaka 2015. Ndiyo maana nampongeza kwa kusema hadharani kuwa anataka awe Rais wa nchi hii; lengo ambalo kila asiyekuwa na wivu, inda, choyo au chuki yoyote ile hawezi kamwe kumshutumu katika hali yoyote.

Rais Kikwete naye aliweka nia ya kuitaka nafasi hiyo baada ya kumalizika tu uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, lakini alidhamiria kufanya hivyo huku akilazimika kusubiri kwa miaka 10 baadaye.

Nakumbuka swali aliloulizwa Februari 25, 2005 pale Kibaha na Mhariri Mtendaji wa gazeti hili, Deodatus Balile, alipotangaza rasmi kwamba anakwenda Dodoma kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo, lile alilotakiwa aseme angefanyaje endapo kura za maoni za ndani ya CCM zisingetosha tena kama mwaka 1995.

Akijibu swali la Balile, ambaye wakati huo alikuwa ni Mhariri Mkuu wa gazeti la TANZANIA DAIMA, Kikwete – huku akitabasamu kama ilivyo ada yake – alitamka maneno manne tu: “Hakuna kitu kama hicho.”

Waliombeza kwa jibu hilo walifanya kila wanavyoweza wakijaribu hadi kulipotosha kwa makusudi, wakiwamo waandishi wa habari, baadhi yao wakiandika hadi makala zenye kila aina ya kejeli, dharau na mashambulizi ya chuki.

Alibezwa na hata kushambuliwa na baadhi ya viongozi wenzake serikalini, wakati huo akiwa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Halafu alikumbana na adha hiyo pia kutoka ndani ya CCM na hata vinginevyo, lakini hakuonyesha kubabaika isipokuwa aliendelea kuiheshimu, kuithamini na kuisimamia kidete dhamira nzima ya kutaka awe rais wa nchi hii kama anavyotaka Zitto.

Alidhamiria kumrithi aliyekuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa, lakini hakusema hadharani kutokana na taratibu ndani ya chama.

CCM imeweka utaratibu usioruhusu wanachama kutangaza nia ya kuitaka nafasi hiyo wakati wa kipindi cha Rais aliyepo madarakani, yule atakayekuwa anatokana na chama hicho akiwa bado hajakaribia kumaliza muda wake.

Ni Mtanzania gani kati ya wafuatiliaji wa masuala ya siasa nchini aliyekuwa hajui kwamba Kikwete angejitosa kugombea urais mwaka 2005? Ukweli huo ndiyo unaonifanya nimpongeze Zitto, kisha niseme kuwa ameonyesha ukomavu mkubwa kabisa kwa kutuambia mapema kwamba anaitaka nafasi hiyo ya juu kuliko zote Tanzania.

Jambo tunaloweza kumwambia ni kuwa haruhusiwi kuanza kampeni iwe za ndani ya Chadema au sehemu nyingine, lakini amewapa wananchi fursa pana ya kuweza kumchunguza, kumjadili na kumpima kwa muda mrefu kujua udhaifu wake, ubora wake na kuamua kama anatosha ama hatufai.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu Na. 0713 676 000, 0719 822 244, 0762 633 244 na 0782 133 996