Nimewahi kudaiwa sana katika maisha yangu, na mara nyingi tamati ya usiku wa deni huwa kama saa inajikimbiza yenyewe. Hapo ndipo ninapokumbuka madeni mengi ambayo yamewahi kuniumiza sana kichwa, hasa yale ambayo nilikopa kwa ajili ya matumizi ambayo si ya kuzalisha.
Usiku wa deni haukawii kucha ni msemo mzuri sana kama haudaiwi na haujawahi kudaiwa. Unachekesha na unaweza kumcheka anayedaiwa, lakini ukweli usiopingika ni kwamba hauwezi kuishi dunia hii bila kuwa na madeni, yawe ya serikali au mtu binafsi, liwe deni la rafiki au ndugu, deni ni deni.
Tuna deni la kuletewa ugonjwa ambao wenzetu tayari umeshaanza na unawamaliza. Sisi huku tunasubiri kwa kuamini kwamba ugonjwa uko mbali. Tunasikiliza kama vile tatizo halituhusu kabisa, tunaamini tuko salama na kwamba siku ukija huo ugonjwa, basi tutakuwa na tiba na watu hawatapukutika. Huu ni usiku wa deni la ugonjwa wa corona, kukicha na kuna corona ndipo tutakapojua kuwa ugonjwa huo haukuwa mbali kabisa na ilibidi tuchukue tahadhari mapema.
Nina ushahidi na usiku wa deni haukawii kucha.
Kuna magonjwa mengi yalikuwa kama vile hayatuhusu kabisa miaka ya nyuma, yalipoingia ndipo tulipojua kuwa yanatuhusu na tukaanza kupambana kwa gharama kubwa ambayo hatukuimudu. Ninakumbuka ndui miaka hiyo, ninakumbuka homa ya matumbo, pepopunda na hatimaye ninakumbuka juliana miaka hiyo.
Ukiacha hayo maradhi mengine, juliana ilikuwa ikisikika huko Uganda na sisi tukabweteka sana huku tukijifaragua kama ugonjwa wa Waganda.
Kimuhemuhe kidogo kilikuja tuliposikia huko mipakani kuna watu tayari wameshapata juliana. Mara ghafla tukasikia umeingia mpaka mashariki ya kwetu huku Dar na kusini ya Mtwara, Nyanda za Juu Kusini na Magharibi ya nchi yetu.
Kamati za tahadhari zikawa hazina kazi tena bali kamati za kudhibiti na kuponya. Waliibuka waganga wengi wa uongo na kuzifilisi familia ambazo zilikumbwa na zahama hii.
Kila ninapokumbuka juliana naiona kama tatizo dogo ambalo mtu analipata kutokana na sababu ya msingi, tofauti kabisa na hii corona ambayo huhitaji kuingia katika uhusiano au ajali ya kugusana na kupakana damu. Corona ni suala la upepo unavuma kwenda wapi, corona ni suala la usafi uliokithiri, corona ni zaidi ya juliana. Tunapaswa kukaa ndani na kutoshikana mikono au kugusana ovyo.
Imetolewa tahadhari mapema ya kutoshikana mikono, lakini haijatolewa tahadhari ya kutopanda mabasi yaliyojaa na kufunga madirisha. Haijatolewa tahadhari ya matumizi ya vitu vya jumuiya kama sehemu ya kutolea fedha na fedha zenyewe. Tahadhari ya kukaa pamoja katika mikutano na misiba. Corona ni janga kubwa tunalosubiri usiku wa deni la ugonjwa.
Ninajua wako wenye akili za juliana, ugonjwa uko mbali na hawa ndio wengi wao hujisahau na kutenda yale ambayo ni katazo la maambukizi. Hawa ndio wale wenye nafasi za kuzuia usiku wa ugonjwa, hawa ndio tunaowaangalia kama msaada kwetu katika kipindi hiki cha usiku wa ‘maanani’.
Rai yangu kama mtu mwenye uzoefu na hizi penyenye za magonjwa au hatari yoyote ni kwamba unapodhani iko mbali, basi jua kuwa ipo jirani na wewe. Wananchi wengi hatuna elimu ya kinga bila kufundishwa kwa vitendo vya vifo. Tutakapoingia katika kundi la kuwa miongoni mwa mataifa yenye corona ni dhahiri kuwa tutakuwa tunaokotana kama nzige barabarani.
Naziomba mamlaka zinazohusika katika kudhibiti maradhi na afya zetu zifanye kila njia ya kuzuia usiku huu usiwe mfupi. Sisi ni watu tunaoishi kwa mazoea, sisi ni watu tunaoishi kwa kushirikiana, sisi ni watu tunaoishi kwa ubishi, sisi ni watu tunaoamini katika siasa kwa kila jambo, msiposhika nafasi yenu vizuri hata nyinyi hamtakuwa salama.
Maradhi yameanzia mahali ambapo watu wanajua maana ya usafi, watu wanajua maana ya kuchukua hadhari, kuna mazingira mazuri ya matibabu na kuwekeana karantini, kuna namna za kisasa katika kufikisha huduma za kijamii kwa watu wote walioathirika na wasio athirika. Tujifunze wanafanya nini kuukabili.
Mola tuepushe na usiku huu.
Wasalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.