Bei za jumla za mazao mengi ya chakula zilipanda kwa kiasi kikubwa mwezi Januari mwaka huu ikilinganishwa na mwezi uliotangulia kutokana na kuongezeka kwa mahitaji yake kwenye baadhi ya nchi jirani, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema.

Kuongezeka kwa bei hizo pia kulitokana na kupungua kwa uzalishaji wa vyakula hivyo katika baadhi ya mikoa humu nchini, hasa ile iliyoko Kanda ya Ziwa na Kaskazini wakati wa msimu wa 2018/19.

Mazao ambayo bei zake zilipanda ni pamoja na mahindi, mchele, maharage, uwele na viazi mviringo. Zao pekee la chakula ambalo bei yake haikupanda mwezi wa kwanza mwaka 2020 ni mtama.

Bei ya jumla ya mazao haya yote pia iliongezeka sana ikilinganishwa na bei zake kwa mwezi Januari mwaka 2019 na hata mwezi huo huo mwaka 2018.

Kwa mujibu wa Tathmini ya Hali ya Uchumi kwa Mwezi (MER) ya hivi karibuni, bei ya gunia la kilo 100 la mahindi iliongezeka kutoka Sh 87,591.8 mwezi Disemba mwaka jana hadi Sh 92,795.8 mwezi Januari mwaka huu.

Bei hiyo ya jumla ya mahindi ni karibu ongezeko la asilimia 90 ya bei ya zao hilo mwezi Januari mwaka 2019 ya Sh 49,011.1 kwa kila gunia. Kupanda kwa bei ya mahindi kumesababisha pia kuongezeka kwa bei ya unga, ambayo sasa hivi imepanda hadi Sh 1,800 kwa kilo.

Wakati bei ya gunia la mchele ilikuwa Sh 188,754.6 mwezi Disemba mwaka jana na Sh 189,486.2 Januari mwaka huu, Januari mwaka 2019 gunia hilo liliuzwa kwa bei ya Sh 160,282.9. 

Bei ya maharage ilikuwa Sh 218,789.3 Januari mwaka huu na Sh 161,710.6 Januari mwaka 2019 kabla ya kupanda hadi Sh 210,864.6 Disemba mwaka huo huo.

Januari mwaka jana bei ya jumla ya gunia la uwele ilikuwa Sh 74,328.7 ambayo ilipanda hadi Sh 104,842.7 mwezi Disemba na kufikia Sh 106,981.3 Januari mwaka 2020. 

Kilo 100 za viazi mviringo ziliuzwa kwa Sh 72,527.9 Januari mwaka huu ukilinganisha na Sh 80,484.7 na Sh 69,485.3 mwezi Januari na Disemba mwaka jana mtawalia.

Bei ya gunia la kilo 100 la mtama ilishuka kutoka Sh 136,845.5 Januari mwaka jana hadi Sh 130,428.3 mwezi Disemba na kufikia Sh 127,849.8 mwanzoni mwa mwaka huu.

Wakati huo huo, nafaka zinazohifadhiwa kwenye maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imepungua hadi tani 43,596.7 mwezi Januari mwaka 2020 kiasi ambacho ni cha chini katika kipindi cha miaka sita.

Kwa sasa NFRA ina maghala 34 yenye uwezo wa kuhifadhi tani 251,000 kwa wakati mmoja. Ili nchi iwe salama, NFRA inahitaji kuwa na maghala yenye uwezo wa kuhifadhi akiba isiyopungua tani 700,000.

Mara ya mwisho NFRA kuwa na shehena ya nafaka inayozidi tani 100,000 ilikuwa Januari mwaka 2016 ilipokuwa na tani 125,668 kwenye maghala yake. Kiasi cha chakula kwenye maghala hayo Disemba mwaka jana ilikuwa tani 52,498.1 ukilinganisha na tani 52,726.9 mwezi Novemba.

“Mwezi Januari mwaka 2020, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) uliuza tani 8,901.4 kwa wafanyabiashara, Programu ya Chakula Duniani na Idara ya Magereza.

Hii ilisababisha chakula kilichohifadhiwa na NFRA kufikia tani 43,597 mwishoni mwa mwezi Januari 2020 kutoka tani 52,498 zilizokuwepo mwishoni mwa mwezi uliotangulia,” Benki Kuu inasema kwenye MER ya Februari mwaka huu.