Nimeshtuka sana na kuingiwa wasiwasi kusikia eti yupo mbunge amediriki kuandika barua kwenda Benki ya Dunia kutaka zuio la fedha za maendeleo ya elimu hapa nchini.





Mbunge wa Kigoma Mjini, Zito Kabwe (kushoto) akila kiapo cha utii baada ya kuhitimu mafunzo katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa Mgambo mkoani Tanga mwaka 2013.

Nasema nimeshtuka kwa vile aliyetenda hivyo ninamfahamu kama ni askari wa Jeshi la Akiba katika nchi hii. Katika Bunge la 10 mwaka 2012, Zitto Kabwe, akiwa na wabunge vijana wenzake waliomba kwa hiari yao wapatiwe nafasi angalau kwa wiki chache tu kushiriki ujenzi wa taifa letu katika kambi ya JKT.

Walikuwa wabunge 22 waliojitokeza kuomba wakalihudumie taifa katika kambi za JKT wakidai kuwa enzi zao mafunzo ya JKT yalisitishwa. Lakini kwa kuwa wakati huo JKT ilikuwa imerejeshwa, wakaomba na wao wapate fursa ya kuhudhuria mafunzo hayo adhimu.

Kutokana na moyo ule wa uzalendo na ari ile waliyoionyesha bungeni, serikali iliwapatia fursa waliyoomba. Kwa mpango ule ulioitwa ‘mature age entry’ kama walivyofanya kina mzee Rashid Kawawa, mzee Aboud Jumbe, mzee Job Lusinde na Chief Adam Sapi mwaka 1968.

Nakumbuka waheshimiwa wale walipewa mafunzo ya wiki tatu hivi katika kambi mbalimbali za JKT. Zitto Kabwe na wenzake kadhaa walipangiwa kule Mgambo JKT, Kabuku, katika Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga. Ninakumbuka Halima Mdee na wenzake walipangiwa Ruvu JKT, Pwani. Wapo wabunge waliopangiwa Msange JKT, Tabora na wapo wabunge waliopangiwa Bulombora JKT, Kigoma.

Mafunzo yao yalianza Machi 5 na wakahitimu Machi 26, 2013. Waliitwa Operesheni miaka 50. Nilibahatika kwenda kuwapa somo pale Mgambo na Ruvu wakiwa makuruta.

Sasa, kwa ari waliyokuwa nayo wabunge wale na walivyoonyesha uzalendo na ushirikiano wao, usipoambiwa mtu usingeweza kutofautisha kuruta ni yupi – ni chama gani, wote pale walikuwa Watanzania wenye dhamira moja tu, ya kujenga taifa lao.

Machi 26, 2013 walikuwa wana – “pass out parade” (gwaride la kuhitimu mafunzo) na wakala kiapo chao cha utii kwa Rais wa Jamhuru ya Muungano wa Tanzania na serikali yake. Hapo waheshimiwa wote 22 wakawa ni askari wa akiba katika taifa letu. Kule kulikuwa ni kudhihirisha uzalendo wao kwa taifa letu. Wameonekana hivyo machoni pa nchi.

Sasa niliposikia Mbunge wa Hai, Dk. Godwin Mollel, anatoa hoja binafsi bungeni akimtaja Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini kuwa ameandika barua kupeleka Benki ya Dunia, mimi sikuelewa hata kidogo.

Kwanza, nikajiuliza, ni Zitto yupi, ni yule askari wa Mgambo JKT au Zitto mwingine? Ni yule aliyeongelea kwa uchungu mkubwa bungeni kuomba kuonyesha moyo wake wa uzalendo au siye? Amegeukia kuinanga serikali aliyoapa pale Mgambo JKT kuwa ataitumikia?

Ndipo ninauliza, hili jambo maana yake nini? Tukio lote hili sisi Watanzania tunalitafsiri vipi? Tendo la kuandika barua, tena kwa kutumia nembo ya Bunge tunalionaje? Hiyo nembo ya Bunge ni kila mbunge anaruhusiwa kuitumia? Hayo yote yananifanya nisielewe kilichotendeka hapa nchini. Hapo lazima ‘umafia’ umetumika. 

 Kutumia njia za umafia nadhani si halali kwa mzalendo yeyote nchini. Hebu tufikirie amani na umoja uliojengeka kwa miaka yote 58 hii, inawezekanaje mbunge wa kuchaguliwa azuie fedha za maendeleo katika nchi?

Kwanza nilikwenda kwenye kamusi ya Kiswahili Sanifu nijiridhishe na maneno mawili: moja ‘uzalendo’ na pili ‘uhaini’. Katika ile Kamusi iliyotolewa na taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), toleo la 3 kwenye ukurasa wa 630 nikakuta neno ‘uzalendo’ limetafsiriwa hivi: Hali  ya kuwa tayari kufia nchi yake, hali  ya kuwa mzalendo. Nikatafuta neno ‘uhaini’; nikakuta katika ukurasa wa 146 limetafsiriwa namna hii: 1.  Fanya tendo la kusaliti nchi, serikali au mfadhili wako. 2. Mtu anayesaliti nchi, serikali au mfadhili wake, muasi, msaliti mchi, serikali au mfadhili wake, mshiriki katika jambo baya, mdanganyifu.

Haya baada ya kujiridhisha na tafsiri za maneno haya mawili sasa nikawa najiuliza, Mheshimiwa Zitto Kabwe wa Mgambo JKT ni kweli ameigeuka nchi na taifa lake hata akaja kutenda hivi alivyotenda? Tendo hili kitaifa linatafsiriwa namna gani? Mtendaji anastahili kweli kuitwa mzalendo au aitwe mhaini?

Upo usemi hapa nchini au ipo methali isemayo “mvunja nchi ni mwananchi”. Hii inamaanisha mtu anayepinga maendeleo katika nchi yake yukoje? Kwani zile fedha zilizoombwa na serikali zisingetumika kujenga shule na mabweni kwa ajili ya wanyonge wa Kigoma?

Kwa uelewa wangu, mtu kufanya ujanja hadi kupata karatasi zenye nembo ya Bunge ni tendo la ‘uhaini’. Ni uhalifu. Pili, kuwa na moyo au dhamira ya kuvuruga maendeleo, ni tabia ya kimamluki ulimwenguni kote. Kwa vile mwenzetu huyu alishajiandikisha kuwa askari wa akiba baada ya kupitia yale mafunzo ya JKT na akala kiapo cha utii, basi kwa tendo lake hili tu inatosha kuitwa msaliti.

Katika kila nchi hapa duniani na katika kila taifa kunakuwa na raia wa aina mbili. Wapo raia kwa kuzaliwa kwao na wapo raia wa kuja kutoka nchi nyingine lakini wakaomba na kukubaliwa kuandikishwa kama raia wa nchi au taifa waliomo. 

Hawa ndio Ugiriki ya zamani waliwaita ‘aliens’. Enzi hizo kule Ugiriki, ma aliens kutoka Ujerumani, Italia, Uturuki na kwingineko hawakuruhusiwa kupiga kura na kuchagua viongozi kwa kuwa uzalendo wao haukuaminiwa na Wagiriki wazawa.

Basi kwa mtazamo namna ile, ‘aliens’ hawaaminiki. Hapo ndipo kinakuja kishawishi cha kuuliza ni kweli Zitto Kabwe ni Mtanzania kwa kuzaliwa au ni ‘alien’?

Wakati nikiwa na mawazo ya tukio lote hili, huku nikiwaza kuhusu uraia wa mwenzetu huyu, nikapata kusoma katika  mtandao mawazo kutoka kwa Baba Askofu Bagonza. Huyu ameandika mtandaoni hivi: “Serikali ikaomba mkopo Benki ya Dunia. Huyu kaandika barua Benki ya Dunia kulalamika na kushauri Benki ya Dunia usitolewe. Mwingine akakemia na kuhukumu kuwa waandika barua na kusema haya wanaiachafua nchi. Hili ni somo kamili la uraia darasa la saba; Civics – Kidato cha Tatu; History paper two Kidato cha Tano.”

Maoni haya ya baba askofu hayakuishia hapo tu bali aliendelea kuandika hivi: “Kwamba kuna tofauti kati ya Nchi na Serikali. Kuna tofauti kati ya Rais na Serikali. Kwa hiyo, waweza  kumkosoa Rais lakini usikosoe Serikali, na waweza kuikosoa Serikali lakini usomkosoe Rais.

Mungu wetu ni mkarimu sana. Ameumba watu na kuwapa hata utashi wa kumkataa yeye aliyewaumba. Hata kwa nchi moja, wapo watu aina mbalimbali. Kuna watu wanaweza kuipenda nchi wasiipende Serikali. Kuna watu wanapenda niandikayo lakini wananichukia mimi. Hali kadhalika kuna wanasiasa wengi wanapenda kura zetu, lakini hawapendi mambo yetu.”

Baada ya kusoma hayo katika mtandao nikawa bado sijafanikiwa kuuridhisha moyo wangu juu ya tukio hili.  Bado ninafikiria ulikuwa uhaini au ni mchezo wa kuigiza?

Hebu tukumbushane yale yaliyotokea siku zile za mwanzo mwanzo za Uhuru wetu. Mara baada ya TANU kupata Serikali ya Tanganyika, walitokea raia wa Tanganyika, wazawa na ‘aliens’, kutoipokea vema ile Serikali ya TANU.

Hawa raia wenzetu katika kule kutokuridhika kwao na Serikali ya TANU, wakawa na matendo hatarishi yaliyoelekea kwenye uvunjifu wa amani katika nchi. ‘Aliens’ walionyesha tabia ya kuwadharau raia weusi wazawa (tukiitwa Africans). Lakini na raia wazawa wengine wakawa wanainanga serikali kwa vile walijiona hadhi yao ilikuwa bora kuliko sisi wengine.

Mwalimu Nyerere hakuivumilia hali ile hata kidogo, maana ingeweza kusababisha kuvunjika kwa amani na umoja. Basi Serikali ya TANU ikaja na dawa iliyoitwa ‘mruturutu’ kukomesha kabisa hali ile isitokee tena.

 Wale ‘aliens’ wote (walikuwa Wazungu watano) walifukuzwa nchini mara moja. Adhabu ile iliitwa ‘deportation’ (kuondolewa nchini na kurejeshwa makwao). Ni adhabu iliyowashikisha adabu ‘aliens’ wote na wala hawakuthubutu tena kuichezea Serikali ya TANU tangu mwaka ule wa 1963 mpaka leo hii.

Lakini walikuwepo na wazawa kadhaa katika mikoa mbalimbali wasiokubaliana na Serikali ya TANU. Hawa nao walijaribu kuleta uchochezi pale walipoishi. Hawa wote nao serikali ilikuja na adhabu iliyoitwa ‘rustication’, yaani kuondolewa pale ulipozaliwa na kupelekwa kuishi mbali na kwako ndani ya Tanganyika. 

Ni wazi wasingeliweza kupelekwa nje ya nchi, kwa nani na kwa msingi gani? Hawa walikuwa ni Watanganyika kwa kuzaliwa, hivyo wana haki ya kuishi humu humu nchini.

Mbenna ni Brigedia Jenerali mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).