Taasisi mbili kubwa za fedha duniani zimepinga sera ambazo Zimbabwe imeamua kuzitumia kufufua uchumi wake.
Taasisi hizo, Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), zimesema Zimbabwe inahitaji kufanya mambo mengine mengi zaidi ya sera hizo iwapo inataka kufufua uchumi wake kwa kasi.
Kwa muda wa muongo mmoja uliopita Zimbabwe imepitia katika kipindi kigumu kiuchumi na kusababisha kupanda kwa mfumko wa bei kufikia tarakimu tatu, mishahara midogo na upungufu mkubwa wa bidhaa muhimu kama vile unga, mafuta na umeme.
Alipochaguliwa mwaka 2017, Rais Emmerson Mnangagwa, alileta matumaini akiahidi kufufua uchumi lakini hali imezidi kuwa mbaya.
Mnangagwa alichukua uongozi baada ya kuondolewa madarakani Robert Mugabe, ambaye aliiongoza nchi hiyo tangu ipate uhuru. Ilielezwa kuwa sera za Mugabe ndizo ziliiingiza Zimbabwe kwenye matatizo ya kiuchumi baada ya kuwaondoa walowezi waliokuwa wanaendesha shughuli za kilimo nchini humo, kwa maelezo kuwa walikuwa wanamiliki ardhi kubwa huku wenyeji wakiwa hawana ardhi kwa ajili ya shughuli zao. Taarifa iliyotolewa baada ya maofisa wa IMF kutembelea Zimbabwe, imesema Zimbabwe inashuhudia matatizo makubwa ya kiuchumi na kibinadamu huku uchumi mkubwa ukiwa umevurugika kabisa.
“Serikali iliyoingia madarakani baada ya uchaguzi wa mwaka 2018 ilikuja na ajenda ya kufufua uchumi mdogo na kufanya mabadiliko. Hili lilikubaliwa na IMF lakini mkakati huo haujazaa matunda, kwa sababu hakuna utekelezaji wake,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Mwaka uliopita Zimbabwe ilizindua sarafu yake ambayo ilianza kuuzwa kwa thamani ya 2.50 kwa dola ya Marekani lakini thamani hiyo imeendelea kuporomoka na sasa hivi inauzwa kwa 28 kwa dola moja.
Katika taarifa nyingine iliyotolewa wiki iliyopita, maofisa wa AfDB nao walikosoa jinsi nchi hiyo inavyoshughulikia matatizo yake ya kiuchumi.
“Wakurugenzi wa AfDB wamebaini kuwa licha ya matokeo yaliyoonekana, bado kuna tatizo kubwa la kutekeleza mabadiliko ambayo yaliahidiwa, hivyo kusababisha kiwango cha umaskini kuongezeka, hasa katika maeneo ya mijini,” inaeleza taarifa ya AfDB.