Wanaitwa nzige wa jangwani na mtu angeweza kuhisi kuwa wanastawi sana katika maeneo ya jangwani, lakini si hivyo. Nzige hawa ambao hivi sasa wanalitesa eneo la Afrika Mashariki wanastawi sana katika maeneo yenye mvua nyingi.
Kwa miezi kadhaa sasa nchi kadhaa katika eneo la Afrika Mashariki zimekuwa zikipambana na nzige hao ambao kuibuka kwao kumezua taharuki kubwa.
Tayari tahadhari imekwisha kutolewa kuwa janga hilo la nzige wa jangwani linaweza kusababisha upungufu mkubwa wa chakula. Tayari nzige hao wamekwisha kuharibu hekta kadhaa za mazao katika nchi za Kenya, Djibouti, Eritrea Somalia, Ethiopia, Yemen, Uganda na Sudan Kusini.
Tanzania, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zimelazimika kukaa katika mkao wa tahadhari kutokana na nzige hao kusambaa kwa kasi katika eneo hilo. Wataalamu wanaonya kuwa ni sula la muda tu kabla nchi hizi nazo hazijavamiwa na nzige hao, kwa sababu hivi sasa kuna mazingira mazuri kwa nzige kuzaliana kwa wingi na kusambaa kwa kasi.
Wakati tahadhari zikichukuliwa kuhusiana na nzige hao, kwa upande mwingine wataalamu wamekuwa wakihangaika kutaka kujua ni nini kimesababisha nzige hao kuibuka hivi sasa na tayari mwanga umeshaanza kuonekana.
Taarifa za awali za utafiti unaoendelea zinaonyesha kuwa janga hilo limetengenezwa kwa miaka kadhaa kupitia mifumo ya mvua katika eneo la Afrika Mshariki na Pembe ya Afrika.
Wataalamu wamebaini kuwa mabadiliko ya hali hewa katika eneo hilo inaweza kuwa sababu kubwa ya kuibuka kwa makundi makubwa ya nzige hao hivi sasa na kusambaa kwa kasi.
Kwa mujibu wa utafiti huo, mabadiliko ya hali ya hewa yaliyosababisha kubadilika kwa mifumo ya upepo baharini ndiko kumesababisha hali hiyo. Lakini haiishii hapo. Mabadiliko hayo ya mifumo ya upepo baharini kumesababishwa na shughuli za kibinadamu. Kwa hiyo, kimsingi, binadamu wenyewe wanaweza kuwa ndio waliosababisha janga hilo kuibuka hivi sasa.
Janga hili la nzige hivi sasa limeshitua sana kiasi kuwa baadhi ya vyombo vya habari wamelifananisha na yake yaliyoandikwa katika Biblia, kuhusiana na mapigo kumi ambayo nchi ya Misri ilipigwa na Mungu kutokana na mfalme wake kukataa kumruhusu Nabii Musa awaondoe Waisraeli waliokuwa watumwa nchini humo. Kati ya mapigo hayo kumi, mojawapo lilikuwa ni janga la nzige ambao walikuja kwa wingi sana na kufunika mashamba yote!
Watu wanafananisha hivyo kwa sababu makundi ya nzige walioibuka ni makubwa sana. Ukubwa wa makundi hayo ambayo tayari yameshatua katika nchi saba, haujawahi kuonekana awali.
Baadhi ya maeneo inaelezwa kuwa kuna makundi ambayo ukubwa wake unafanana na ukubwa wa baadhi ya majiji katika eneo hili.
Nzige hao tayari wameshaleta wasiwasi kuhusiana na usalama wa chakula katika eneo la Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, kwa sababu tayari wamekwisha kuharibu chakula kingi mashambani.
Kilichotokea
Tabia za nzige hao za kupenda kuishi katika maeneo yaliyopata mvua kubwa hivyo kuwezesha kuota kwa wingi kwa majani ambayo ndiyo chakula chao kikuu, ndiko kuliwafanya watafiti kugundua chanzo cha kuibuka kwa wakati huu. Wataalamu wanabainisha kuwa msimu wa mvua kubwa kuliko kawaida, zilizoambatana na vimbunga katika kipindi cha miezi 18 iliyopita katika eneo la Afrika Mashariki na Pemba ya Afrika ndicho chanzo kikubwa cha kuibuka kwa wadudu hao.
Wachunguzi wa masuala ya hali ya hewa wamebainisha kuwa ongezeko hilo la mvua na vimbunga kumetokana na kuongezeka kwa joto baharini katika eneo hilo. Hali kama hiyo ya ongezeko la joto baharini ndiyo ambayo pia imetajwa kuwa ni sababu kubwa ya moto mkubwa uliolikumba eneo la mashariki mwa Australia mwishoni mwa mwaka jana.
Kwa mujibu wa watalaamu, ongezeko la mvua katika eneo hilo katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu kilichopita, kulisababisha kuibuka kwa mabwawa makubwa ya maji katika maeneo mengi ambayo kwa kawaida yanakuwa makame. Mabwawa hayo ya maji yaliwezesha uoto wa asili kushamiri lakini pia kukawawezesha wakazi wa maeneo hayo kulima mazao ambayo yalistawi sana kutokana na kuwapo kwa maji ya kutosha.
Kwanza. Kuwapo kwa unyevunyevu wa kutosha ardhini kulitengeneza mazingira mazuri kwa nzige kuzaliana. Na kwa upande wa pili, walipozaliwa, wakakutana na mazingira ambayo yana nyasi nyingi. Hivyo wakazidi kushamiri kwa sababu walikutana na chakula kingi.
Mbaya zaidi, mabadiliko ya mifumo ya upepo baharini ikasababisha mikondo ya upepo ambayo inawawezesha nzige hawa kusambaa katika maeneo mengi kwa muda mfupi, wakisukumwa na upepo huo. Si ajabu kuwa katika kipindi kifupi tu nzige hawa wameweza kusambaa katika nchi kama saba hivi katika eneo hilo.
Kwa bahati mbaya, wataalamu wanaonya kuwa hali ya joto baharini inaweza kuendelea, hivyo kusababisha janga la nzige liwe gumu kulikabili, maana wadudu hao watazidi kuzaliana na kusambaa.
“Kama kutakuwa na ongezeko la vimbunga, ninaamini kutakuwa na ongezeko la wadudu hawa katika eneo la Afrika Mshariki na Pembe ya Afrika,” anasema Keith Cressman, mtaalamu mwandamizi wa masuala ya nzige anayefanya kazi katika Shirika la Chakula Ulimwenguni (FAO).
Nzige walivyoanza
Kwa mujibu wa Cressman, janga hili la nzige lilianza Mei 2018, wakati kimbunga Mekunu kilipopita katika eneo kubwa la jangwa ambalo halikaliwi na watu katika eneo la Peninsula ya Arabia, linalojulikana kama Empty Quarter, na kusababisha mabwawa makubwa ya maji katike eneo hilo. Kwa sbabu nzige wa jangwani huzaliana kwa wingi katika eneo hilo, inaaminika kuwa ndipo ambapo hawa nzige wa sasa walipoanzia.
Baadaye, mwezi Oktoba mwaka huo huo, kimbunga Luban kikalikumba eneo la Bahari ya Arabia, kikasambaa kuelekea magharibi na kusababisha mvua kubwa katika eneo la Empty Quarter, karibu na mpaka wa nchi za Yemen na Oman.
“Kwa kawaida nzige wa jangwani huishi kwa kipindi cha miezi mitatu. Baada ya kupevuka nzige wakubwa hutaga mayai ambayo kukiwa na mazingira mazuri yanaanguliwa na kutengeneza kundi kubwa mara 20 ya lile lililotaga mayai. Kwa njia hii, nzige wa jangwani wanaweza kuongezeka wingi kwa kiasi kikubwa sana katika kipindi kifupi tu,” Cressman anasema. Anabainisha kuwa vimbunga hivi vilivyotokea mwaka 2018, vilitengeneza mazingira ya nzige kuzaliana kwa wingi katika kipindi cha miezi tisa, na kuongeza idadi ya nzige katika ukanda wa Arabia mara 8,000.
Baada ya hapo nzige hao wakaanza kusambaa. Ilipofika majira ya joto mwaka 2019, makundi ya nzige yakavuka Bahari Nyekundu na Rasi ya Eden na kuingia Ethiopia na Somalia, ambako pia walikutana na mazingira mazuri ya kuzaliana kutokana na ongezeko la mvua ambalo eneo hilo lilipata kabla ya hapo.
Cressman anaongeza kuwa kuna uwezekano kuwa nzige hawa wangeishia hapo kama mambo yasingebadilika mwezi Oktoba mwaka jana ambapo Afrika Mashariki ilipata mvua kubwa za vuli katika maaneo mengi ambazo ziliungana na kipindi cha vimbunga mwezi Disemba. Matukio haya yakatengeneza mazingira mengine mazuri kwa nzige kuzaliana na kusambaa zaidi.
Nzige wakazidi kuzaliana kwa wingi na kuvamia maeneo mapya. Ilipofika mwishoni mwa Disemba wakaingia nchini Kenya, wakisambaa kwa kasi maeneo ya kaskazini na kati na ilipofika Januari mwaka huu Kenya ikawa inashuhudia janga baya kabisa la nzige kuwahi kuikumba nchi hiyo katika kipindi cha miaka 70.
Kujiandaa na hali mbaya
Ingawa watu wanadhani kuwa janga hili limekwisha kuwa kubwa sana, lakini Cressman anaonya kuwa bado hali inaweza kuwa mbaya zaidi ya ilivyo sasa. Anasema iwapo mvua zitaendelea kunyesha katika maeneo haya, upo uwezekano mkubwa wa nzige hawa kuendelea kuzaliana, hivyo kusambaa katika maeneo mengi zaidi.
“Kwa jinsi hali ilivyo, kuna uwezekano wa nzige hawa kuendelea kuzaliana katika mizao miwili zaidi,” anasema.
Anasema iwapo mvua zitanyesha, upo uwezekano kuwa hadi kufikia Juni, idadi ya nzige itakuwa imeongezeka mara 400 zaidi ya ilivyo leo, hivyo kusababisha majanga makubwa zaidi, hasa katika suala la usalama wa chakula na malisho ya wanyama.
Wataalamu tayari wameshaonya kuwa eneo la Afrika Mashariki na Pemba ya Afrika linakabiliwa na uhaba wa chakula kutokana na janga la nzige hao. FAO inaeleza kuwa zaidi ya watu milioni 13 katika nchi za Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya na Somalia wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula huku watu milioni 20 wengine nao wakiwa hatarini kuingia katika janga hilo.
“Lililopo hapa ni majira ya hali ya hewa. Wakati kipindi cha mvua za masika kitakapoanza kinaweza kukutana na nzige hawa na hapo hali itakuwa mbaya zaidi,” anasema Cressman.
Kwa kawaida maeneo mengi ya Afrika Mashariki, yakiwamo maeneo kadhaa Tanzania, yanapata mvua za masika kuanzia Machi hadi Mei kila mwaka. Wataalamu wanaamini kuwa hali hiyo inaweza kuleta mazingira mazuri ya nzige kuendelea kuzaliana na kusambaa mwaka huu.
Mabadiliko zaidi
Ingawa vimbunga hujitokeza kila mwaka, lakini ripoti zinaonyesha kuwa vimbunga vilivyotokea mwaka 2018 ambavyo ndivyo vilisababisha nzige kuanza kuzaliana kwa wingi katika Peninsula ya Arabia, vilikuwa si vya kawaida. Taasisi ya Uchunguzi wa Anga za Juu ya Marekani (NASA) inaeleza kuwa ni nadra sana kwa vimbunga kutokea katika Bahari ya Arabia. Eneo hilo linaweza kukaa miaka kadhaa bila kupata kimbunga.
Lakini mwaka 2018 ulikuwa mwaka wa vimbunga katika eneo hilo na hali ikazidi mwaka 2019, huku eneo la kaskazini mwa Bahari ya Hindi likivunja rekodi kwa kuwa na vimbunga vingi.
Hali hii ya vimbunga, hasa mwaka 2019, ikachangamana na hali ya joto katika Bahari ya Hindi na kusababisha mvua kubwa katika eneo la Afrika Mashariki.
Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa hali hiyo inaweza kuwa ya kawaida katika maeneo mengi kutokana na ongezeko la joto duniani. Ripoti iliyochapishwa mwaka 2014 ilionyesha kutokana na ongezeko la uzalishaji wa hewa ukaa, joto linaweza kuongezeka sana katika eneo la Bahari ya Hindi na kuharibu mifumo ya upepo katika maeneo mengi mara tatu zaidi ya wastani.
Utafiti mwingine wa mwaka 2018 ulibaini kuwa iwapo joto duniani litaongezeka kwa nyuzi 1.5 tu – kiasi ambacho dunia inaweza kukipita ndani ya muongo mmoja ujao – mabadiliko ya joto katika Bahari ya Hindi yatakuwa makubwa maradufu. Kwa mujibu wa utafiti wa awali, tayari kuna ushahidi wa mabadiliko makubwa ya mifumo ya joto katika Bahari ya Hindi.
Hali ya chakula
Wakati wanasayansi wakiendelea kuangalia mifumo ya hali ya hewa katika eneo la Afrika Mashariki, mashirika ya misaada ya kiutu nayo yameanza kujiandaa kukabiliana na matokeo ya janga hili la nzige na majanga mengine ya asili yanayotarajiwa kulikumba eneo hili kutokana na mabadiliko haya ya hali ya hewa.
Mwezi uliopita FAO iliomba wahisani kuchanga dola za Marekani milioni 76 ili kukabiliana na nzige na kuzuia janga hilo lisiwe baya zaidi. FAO imeomba fedha hizo ili kuwakinga wakulima na wafugaji katika nchi tano zilizoathiriwa na nzige.
Lakini jinsi nzige hao wanavyozidi kusambaa, kuna uwezekano kiasi hicho cha fedha kikawa hakitoshi.
“Nzige hawa wa jangwani wana uwezo wa kuruka umbali wa kilometa 150 kwa siku na jinsi upepo unavyovuma wanaweza kusambaa mbali zaidi. Kundi dogo tu lenye ukubwa wa kilometa moja ya mraba lina uwezo wa kula chakula kinachowatosheleza watu 35,000 kwa siku,” inasema FAO.
“Ndiyo maana tunaamini hali ni mbaya nchini Kenya, Ethiopia na Somalia ambako makundi makubwa ya nzige bado wanaendelea kushambulia mashamba huku kukiwa na mazingira mazuri ya nzige wengine kuzaliwa na kusambaa,” inaonya FAO katika taarifa yake.
Wanakula sana
Imekwisha kuelezwa kuwa janga la nzige nchini Kenya ni kubwa kuikumba nchi hiyo katika kipindi cha miaka 70 huku Somalia na Ethiopia zikiwa hazijaona janga kubwa kama hilo katika kipindi cha miaka 25 iliyopita.
Nchini Kenya makundi makubwa ya nzige ambao wakiwa angani wanaonekana kama wingu jeusi yanashuka katika mashamba na kula mahindi, miraa, maharage, mbaazi, malisho ya wanyama na mazao mengine yaliyopandwa na kuyamaliza katika kipindi cha saa chache tu.
Maeneo kama Mandera na Isiolo – kaskazini mwa Kenya na Tharaka Nithi katika nchi hiyo yalivamiwa tena na makundi ya nzige licha ya maeneo hayo kupuliziwa sumu ya kuua wadudu hao siku chache zilizopita. Ingawa serikali ilifanya kampeni ya kupuliza kemikali katika maeneo mengi, lakini hadi hivi sasa kaunti 18 kati ya 47 za Kenya tayari zimekwisha kuvamiwa na wadudu hao.
FAO imeshaonya kuwa takriban watu milioni 239 katika eneo la Afrika – Kusini mwa Jangwa la Sahara wanakabiliwa na njaa na utapiamlo, na zaidi ya watu milioni 20 wana hali mbaya ya chakula katika eneo la Pembe ya Afrika.
Makala hii imeandaliwa kutoka vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.