Nyaraka za uhamisho
Nayaraka za uhamisho zinajumuisha fomu namba 29 ijulikanayo kama fomu ya kusudio la uhamisho ambayo hueleza nia na lengo la muuzaji kutaka kubadili jina au kuondoa jina lake katika hati. Hii utaandaa nakala tatu.
Pili, ni fomu namba 30 ambayo hujulikana kama fomu ya ithibati ya uhamisho. Katika fomu hii muuzaji pia atakuwa anatoa idhini kwa mamlaka za ardhi kuidhinisha hiari yake ya kuachia umiliki kutoka kwake kwenda kwa mtu mwingine ambaye ndiye mnunuzi.
Mwisho ni fomu namba 35 ijulikanayo kama fomu rasmi ya kuhamisha umiliki ambayo ndiyo rasmi sasa hutumika kuhamisha umiliki kutoka kwa muuzaji kwenda kwa mnunuzi. Hii ndiyo humpa mnunuzi umiliki rasmi. Pia mkataba wa mauziano ni nyaraka ambayo itaambatanishwa hapa.
Kwa kiwanja au eneo ambalo halijaendelezwa (halijajengwa) huandaliwa kitu kiitwacho commitment bond kikiwa kama ziada ya nilivyotaja hapo juu. Fomu zote hizo pamoja na commitment bond hupatikana katika ofisi za wanasheria na huandaliwa na wanasheria.
Taarifa ya uthamini
Taarifa ya uthamini ni taarifa rasmi ambayo hutoa tathmini ya thamani ya eneo/jengo. Lazima umtafute mthamini ili afanye tathmini ya thamani ya eneo/jengo lako na taarifa hiyo iwasilishwe mamlaka za ardhi ili iweze kupitishwa na mthamini mkuu wa serikali katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Ukienda mamlaka za ardhi uliza, utawakuta wathamini ili wakufanyie kazi ya uthamini ninayoongelea hapa.
(c) Uraia
Sheria iko wazi kuwa wanaotakiwa kumiliki ardhi ni raia wa nchi hii tu. Hivyo unapotakiwa kupata hati ya umiliki lazima pia uthibitishe uraia wako. Hapa utatakiwa kuandaa nakala ya cheti cha kuzaliwa ambayo imethibitishwa na wakili au nakala ya pasipoti ambayo imethibitishwa na wakili au kama hauna hivyo vyote, basi yakupasa kuandaa kiapo.
(d) Ada
Ni muhimu pia unapofanya taratibu za kupata hati au kubadili jina kujiandaa na malipo ya ada za ardhi. Ada ziko za aina tatu, ambazo ni stamp duty fee, consent/approval fee na registration fee.
Sitaweka viwango vya ada hizi kwa kuwa vinabadilikabadilika mara kwa mara.
Mwisho, niseme kuwa ikiwa utajiandaa vema kwa haya, utapata hati kwa urahisi au kama unabadili jina utabadili kwa urahisi pia. Jiandae, epuka usumbufu.
Umuhimu wa kubadili jina
Sheria iko wazi kuwa mmiliki wa eneo au jengo ni yule ambaye jina lake linaonekana kwenye hati. Kwa kauli hii mnunuzi anatakiwa kufanya jitihada za haraka na za makusudi kubadili jina mara tu baada ya kununua kiwanja au nyumba.
Sikatai kuwa kunakuwa na mkataba wa mauziano, lakini lazima ieleweke kuwa mbele ya macho ya sheria, jina lililo kwenye hati lina uzito kuliko mkataba wa mauziano. Usiridhike kukaa na mkataba wa mauziano ikiwa haujabadili jina. Hii ni kwa ajili ya ulinzi wako na wa ardhi yako.
Utakapotokea mgogoro wa umiliki ikiwa haujabadili jina waweza kuwa katika hatari kubwa ya kupoteza, hasa kama mgogoro huo umeanzishwa na aliyekuuzia. Huu ndio ukweli na lazima tuonyane ili tuwe salama kwa mali zetu.
Lakini pia hata ukitokea mgogoro mwingine wowote wa umiliki, kuna mambo ndani ya sheria yataufanya kuwa mgumu kutokana na sababu tu kuwa ulikuwa haujabadili jina. Hapo sijaongelea faida nyingine za kubadili jina kama kukuwezesha kuitumia hati kukopa n.k.
Nishauri tu kwa ufupi kuwa unapojiandaa kununua nyumba au kiwanja, jiandae pia kubadili jina moja kwa moja. Hakikisha haya mawili yanakwenda pamoja.
Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.