Miaka mitatu iliyopita katika safu hii niliandika jambo linaloweza kuonekana dogo lakini lenye athari kubwa kwa mazingira na wanadamu. Linahusu wananchi katika Hifadhi ya Asili ya Amani kuzuiwa kusafirisha vipepeo nje ya nchi. Hii si haki.
Safu hii ya Mashariki ya Milima ya Usambara imeorodheshwa kama kituo cha kimataifa cha baioanuai ya mimea na inajivunia kuwa ya pili kwa kuwa na aina nyingi za mimea katika Bara la Afrika.
Ni kwa sababu hiyo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) halikusita kuitambua Amani kuwa Hifadhi ya Binadamu na Viumbe hai, mwaka 2000. Ina ukubwa wa hekta 83,600 zinazojumuisha misitu ya mvua na ardhi ya nyasi na miti ya uwanda wa chini. Ina sifa ya kuwa na mimea mingi iliyo katika hatari ya kutoweka (ikiwemo mimea yenye kutoa dawa mbalimbali); na ni makazi ya aina zaidi ya 13 za ndege wasiopatikana mahali pengine popote duniani.
Amani ndiyo chanzo kikuu cha maji kwa wakazi zaidi ya 300,000 katika mji wa Tanga, na wenyeji wa milimani wanategemea misitu hii kwa ajili ya shughuli zao za maisha, lakini sasa wakiwa wamebanwa na sheria za uhifadhi.
Amani ni urithi wa dunia kwa maana ya miti na viumbe wanaopatikana humo, lakini pia kwa kuwa msitu huu ni sehemu muhimu mno katika kunyonya hewa ya ukaa inayozaliwa duniani, hasa katika mataifa yenye viwanda vikubwa.
Ni kwa sababu hiyo, faida za Hifadhi ya Msitu wa Amani zinavuka mipaka ya Muheza, Tanga, Tanzania na Afrika. Kwanini tuilinde Amani? Kwa mujibu wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Milima ya Mashariki ya Usambara imejumuishwa katika ‘jamii inayohatarishwa kutoweka’ katika kitabu chekundu cha data za viumbe wasio na uti wa mgongo cha IUCN.
Spishi nyingi zisizo na uti wa mgongo za milima hii hazipatikani sehemu nyingine. Kwa mfano, spishi 41 za jongoo zimebainishwa na asilimia 8 ya spishi hizi hazipatikani sehemu nyingine. Asilimia 45 ya konokono wa nchi kavu waliopo ndani ya hifadhi hawapatikani sehemu nyingine wakati konokono wa aina ya Gulella ni asilimia 75. Spishi 15 kati ya 37 za vipepeo wa misitu ya milimani, mashariki mwa Usambara pia hazipatikani mahali pengine.
Hifadhi ya Asili ya Amani ni makazi ya spishi za wanyama wakubwa. Spishi 15 za vyura wa msituni na spishi 13 za reptilia zilizopo mashariki mwa Usambara hazipatikani sehemu nyingine Tanzania. Kadhalika, spishi nyingine za mamalia zimeorodheshwa kidunia kama viumbe waliopo katika hatari ya kutoweka – popo (Myonycteris relicta), nguchiro kijivu (Bdeogale crassicauda), Mindi (Cephalophus spadix), Panya-buku (Rhyncochyon petersi) – wakati spishi nyingine ndogo, Perere (Dendrohyrax validus vosseleri) zinaweza kuwa hazipatikani sehemu nyingine.
Wananchi wanaoishi karibu na hifadhi hii, kama walivyo watu wa maeneo mengine, wangependa kuzifaidia rasilimali misitu. Wangependa kulima, wangependa kukata na kuuza mbao, na wangependa kuchoma mkaa kwa dhana ‘hafifu’ ya kuondokana na umaskini. Yote haya yamezuiwa, isipokuwa kwa utaratibu maalumu unaoruhusiwa kisheria.
Wananchi wanaoishi ndani na kando ya misitu hii mizuri ya kuvutia, ni binadamu. Wana mahitaji yao mbalimbali ya kiuchumi lakini hawawezi kuyafanya hayo niliyoyasema hapo juu kwa sababu wanabanwa kisheria, na kwa kweli hilo halipaswi kuwa na mjadala. Lakini haiwezekani tu kuwataka wananchi hawa watulie kama hakuna njia mbadala ya kuwafanya waimarike kiuchumi.
Ndiyo maana mwaka 2003 kukaanzishwa Mradi wa Vipepeo Amani. Huu ni mradi wa kiuchumi wa kijamii unaoendeshwa na Kikundi cha Uhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG). Upo chini ya uangalizi mkubwa wa Hifadhi ya Misitu ya Amani (ANR), Idara ya Wanyamapori; na Halmashauri ya Wilaya ya Muheza.
Ulianzishwa kwa juhudi kubwa na mawazo kutoka kwa mshauri wa mradi, Theron Brown. Hadi unafungwa ulikuwa na wafugaji 156; ambao kati yao asilimia 43 ni wanawake. Unajumuisha vijiji sita katika Tarafa ya Amani, Muheza pamoja na wafugaji wapya kutoka wilaya za Korogwe (Tanga) na Same (Kilimanjaro).
Wanunuzi wakuu wa vipepeo ni Marekani, Uingereza, Uswisi, Ujerumani, Ufaransa na Australia. Hawa hutumia vipepeo katika majumba ya maonyesho ya vipepeo na matumizi mengine.
Mradi huu ulisaidia mno kuongeza kipato cha wananchi wanaozunguka hifadhi za Milima ya Usambara Mashariki; ulisaidia kuhifadhi baioanuai zinazozunguka milima hii; na kweli ulikuwa ‘shamba darasa’.
Kuanzia mwaka 2004 ambao ulikuwa wa kwanza kwa mauzo hadi mwaka 2015 uliwaingizia wafugaji shilingi zaidi ya milioni 500. Fedha hizo zimesaidia ujenzi wa nyumba bora, ada za watoto na matumizi mengi ya kila siku.
Asilimia 65 ya mauzo yote huenda moja kwa moja kama malipo kwa wafugaji wa vipepeo. Asilimia 28 zinatumika kuendeshea mradi. Asilimia 7 ya mauzo hugawanywa katika mfuko wa maendeleo ya jamii katika vijiji husika.
Wananchi wa Amani wameangukia kwenye wale wanaoumia baada ya serikali kuzuia usafirishaji viumbe hai nje ya nchi. Fikiria, vipepeo ambao maisha/uhai wao ni mfupi mno, wakisafirishwa nje ya nchi tunapoteza kitu gani kama nchi? Wananchi hawa wa Amani kuzuiwa kusafirisha viumbe hawa wanaowaandaa wao wenyewe kwenye mashamba yao kunamaanisha nini kama si kuwafanya wavamie na wahujumu Msitu wa Amani?
Waziri Mkuu Kasssim Majaliwa yumo ziarani mkoani Tanga. Akifika Muheza, wananchi mwelezeni kero hii. Kipepeo si ngedere wala tembo. Mwambieni serikali iwafungulie biashara hii ili mpambane na hatimaye muushinde umaskini. Hili waziri mkuu analimudu. Serikali isipofanya hivyo, maana yake inawaambia wananchi waumalize Msitu wa Amani.