Aliyemuibua Joseph Yobo hadi akawa mmoja wa wachezaji maarufu nchini Nigeria ni mama mmoja aliyekuwa akishughulika na ukuzaji wa vipaji vya watoto katika Jimbo la River.
Alitumia fedha zake mwenyewe kwa miaka mingi, lakini baadaye dunia ikaanza kumfahamu baada ya Joseph Yobo kupata nafasi ya kuchezea timu za Ulaya. Nchi za Afrika Magharibi zinatuzidi katika suala hilo la uwepo wa wingi wa wanafamilia ya soka. Wametapakaa katika mikoa na majimbo yao.
Wanahangaikia upatikanaji wa wanasoka bora ndani ya mwaka mzima. Hawatazami upi ni mwaka wa uchaguzi mkuu ndipo eti waanze kuthibitisha ni kwa kiasi gani mchezo wa soka ni muhimu kwao na kwa maisha ya watoto na vijana wao.
Msukumo wa wanasoka wa mataifa ya Afrika Magharibi kutaka kufanikiwa kimaisha kupitia kandanda, unasababisha uwepo wa wingi wa mashindano mengi, yenye lengo la kubadilisha hali nzima ya maisha ya wadau wa soka.
Tanzania inao wanafamilia ya soka, ambao huguswa na hamu ya vijana kutaka kufanikiwa kupitia mchezo wa mpira wa miguu. Yupo mdau wa soka ambaye aliweza kuendesha mashindano ya Mufindi kwa miaka 19, akitumia rasilimali zake mwenyewe!
Simba na Yanga
Ukizungumzia mechi yao ya Machi 8 kwa sasa ni sawa na kucheza ngoma usiyoijua, ila tutajua tu baada ya mchezo huo kumalizika na hapo ndipo utakapotoka na uchambuzi wa maana.
Swali kubwa unalojiuliza kwa sasa nje ya mechi hiyo ya mwishoni mwa wiki, je, timu hizi zina nia ya dhati kabisa kukuza vipaji na kuibua wachezaji wapya au kuwaangamiza?
Ni timu za furaha ya muda. Ole wake kocha achezeshe mchezaji kinda katika mchezo huo na asiyejulikana halafu timu ifungwe. Atajuta!
TFF nayo
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakiwa kama chombo chenye kutazamwa kwa ukaribu na wanafamilia ya soka nchini Tanzania, linapaswa kushuka mpaka kwenye ngazi za chini kabisa ili kuangalia ni kwa namna gani wadau kama huyo wa Mashindano ya Mufindi wanaweza kusaidiwa.
Siku zote mtafuta kura za wananchi kupitia michezo anao uwezo wa kutumia akili ya kufanikisha lengo lake la kisiasa na uchaguzi unapomalizika na yeye akianza kutambulishwa kama mheshimiwa mbunge au diwani, huweza kujikuta akiusahau kwa miaka kadhaa ule umuhimu wa mashindano ya soka ya watoto au vijana.
Mtu wa aina hiyo yupo tofauti na yule ambaye anaanzisha mashindano kwa nia ya kuzalisha vipaji vingi, bila ya kuongozwa na msukumo au matakwa ya kisiasa.
Umuhimu wa TFF upo kwenye ukuzaji wa soka, si katika yale maeneo yenye kuweza kufikika peke yake. Vijana wa mikoa mingi ya nchi hii wanashindwa kucheza soka la ushindani mara kwa mara kwa sababu ya ukosefu wa mashindano yenye kuweza kufadhiliwa na watu mbalimbali.
TFF wafikirie namna ya kuwapa motisha waandaaji wa mashindano maalumu ya ngazi za wilaya na mikoa. Ili waone kuwa kile wakifanyacho kinathaminiwa na TFF ngazi ya taifa.
Mwenye kuandaa mashindano ya soka ngazi ya vijana kule Kigoma akiona mdau kama yeye aliyeko mkoa wa Tanga anapewa tuzo ya heshima inayoambatana na fungu la fedha, ni lazima atatumia kila aina ya maarifa ili mwakani apewe tuzo hiyo inayoambatana na kuwezeshwa kiuchumi.
Ndani ya ushindani huo miongoni mwa wanafamilia ya soka ambao wanaguswa na maendeleo ya mchezo huu, tunaweza kujikuta tunaanza kupeleka nje ya nchi wachezaji wengi kila mwaka.
Kwanza, watakuwa wamejitengenezea urahisi wa kuwafahamu wachezaji wengi zaidi, kwani wapo wale ambao hawachezei timu za mikoa za vijana lakini wanao uwezo kama wa wale wanaochaguliwa.
Pili, watakuwa wameondoa manung’uniko yanayokuwepo miongoni mwa baadhi ya wanasoka wenye umri mdogo, wenye kuhisi kwamba kuna upendeleo katika uteuzi wa timu za vijana za wilaya na zile za mikoa.
TFF itakuwa imesogea karibu zaidi na soka la nchi nzima, haitaonekana kuwa ni taasisi ambayo inashughulikia soka la ngazi za juu tu, kwa sababu ya urahisi wa wadhamini kuweza kuingiza fedha zao.
TFF itakuwa karibu na shida zinazokwamisha ukuaji wa kweli wa soka ngazi za kata na vitongoji.
Lawama zisizo na msingi kutoka kwa wanafamilia wengi wa soka la Tanzania zitapungua, tofauti na hali ilivyo sasa. Fedha nyingi zinazoingia kwenye soka ni mtaji muhimu katika ukuzaji wa mchezo huu nchini kote.
Etienne Ndayiragiye
Kocha wa Taifa Stars, ambaye anakiri anaamini katika soka la vijana, ila kubwa zaidi analoona ni klabu kubwa nchini kutowaamini na kuwapa nafasi.
“Hizi timu kubwa zinapaswa kuwapa nafasi (vijana), zikiwanyima wanazidi kuidumuza Taifa Stars kwani kuna wakongwe ambao karibu wanafikia mwisho.”
Salum Mayanja
Amefundisha sana Tanzania, naye anakiri kuna tatizo kubwa la kutowapa nafasi makinda, ingawa wengi ni wazuri.
“Hili ndilo tatizo, lakini ninaamini litakuja kwisha,” anasema kocha huyo mzoefu.
Sven van der Broeck
Kocha wa Simba, ambaye amekiri hilo tatizo lipo, lakini anaamini akidumu na timu muda mrefu kuna mabadiliko makubwa atayafanya.
Ushauri
Yule mama wa Nigeria aliyemuibua Joseph Yobo kutoka kusikojulikana, hivi sasa anaheshimika kokote kule ambako historia ya kijana aliyepitia mikononi mwake inapoongelewa.
Kwanini na sisi tusirahisishe mazingira ya kutuongezea wachezaji wengi kutoka kila kona ya nchi hii? TFF ijiandae kwa ajili ya kufanya kazi ya kumtambua kwa ukaribu na kumthamini kila anayemwaga jasho lake kwa faida ya soka la Tanzania.