Amini kile unachotaka kukifanya na ukifanye
Imani ni msingi wa mafanikio ya kitu chochote. Muda wowote unapotaka kuanza kufanya kitu iruhusu imani itembee mbele yako, kwani kuamini kwamba unaweza kufanya jambo fulani ni kama garimoshi lililoingia kwenye reli yake, lazima liifuate.
Yeyote unayemuona kama mfano wa kuigwa kwenye jamii yako si kwamba hakukumbana na changamoto katika kutimiza ndoto zake au kufanya mambo makubwa, hapana, aliongozwa na imani kwamba anaweza kufanya ndoto zake kuwa kweli na kutimiza yale aliyoyapanga.
Anafanikiwa yule anayeamini katika lile alifanyalo. Hakuna kitu kinachoniumiza kama pale ninapomsikia mtu akisema: “Ninafanya tu ili siku ziende.” Mtu wa namna hiyo ni mtu aliyekosa tumaini kwa kile anachokifanya.
Unapokosa tumaini ni rahisi kukata tamaa. Wanasema washindi si wale waliokata tamaa. Kwa hiyo unapokata tamaa tayari kwenye orodha ya washindi wewe haumo.
“Wale ambao wanaofikiri wana uwezo wa kuibadili dunia ndio watakaoibadili dunia,” alisema Steve Jobs, mwanzilishi wa Kampuni ya Apple Inc inayotengeneza vifaa vya kielektroniki. Kufikiri unaweza kuibadili dunia lazima uongozwe na imani, lazima uamini kwenye kile unachokifanya hata kama dunia nzima inaona unapoteza muda tu.
Thomas Edson, maarufu kama ‘Baba wa Umeme’ duniani, huyu aligundua balbu ya umeme. Ilimchukua takriban miaka mitatu akifanya majaribio ya kutengeneza balbu hiyo. Jambo hilo lilikuwa limewashinda wanasayansi kwa kipindi cha miaka 50. Anashinda anayeamini kwenye kile anachokifanya.
Hauwezi kufanya zaidi ya pale unapoamini unaweza kufanya. Mara nyingi tunapolenga ndipo tunapoanguka au tunaanguka chini zaidi. Sasa kwa nini usilenge mbali zaidi hata ukianguka uanguke sehemu ambayo utasema ama kweli kuna hatua nimepiga?
Tumesikia historia za watu wengi ambao kusema ukweli bila kuamini kwenye kile walichokifanya wasingelifika hapo walipofika. Oprah Winfrey, mtangazaji maarufu, aliwahi kuambiwa kwamba hana mvuto na hawezi kuwa mtangazaji. Maneno hayo hayakumkatisha tamaa, bali yalimpa hamasa. Ni kama kumpiga chura teke, walimuongezea mwendo. Baadaye alikuja kuwa mtangazaji maarufu duniani.
William Kamukwamba, kijana kutoka Malawi, alitengeneza pangaboi iliyoweza kuleta maji na umeme kijijini kwao, jambo ambalo anasema aliweza kulifanya kwa kusoma vitabu vilivyokuwa katika maktaba shuleni kwao. Ingawa alisoma kwa shida kwa kukosa karo na kufukuzwa mara kwa mara shuleni, aliamini kwamba kuna kitu kikubwa anaweza kukifanya na kweli aliweza. Bado unafikiri kile unachokifanya unapoteza muda?
Wayne Root ni mtu aliyetamani kuwa mtangazaji wa redio siku nyingi. Siku zote aliwaambia watu hicho ndicho kitu alichotamani kukifanya, kila mtu alimwambia haiwezekani. Kwanza alikuwa hajajifunza lolote kuhusu utangazaji, hivyo hicho kilikuwa kikwazo kwake.
Aliwahi kupiga simu 28 kwa meneja wa redio moja na simu yake haikuwahi kupokewa. Aliendelea kujinoa kwa kutazama wengine walivyokuwa wakitangaza, kwake neno ‘HAPANA’ lilikuwa mwanzo wa mazungumzo, si mwisho.
Siku moja alipigiwa simu ili aende kwenye usaili wa watangazaji. Jambo la kushangaza yeye ndiye peke yake aliyepita katika usaili huo. Leo hii dunia inamtambua kama mmojawapo wa watangazaji mahiri duniani.
Unaifahamu bendi kutoka jalalani? Huko nchini Paraguay kuna kijiji kimoja kinachoitwa Cateura. Cateura inazo familia takriban 2,500 zinazoishi katika eneo hilo. Watu wa Cateura huchukua takataka zinazotupwa katika kijiji hicho na kuzirudisha katika matumizi ya kawaida.
Ripoti ya mwaka 2010 ya UNICEF inasema zaidi ya tani 1,500 za taka hutupwa katika eneo hilo kila siku. Watu wengi wa eneo hilo si wasomi. Maji ya eneo hilo si salama kabisa. Watoto wa Cateura huokota taka katika eneo hilo na kwenda kuziuza.
Siku moja Favio Chavez, mtaalamu wa mazingira alikuja na wazo la kuwashangaza wengi. Aliwakusanya watoto wa Cateura waliokuwa wakishinda jalalani na kuanza kuwafundisha muziki katika bendi.
Familia nyingi hazikuweza kumudu kununua vifaa vya muziki. Anasema hata tarumbeta lina thamani zaidi ya nyumba. Chavez aligundua suluhisho limo mikononi mwake. Katika jalala lile kulikuwa na vitu vingi vilivyoweza kutengeneza vifaa vya muziki. Kutoka jalalani walitengeneza ngoma, gitaa, tarumbeta, n.k
Bendi ikaanza kufanya vema. Chavez anasema: “Dunia inapotutumia taka sisi tunaitumia muziki.” Leo hii bendi hiyo ina watumbuizaji wapatao 30 wakizunguka dunia kutoa burudani. Favio Chavez aliamini kwenye kile alichokifanya. Fanya unachokiamini.