Ni tembo aliyekuwa na meno marefu sana

Aliishi katika Hifadhi ya Amboseli, Kenya

Mabaki yake kukaushwa, kufanywa kumbukumbu

India yaweka rekodi ya tembo mzee zaidi duniani

Alipewa jina la Tim na aliheshimika katika jamii yake. Huyu si binadamu bali ni tembo ambaye alikuwa miongoni mwa tembo wenye sifa ya kuwa na meno marefu sana.

Alikuwa akiishi katika Hifadhi ya wanyama ya Amboseli nchini Kenya na alikufa mwezi uliopita na kuzusha simanzi kwa wahifadhi katika mbuga hiyo na maeneo mengine duniani ambao hufuatilia maisha ya tembo kwa karibu.

Mamlaka ya Wanyamapori nchini Kenya (KWS) ilitangaza kuwa Tim alikufa akiwa na umri wa miaka 50 na wahifadhi wanaamini kuwa kifo chake kilitokana na sababu asilia, huku ikielezwa kuwa umri mkubwa ndiyo sababu kubwa ya kifo chake. 

Ili kuhifadhi historia, mabaki ya tembo huyo yalisafirishwa hadi Nairobi ambako mipango inafanywa ili kuyakausha na kuyahifadhi vizuri ili yatumike kama kumbukumbu. Lakini pia mabaki hayo yatatumika kama kivutio kingine cha utalii, pia watafiti wanaweza kuyatumia kwa kazi zao.

KWS ilieleza katika taarifa yake kuwa Tim alikuwa miongoni mwa tembo maarufu sana ndani na nje ya nchi hiyo. Meno yake yanaelezwa kuwa yalifikia uzito wa kilo 45 kila moja.

Tim hakutambulika katika maeneo kuzunguka Amboseli kwa rekodi hiyo ya meno tu, alikuwa mkorofi pia. Wanavijiji wengi kuzunguka Mbuga ya Amboseli wanamfahamu Tim kwa tabia yake ya kuvamia mashamba yao na kula mazao. Katika maisha yake, Tim alinusurika kuuawa mara tatu kutokana na tabia yake hiyo.

Ili kuhakikisha Tim analindwa na mazao ya wakulina yanakuwa salama, timu ya walinzi wa wanyamapori, wakishirikiana na wataalamu wa KWS walimvalisha kola maalumu yenye kifaa cha kufuatilia nyendo zake. Kifaa hicho chenye GPS kiliwawezesha wataalamu hao kufuatilia kila anapopita Tim na walipoona anakaribia mashamba ya watu walimrudisha hifadhini.

Hata hivyo, baada ya muda Tim alibaini mbinu hizo na yeye akaanza kutumia ujanja kuwakwepa askari wanyamapori ambao walikuwa wanataka kumrudisha kwenye hifadhi. Haieleweki ni kwa nini Tim alipenda kula mazao ya mashambani wakati katika hifadhi kulikuwa na nyasi za kutosha.

Tim alikuwa mkorofi

Mwaka wa kwanza baada ya kufungwa kifaa cha kufuatilia nyendo zake, Tim alifanya majaribio 183 ya kuvuka mipaka ya hifadhi na kuingia kwenye mashamba katika vijiji jirani. Timu iliyokuwa inamfuatilia kwa karibu ilifanikiwa kumrudisha katika asilimia 50 tu ya matukio, baada ya yeye kutumia ujanja kuwakwepa.

Februari mwaka jana Tim alinusurika kuuawa baada ya kunasa kwenye bwawa lenye tope zito. Baadaye aliokolewa na askari wanyamapori wa KWS na wataalamu wa kulinda wanyama.

Mmoja wa viongozi wa taasisi ijulikanayo kama Save the Elephants, ambayo ilijihusisha kufuatilia maisha ya Tim kwa karibu, Ryan Wilkie anasema: “Tim alikuwa ni tembo wa kipekee, si tu kwangu mimi binafsi bali kwa mamia ya watu wengine ambao walikuja Amboseli kwa ajili ya kumuangalia.”

Anaongeza: “Alikuwa na akili nyingi sana, mtundu na mkorofi lakini pia alikuwa mtaratibu sana, hivyo kuwa balozi mzuri sana wa tembo wengine.”

Kifo cha Tim kimezidi kupunguza idadi ya tembo wa aina yake ambao wana sifa ya kuwa na meno marefu na mazito sana. Taarifa zinaonyesha kuwa hivi sasa aina hii ya tembo wamesalia wachache sana barani Afrika.

Ukiacha Kenya, eneo jingine ambalo tembo wenye sifa hii wanapatikana ni Afrika Kusini, katika Hifadhi maarufu ya Kruger.

Mwaka 2017 tembo wengine wenye sifa hii wapatao 12 waligundulika katika hifadhi hiyo kupitia utafiti maalumu uliofanyika katika hifadhi hiyo kwa kipindi kirefu.

Utafiti huo ulifanywa kupitia mradi wa sayansi unaosimamiwa na Hifadhi za Wanyama za Afrika Kusini (SANParks). Kwa msaada wa askari wanyamapori na matumizi ya ndege, maofisa wa hifadhi pia walitumia picha mnato na za video zilizowasilishwa na watalii katika kipindi cha muongo mmoja kuwabaini tembo hao wenye meno marefu.

“Tembo yeyote (mwenye meno yenye urefu wa zaidi ya meta 1.5) anahesabika kuwa ni wa ajabu,” ilisema taarifa ya timu hiyo ya utafiti na kuongeza: “Kila tembo wa aina hiyo alifuatiliwa na kuwekewa alama na baada ya hapo tunaanza kumfuatilia.”

Awali, tembo kama 28 hivi walionekana kuwa na sifa za aina hiyo lakini utafiti wa kina ulipofanyika ilibainika kuwa ni tembo 12 tu kati yao ndio waliokuwa na sifa hizo.

Hatarini

Ingawa kwa upande mmoja tembo hawa ni kivutio kikubwa, lakini kwa upande mwingine wapo hatarini pia. Majangili wanawatafuta sana kwa sababu jino moja la tembo wa aina hii linaweza kuwa na uzito unaofikia kilo 50, hivyo kuwa na thamani kubwa, jambo ambalo linawafanya majangili wawatafute tembo wa aina hiyo kwa udi na uvumba.

Kuthibitisha hilo, mwaka 2016 tembo maarufu aliyekuwa anaitwa Satao 2, aliyekuwa anaishi katika Mbuga ya Tsavo nchini Kenya, ambaye alikuwa na meno makubwa ajabu, aliuawa na majangili. Kabla ya hapo, tembo mwingine aliyekuwa anashikilia rekodi ya kuwa na meno marefu katika mbuga hiyohiyo, naye aliuawa katika tukio la ujangili.

“Tunapomgundua tembo mwenye meno marefu hivi sasa, mara moja tunampa jina. Aghalabu huwa ni jina la mmoja wa askari wa wanyamapori au mtumishi mwingine wa idara yetu. Ni kawaida kwa askari wa wanyamapori kupewa majina ya utani na wenzao na majina hayo ndiyo tunawapa tembo hao pia,” inasema taaarifa ya timu hiyo ya utafiti.

Utaratibu huu ulianza kutumika baada ya vifo vya tembo saba wenye meno makubwa katika Mbuga ya Kruger zaidi ya miaka 30 iliyopita.

“Jamii nzima ilihuzunika kutokana na vifo vya tembo wale saba. Walipokufa, ilikubaliwa kuwa mafuvu yao, yakiwa na meno, yawekwe kama kumbukumbu na maonyesho,” inasema SANparks.

Tembo wenye meno makubwa katika Mbuga ya Kruger ni moja ya vivutio vikubwa vinavyovuta watalii wengi kutoka duniani kote kuitembelea mbuga hiyo kila mwaka. Pia tembo hao huwavutia wawindaji ambao wanalenga kupata tembo mwenye meno marefu na makubwa.

Satao

Kama tuivyoona awali, mmoja wa tembo wenye meno marefu na makubwa ambaye alijizolea umaarufu nchini Kenya alipewa jina la Satao. Inakadiriwa kuwa alizaliwa mwishoni mwa miaka ya 1960 na kufa Mei 30, 2014, akikadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 45 na 46.

Alikuwa ni mmoja wa tembo maarufu sana nchini Kenya kutokana na umbo lake kubwa na meno yake marefu na makubwa. Meno yake yalikuwa marefu sana kiasi kuwa yalikuwa yanakaribia kuburuza ardhini wakati anatembea. Mbuga ya Tsavo, ambamo tembo huyo alikuwa anaishi ilitangaza kuwa aliuawa na majangili Mei 30, 2914.

Wakati huo alikuwa anahesabika kuwa mmoja wa tembo wakubwa kabisa duniani na alikuwa kama alama ya Kenya. Meno ya Satao yalikadiriwa kuwa na uzito wa kilo 45 kila moja.

Ujangili ni moja ya tatizo kubwa sana la uhifadhi barani Afrika. Mwaka 2013 zaidi ya tembo 20,000 waliuawa na majangili. Ujangili barani Afrika unachochewa na kushamiri kwa soko la magendo la bidhaa za wanyama pori kama vile meno ya tembo, pembe za faru, ngozi za wanyama kama vile simba, chui na duma na vifaa vingine.

Tangu mwaka 2007, biashara haramu ya meno ya tembo imeongezeka maradufu duniani. Ingawa China ndiyo inatajwa kuwa ndilo soko kubwa la bidhaa hizo, lakini nchi kama Marekani, Thailand, Vietnam na Ufilipino nazo pia zinahusika kwa kiasi kikubwa kuchochea biashara hiyo kwa kuwa masoko makubwa ya bidhaa za ujangili. Ongezeko la ujangili pia linachangiwa kwa kiasi kikubwa na magenge ya kihalifu na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe katika nchi kadhaa barani Afrika.

Kutokana na thamani kubwa ya meno yake, Satao alikuwa anafuatiliwa kwa karibu wakati wote na KWS kwa kushirikiana na Mfuko wa Tsavo. Ufuatiliaji huu ulifanyika Mei 18 kabla ya kifo chake Juni 2014. Awali, Satao hakuwa mzururaji, aliishi katika eneo dogo ndani ya mbuga hiyo. Lakini baadaye akaanza kuzunguka na kuingia katika maeneo ambayo ujangili ulikuwa umeshamiri.

Kutokana na eneo alilotembea kuwa kubwa sana na lenye hatari kubwa ya ujangili, KWS na Tsavo wakashindwa kumlinda Satao na kuwapa fursa majangili kumuua kwa kutumia mshale wenye sumu.

Kabla ya kuuawa, Machi 2014, Satao alikutwa akiwa taabani huku akiwa na majeraha mawili yaliyotokana na mishale yenye sumu. Wataalamu walimtibu na akapona haraka.

Kwa mara ya mwisho, Satao alionekana akiwa hai Mei 19, 2014. Juni 2, 2014, Richard Moller, wa Mfuko wa Tsavo, alikutana na mzoga mkubwa wa tembo ukiwa kando ya bwawa lililo katika mpaka wa mbuga nyingine ya Tsavo East. Meno yalikuwa yamekwisha kuchukuliwa na sura yake ilikuwa imeharibiwa, kwa hiyo mzoga huo haukuweza kutambuliwa mara moja.

Kwa muda wa siku kumi, Moller na KWS walifanya msako katika Mbuga ya Tsavo wakimtafuta Satao na baadaye wakabaini kuwa alikwisha kuuawa na mzoga wake ndio ambao Moller alikuwa ameuona. Satao aliuawa kwa kutumia mshale wenye sumu Mei 30, 2014. Juni 13, 2014 ikatangazwa rasmi kuwa Satao alikuwa ameuawa na majangili.

Juni 20, 2014, maofisa wa KWS walisema kuwa askari wanyamapori walikuwa wamewakamata watu watatu wakihusishwa na kifo cha Satao.

Mwingine wa miaka mingi

Wakati Tim na Satao wakipata sifa kutokana na ukubwa wa meno yao, huko India tembo mwingine ameweka rekodi ya dunia kutokana na kuishi muda mrefu. Kwa kawaida wastani wa tembo kuishi ni miaka 45, lakini tembo huyo wa India ambaye alikuwa akiishi katika hekalu la Travancore Devaswom amekufa akiwa na umri wa miaka 98.

Kifo cha tembo huyo aliyekuwa anaitwa Daikshayani kimeacha funzo kwa nchi nyingine kuona umuhimu wa kuwalinda na kuwatunza wanyamapori kwa manufaa ya mazingira na ustawi wa taifa. Kifo hicho kimedhihirisha kuwa iwapo atatunzwa vizuri, tembo anaweza kuishi muda mrefu kuliko ilivyozoeleka.

Daikshayani ni mmoja wa tembo aliyekufa akiwa na umri mubwa ingawa rekodi ya tembo mwenye umri mkubwa kabisa duniani inashikiliwa na yule aliyekuwa anaitwa Lin Wang, kwa mujibu wa kitabu cha rekodi za dunia cha Guinness.

India inakadiriwa kuwa na tembo 2,400 wanaotunzwa katika bustani mbalimbali. Rais wa zamani wa Bodi ya Travancore Devaswom aliliambia Shirika la Habari la AFP kwamba Dakshayani alikuwa akitunzwa vizuri.

Wiki moja kabla ya kifo chake, tembo huyo alionekana katika picha iliyopigwa akiwa amesimama na mmoja wa watu waliokuwa wanamtunza akiwa anampatia chakula.

Wahifadhi wa tembo huyo walilazimika kuanza kumlisha mananasi na karoti miaka ya hivi karibuni baada ya Daikshayani kukabiliwa na tatizo la kushindwa kula. Kutokana na uzee, tembo huyo, ambaye alikuwa anatumika kwa maonyesho, pia alishindwa kufanya hivyo na kusababisha asitumike kwenye shughuli yoyote.

Kabla yake, tembo mwingine mwenye umri mkubwa alikufa mwaka 2003 nchini Taiwan, akiwa na umri wa miaka 86. Wakati wa uhai wake, pamoja na mambo mengine, tembo huyo aliwahi kutumikia pia katika Jeshi la Uingereza katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Tembo mwingine ni Indira, aliyekufa nchini India katika Jimbo la Karnataka mwaka 2017 na iliripotiwa kuwa alikuwa mzee wa kati ya miaka 85 na 90.

Matumizi ya tembo katika shughuli za utalii nchini India ni jambo la kawaida. Ingawa tembo hao wanapaswa kupatiwa matunzo mazuri, lakini kumekuwa na taarifa kuwa hilo halizingatiwi. Kuna taarifa kuwa tembo hao huishi katika mazingira mabaya na hawapatiwi huduma zote kama inavyopaswa.

Sifa za tembo
Tembo ndiye mnyama mkubwa kuliko wote kwa wanyama wanaoishi nchi kavu. Ana uwezo mkubwa wa kusikia, kwani taarifa zinaonyesha kuwa ana uwezo wa kusikia sauti kwa umbali wa kilometa nane. Pamoja na ukubwa wa mwili wake, lakini tembo ni mwoga sana wa wadudu wadogo waitwao nyuki.

Tembo hubeba mimba kwa muda wa miezi 22 na hulala kwa muda mfupi sana, kati ya saa mbili na tatu kwa siku. Kwa siku tembo hula hadi kilo 300 za chakula.

Tafiti zinaonyesha kwamba kwa siku tembo hunywa lita 160 za maji na ndiye mnyama pekee asiyezaa watoto mapacha na hushika mimba kila baada ya miaka miwili baada ya kuzaa.

Tembo hali nyama japo kuwa huua wanyama wanaomchokoza. Jino kubwa kabisa la tembo linafikia uzito wa kati ya kilo 60 na 80.

Kwa kawaida tembo huishi katika makundi ambayo huongozwa na tembo jike, ambaye ana uwezo mkubwa wa kutunza kumbukumbu kuliko tembo dume. Tembo ndiye mnyama anayeongoza kwa kutunza kumbukumbu kwa muda mrefu duniani.

Nini kifanyike

Kuna haja ya Tanzania, kama moja ya nchi ambazo zina tembo wengi barani Afrika, kwa kushirikiana na nchi na taasisi nyingine, kuweka mazingira mazuri yatakayowezesha tembo na wanyamapori wengine kuishi kwa usalama.

Wanyama hao ni muhimu kwa ajili ya uhifadhi na pia ni chanzo kikubwa cha mapato ya fedha za kigeni kupitia shughuli za utalii.

Ni muhimu kwa serikali kutunga na kutekeleza kikamilifu sheria za kuwalinda wanyama hao na kuhakikisha wanaishi bila kubughudhiwa. Harakati za kudhibiti na kukomesha ujangili inabidi zipewe mkazo zaidi kama njia ya kuhakikisha wanyamapori wanalindwa ipasavyo.

Makala hii imeandaliwa kutoka vyanzo mbalimbali mtandaoni.