Ndugu Rais, wako waliosema dunia hadaa, ulimwengu shujaa. Kwa muoga huenda kicheko, na kwa shujaa huenda kilio. Waliosikia walibadilika na kuwa wema na hivyo wakaponyoka adhabu yake, lakini vimbulu walingojea mpaka wakaangamia kwa mateso makali!
Unajitengenezea aina ya kifo mwenyewe kwa mwenendo wako. Je, kitafanana na kifo cha Muadhama Laurian Kadinali Rugambwa? Waliokuwa naye katika kitanda chake cha mauti, saa yake ilipofika walituambia, hata hawakujua Muadhama alipita saa ngapi jinsi kifo chake kilivyokuwa cha amani!
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa amelala juu ya kitanda chake cha mauti huku akijua fika kuwa saa yake imefika bado alisali kuwakumbuka watu wake. Benjamin William Mkapa alituambia watanzania kuwa baba aliomba akisema, “Najua watanzania watalia sana, lakini nitaenda kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu!”
Paroko wetu Nico tukiwa mazikoni, alituasa akisema, “Busara si kuogopa kifo. Busara ni kujiweka tayari kwa kifo chema!” Rais Julius Kambarage Nyerere alijiwekea utayari wa kifo chema.
Mwanamwema umejitayarishia kifo cha aina gani? Umeruhusu ufe kifo cha mateso makali kama kifo alichokufa Rais Samwel Doe? Rais Samuel Doe alipokamatwa aligeuka nyuma awaone waliokuwa wakimsifia muda wote kwa makubwa aliowafanyia lakini hakumwona hata moja. Mazezeta, vuvuzela na makuwadi wake wote walimkimbia. Rais Samuel Doe alikuwa na walinzi wakali aliowatoa kwa marafiki zake, lakini nao walipoona saa imeenea, walimkimbia wakarudi kwao. Alibaki peke yake!
Rais Samuel Doe aliwambwa kama inavyowambwa ngoma. Alikatwa masikio na kutobolewa macho akiwa angali hai, huku wengine wakimkata hata sehemu zake za siri wabaki nazo kwa ukumbusho. Rais Samuel Doe alikufa kwa mateso makali sana lakini nyuma yake aliacha mke na watoto. Usiniulize wako wapi na wako katika hali gani, sijui.
Kibinadamu najua hawana Amani. Unatembea ukiona watu wanakutazama unahisi wanasema bila baba yake huyu, baba yetu angekuwa hai mpaka leo. Au baba yetu asingekuwa na kilema cha maisha alichonacho. Watakuwaje na amani?
Rais Julius Kambarage Nyerere naye alikuwa na walinzi makini lakini hakuonekana kuwa na wakati mgumu wakuwaomba kwa kuwabembeleza walinzi wake wamruhusu raia aliyetaka kumfikishia ujumbe alipokuwa hadharani. Rais Nyerere hakuwa na hofu iliyojionyesha dhahiri kwa wananchi wote, kuwa anayo juu ya maisha yake. Alikuwa na amani kubwa.
Aliacha mke ambaye mpaka leo Taifa na wananchi wanampa heshima kubwa kuliko mwanamke yeyote katika nchi hii. Makongoro, Rose, Madaraka na watoto wa Nyerere wote wanaishi kwa uhuru usio na mipaka katika nchi hii hii, aliyoiacha Rais baba yao.
Sasa angalia na haya. Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi yaonekana kazi ndani ya chama zimekwisha. Umebaki ufahari wakuonyesha sura kwenye TV akivipokea ‘vijitu vidogovidogo.’ (Kwa lugha ya Mwalimu Nyerere). Haijulikani kilichomzuzua ni Ukigoma wao au Udiwani wao! Vyovyote vile huu ni uzuzu.
Tangu kuzaliwa kwangu mpaka namaliza darasa la nane nilikuwa sijawahi kuona upanga wenye makali kuwili! Mambo yakutisha sana yaliyoripotiwa nchini mwetu na Waziri wa Nchi za Nje wa Marekani yanaashiria pasipo kuacha shaka kuwa upanga wetu unaanza kukata huku na huku. Cha kushangaza viongozi wetu wameyakaa kimya. Kitanzi cha Marekani anapoanza kuwaadhibu washukiwa wake duniani nani hakijui? Ameanza lazima atamaliza. Nani atabaki amesimama?
Michael D’Andream jasusi lililokubuhu lililoishi sana hapa kwetu ni data gani juu yetu litakuwa halina? Anaposema ushahidi anao anao kweli. Kama alikuwa anatumwa watamtaja mpaka aliyekuwa anamtuma.
Wakati Yesu anawaambia wafuasi wake kuwa atawalaye kwa upanga atakufa kwa upanga hawakumwelewa. Kwa msaada wa maendeleo makubwa ya teknolojia ‘joto ya jiwe’ ya makali ya upanga imeanza kuonekana tungali hapa hapa duniani. Yale ambayo tulidhani yatabaki kuwa siri mpaka mwisho wetu upite, sasa yanaanza kupeperuka kungali mapema kabisa. Dunia ya sasa hakuna siri tena. Kila kitu kitalipwa hapa hapa. Huu ni ukweli kama jua kuchomoza Mashariki na kuzama Magharibi. Tukumbuke wakati wa Nuhu. Watakaokubali kubadilika na kuwa watu wema, watakubaliwa kuingia katika merikebu ya Nuhu. Bali wababe wote na wote wanaotegemea makali ya upanga, wataangamizwa na maji ya mvua inayoendelea kunyesha!
Neno ushamba kwa wavivu wa kufikiri, wale aliotuonyesha Mzee Mkapa, wanaliona sawa na tusi. Ushamba siyo tusi na wala ushamba siyo ujinga. Ukitoka kijijini ukaingia mjini na kukuta barabara zote ni nyeusi, ngumu yaani ni za lami ukaanza kushangaa wewe ni mshamba. Lakini hiyo haikufanyi wewe kuwa ni mjinga. Ushamba ni sifa anayozaliwa nayo kila mmoja wetu. Kila mtu anathibitisha ushamba wake pale anapokutana na kitu au mazingira ambayo ni mageni kwake. Ushamba ni kama ujinga. Ukiuzoea unakutoka.
Shida ni kwamba washamba wengi kama walivyo wajinga wengi hujisikia aibu wanapoambiwa wauvue ushamba wao. Ni hatari sana kwa ustawi wa jamii yoyote ile kiongozi wao anapokuwa mshamba halafu akadhani watu wake wanamwona hafai.
Wanawema mara kadhaa nimekiri ushamba wangu hadharani. Nilisema nilitumia saa kadhaa pale Mnazi Mmoja kushangaa taa zinavyoongoza magari barabarani. Lakini muda wote nilioutumia kushangaa zile taa sikujihisi kuwa mimi ni mjinga. Nilijiona mshamba tu wakawaida. Na sasa baada ya kukaa miaka 40 Dar es Salaam, nikipita pale Mnazi moja sishangai tena zile taa, naziona ni kitu cha kawaida kabisa. Nikifika na mkweche wangu pale nasimama na mimi ziniongoze.
Hatumshangai Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kwamba pamoja na kwamba ndiye Rais mwenye umri mdogo zaidi bado anaonekana ndiye Rais anayeongoza kwa busara zaidi kuliko hata wanaoonekana kumzidi umri. Hii yote ni kwamba Uhuru hana ushamba wa urais wala hana ushamba wa Ikulu. Amezaliwa Ikulu amekulia Ikulu.
Amekuwa akiyaona madaraka makubwa ya urais aliyokuwanayo baba yake Rais Jomo Kenyetta. Shida ni kwetu sisi ambao hatuna historia hata ya kukulia nyumbani tu kwa mwenyekiti. Kwetu mpaka tunaingia Ikulu ndiyo kunapata anwani. Ukiingia Ikulu lazima utakuwa mshamba. Wengi huzuzuka baada yakutambua kuwa wamebeba mamlaka makubwa ambayo mwanzo hawakuyafahamu.