Jiji la Arusha linakabiliwa na wimbi kubwa la watoto wanaojihusisha na shughuli za kubeba mizigo katika masoko mbalimbali, jambo ambalo limesababisha wengi wao kukatisha masomo pamoja na kujiingiza katika vitendo vya kihalifu.

Watoto hao wanafanya biashara za kubeba mizigo ya wateja wanaofika katika masoko kufanya manunuzi lakini pia hutumiwa kushusha mizigo katika magari makubwa ya mizigo. Hali hiyo imekuwa ni ya kawaida katika Soko Kuu, Soko la Kilombero, pamoja na Soko la Mbauda, yote ya jijini Arusha.

Masoko mengine ambayo watoto hao wamekuwa wakifanya shughuli hizo ni Soko la Tengeru na USA River yaliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Meru pamoja na Soko na Ngaramtoni lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Arusha.

JAMHURI imegundua kuwa asilimia kubwa ya wabeba mizigo katika masoko hayo ni watoto wadogo wenye umri chini ya miaka 18, ambao asilimia kubwa ni wanafunzi wa shule za msingi, na kwamba licha ya shughuli hiyo, pia wanatuhumiwa kujiingiza katika vitendo vya kihalifu, ikiwemo uporaji.

Baadhi ya wafanyabiashara na viongozi wa masoko wamekiri watoto hao kujihusisha na wizi wa mizigo ya wateja, fedha na vifaa vingine.

JAMHURI pia limebaini kuwa kuna dalili ya uwepo wa watu wazima kusaidia kuhifadhi bidhaa zilizoibwa na watoto hao.

Wakizungumza na JAMHURI hivi karibuni, baadhi ya wafanyabiashara katika masoko hayo wamesema watoto wamekuwa wakizunguka kutoka soko moja hadi jingine kutokana na ratiba za minada katika masoko hayo kwa siku. Kuna masoko ya kudumu lakini kuna mengine huendeshwa siku moja tu katika wiki.

Hassan Issa, mfanyabiashara katika Soko Kuu la jijini Arusha, anasema idadi ya watoto hao imekuwa ikiongezeka kadiri siku zinavyokwenda na kwamba watu wengi wamekuwa wakiwatumia watoto katika kubeba mizigo kwa sababu malipo yao ni madogo ikilinganishwa na watu wazima.

“Kwanza unaweza kusikia mtoto fulani aliyepita hapa na mteja amekimbia na mzigo wa mteja, lakini baada ya muda unamuona huyo mtoto, unashindwa kuelewa huo mzigo amekwenda kuuficha wapi. Kwa hiyo hili suala si dogo, tunatakiwa kuwaondoa ili wakasome,” anasema Issa.

Kwa upande wake, Ester Mbuya, mfanyabiashara katika Soko la Tengeru, anasema wakati mwingine watoto hao wamekuwa wakibebeshwa mizigo mikubwa tofauti na umri wao kwa malipo madogo na kuwataka wafanyabiashara wenzake, hasa wale wanaoleta bidhaa kwa magari makubwa kuacha kuwatumikisha watoto na badala yake wawatumie wabeba mizigo wakubwa.

“Na hawa watoto wanazunguka kila soko, kama leo wapo hapa Tengeru, kesho utawakuta Kilombero, siku nyingine utawakuta Soko Kuu, na ukiwauliza hawakosi majibu ya kukudanganya kwamba mara yatima, mara njaa – wanatafuta hela ya kupeleka nyumbani,” anabainisha Mbuya.

Mmoja wa wateja katika soko hilo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini anasema amekuwa akikutana na watoto mara kadhaa ingawa hajawahi kuwauliza kwa nini wapo hapo siku za shule. Anakiri kuwa wakati mwingine huwapatia watoto hao hela kidogo hata kama hajabebewa mzigo ili kukwepa usumbufu wao.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Soko la Kilombero, Abdi Mchomvu, anasema uongozi wa soko hilo kwa kushirikiana na Ofisi ya Kata ya Levolosi, waliendesha operesheni ya kuwaondoa watoto hao lakini baada ya muda watoto hao wakarudi tena sokoni hapo na kuendelea na shughuli hiyo.

“Pia uongozi wa kata ulishaandika barua na mabango ya kukataza watu kuwatumia watoto ndani ya soko hili pamoja na kufanya hiyo operesheni ambayo zaidi ya watoto 30 walikamatwa lakini cha ajabu tatizo limejirudia. Nadhani kuna haja ya kukaa chini na kubuni njia ya kukomesha kabisa tatizo hili kwa sababu hili ni janga la kesho kwenye taifa letu,” anasema Mchomvu.

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Restituta Mvungi, amekiri kuwapo kwa watoto katika masoko yaliyomo wilayani humo, likiwemo Soko la Tengeru na kwamba alishafanya mazungumzo yasiyo rasmi na watoto hao ambapo walikiri kuwa wengi wao ni wanafunzi na kwamba wanatafuta fedha za matumizi.

Anasema ingawa wengine wanadai ni yatima lakini anaamini kuwa wanadanganya ili kupata uhalali wa kufanya shughuli hizo, kitendo ambacho hakikubaliki na kwamba yumo kwenye mchakato wa kuzungumza na mamlaka nyingine ili waweze kuwaondoa watoto hao katika ajira hizo mbaya.

“Hao watoto nimekwisha kuzungumza nao, na nimeshapata picha kamili kwa sababu hata ukiwaambia kama changamoto ni umaskini kuna sehemu wanaweza kupatiwa mahitaji yao ikiwemo elimu, bado hawataki kwenda huko,” anasema Mvungi.

Kwa upande wake Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Neema Mwina, anakiri kuwa wengi wa watoto hao wanatoka katika halmashauri yake na kwamba mwaka juzi walifanya zoezi la kuwaondoa kwa kutumia mgambo lakini baada ya muda wamerudi tena, hivyo ni wazi kuwa wanatakiwa kubuni mbinu mpya.

“Katika zoezi lile watoto zaidi 30 tuliwakamata, wengi wao walitupeleka makwao ingawa tulipata changamoto ya baadhi yao kututoroka njiani kutokana na usafiri tulioutumia. Niligundua kuwa familia zinachangia tatizo hilo, kwani wengi wa wazazi hawafuatilii maendeleo ya watoto wao shuleni,” anasema Mwina.

Pia anasema katika mahojiano yake na wazazi wa watoto hao walisema kuwa wao hawajui kama watoto wao wanajihusisha na shughuli za kubeba mizigo sokoni kwani kila siku wanatoka nyumbani wamevaa sare za shule na kurudi jioni kama walivyotoka.

“Lakini wakati tunapanga nini cha kufanya, pia ninaona jamii nayo ipatiwe elimu kwani nao wanachangia sana tatizo hili, kuanzia wazazi au walezi pamoja na hao wanaowapa hizo kazi. Iwapo wanaobebewa mizigo wataacha kuwatumia watoto ni wazi kuwa hakutakuwa na tatizo hili,” anasisitiza Mwina.

Gazeti hili limefanya mawasiliano na Ofisa Habari wa Halmashauri ya Jiji la Arusha ili kumpata Mkurugenzi au Ofisa Ustawi wa Jamii wa jiji ili kupata ufafanuzi juu ya jambo hili bila mafanikio.

JAMHURI lilielezwa kuwa kwa sasa mkurugenzi amebanwa na majukumu mengine.

Ajira kwa mtoto ni kinyume cha Kifungu cha 12 cha Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 na Kifungu cha 5(1) na (3) vya Sheria na Ajira na Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 ambavyo vinapiga marufuku kumwajiri mtoto katika ajira hatarishi.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 193 zilizokubaliana juu ya ukomeshaji wa ajira mbaya kwa watoto katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1990 ujulikanao kama UN Convention on the Rights of the Child.

Sheria hizo zinataka haki hizo zilindwe na kutambuliwa. Baadhi ya haki hizo ni haki ya ulinzi wa maisha, haki ya elimu, haki ya kupata huduma bora za afya, haki ya kulindwa ili wasipatwe na madhara ya kimwili na kimazingira, pia wawe na haki ya kuabudu pamoja na kushiriki shughuli za maendeleo ya kijamii.