Watu wa kusitasita nawachukia
‘Ningejua,’ na ‘kusitasita’ vikipandwa hakuna kinachoota. Kusitasita ni kutamani jana iendelee. Kusitasita ni mazishi ya fursa. Kusitasita ni mauaji ya neema. Kusitasita ni nukta katikati ya sentensi. “Anza kushona na Mungu atakupa uzi.” (Methali ya Ujerumani). Unapoanza, mambo mengine yanajipanga vizuri. Ukisema nitafanya jambo siku fulani, kumbuka hakuna siku inaitwa fulani. Siku mojawapo, siyo mojawapo ya siku za wiki.
Maneno haya husikika kutoka midomo ya watu wanaositasita: nitaanza kesho; sina kila kitu ninachohitaji; mazingira si rafiki; ngoja nijipange; kesho ipo; haraka ya nini; haraka haraka haina Baraka; nangoja wakati mwafaka. Kusitasita ni falsafa ya “siku fulani nitafanya.”
Bila shaka mtunga zaburi alisikia maneno kama haya na kusema: “Watu wa kusitasita nawachukia.” (Zaburi 119:113). Kusitasita kunafanya mambo mepesi kuwa magumu. Kusitasita kunafanya mambo rahisi kuwa magumu na mambo magumu kuwa hayawezekani. Kuna methali ya Tanzania isemayo: “Asemaye ngoja mnyama ajitokeze kabisa, huchoma mkia.” Ukisitasita na kuacha, unaachwa na fursa.
Unapolala na biashara yako inalala. Kusitasita ni kulala. Unaposimama, ndoto zako zinasimama. Kusitasita ni kusimama kutenda jambo baada ya kuonyesha nia ya kutenda au baada ya kulianza. Acha kusimama. Anza kutembea.
Kusitasita ni kujichelewesha, lakini muda hauchelewi. Chelewa chelewa utamkuta mwana si wako. “Unajua jambo linalotokea unapompa wazo zuri mtu anayesitasita? Hakuna chochote,” alisema Donald Gardener. Ukingoja kujua kila kitu hautafanya lolote. Ukingoja wakati mwafaka hautafanya lolote. Kusitasita ni kuingiwa wasiwasi. Kusitasita ni binamu mvivu wa hofu. “Tunapokuwa na wasiwasi juu ya shughuli fulani tunaahirisha,” alisema Noelle Hancock.
Kesho mara nyingi ni siku ya wiki yenye shughuli nyingi sana. Unaposema utafanya kesho, kesho yako hiyo mikono itakuwa imejaa. Kusitasita na kusema utalifanyia kazi jambo siku za usoni wakati mwingi ni ufunuo wa uvivu, kutojipanga, kutojiamini, kutojithamini, kutokuwa na nidhamu ya kazi, kutojitambua na kutotambuliwa na wengine.
Kusitasita mara nyingi kunasababishwa na hofu ya kushindwa au hofu ya kushinda. Kushinda kunabeba kifurushi cha kuwajibika, kubaki kwenye mstari na kutegemewa na wengi. Mambo yanayokupeleka juu huenda siyo yatakufanya kubaki juu.
“Kama una malengo na kusitasita hauna chochote. Kama una malengo na kuyafanyia kazi, una kila kitu unachotaka,” alisema Thomas J. Vilord. Hauwezi kulima shamba kwa kulilima kichwani tu au kwenye akili. Lazima lionekane kwa macho ya mwili baada ya kuliona kwa macho ya akili.
Napoleon Hill ni mfano wa kuigwa wa mtu ambaye hakusitasita. “Kusitasita ni mazoea mabaya ya kuahirisha hadi kesho jambo ambalo lingefanyika juzi,” alisema Napoleon Hill. Mwamerika huyu amewabadili watu wengi kwa mtazamo wake kusisitiza mawazo chanya na kuyafanyia kazi katika kitabu chake ‘Think and Grow Rich’. Alizaliwa mahali ambapo umaskini ulikuwa unatawala. Akiwa na umri wa miaka 10 mama yake aliaga dunia. Baada ya miaka miwili baba yake alioa mke mwingine.
Tangu utoto wake alikuwa na ndoto ya kuwa mwandishi. Aliweka akiba kidogo kidogo na kununua kamusi. Katika kamusi yake alinyofoa kipande cha karatasi kilichokuwa na neno, “impossible – haiwezekani” kwa kutumia mkasi. Aliyajenga maisha yake kwa msingi wa maneno kuwa hakuna lisilowezekana. Akiwa na umri wa miaka 13 alikuwa analiandikia gazeti la mahalia ambapo alijipatia fedha kidogo ya kusoma. Andrew Carnegie tajiri mkubwa sana wakati huo alimpa kazi ya kuwahoji milionea 500 kugundua kanuni ya mafanikio ambayo ingetumiwa na mtu wa kawaida.
Baada ya kazi ya miaka 25 alitunga kitabu kilichotajwa hapo juu. Kwa kifupi alichokigundua ni kuwa unavyofikiria ndivyo utakavyokuwa. Kuna saikolojia ya utajiri na mafanikio. Lazima unachokifikiria kifanyie kazi ili ufanikiwe. Yote hayo yakishasemwa, ninahitimisha kwa kumuunga mkono mtunga zaburi: “Watu wa kusitasita nawachukia.” (Zaburi 119:113).