Ushauri na uamuzi ni maneno yanayokwenda sanjari katika matumizi ya mawasiliano na matendo ya mwanadamu. Ushauri unapokuwa mzuri unatengeneza uamuzi mzuri, na unapokuwa mbaya unatengeneza uamuzi mbaya, kwa mtu binafsi au kwa kundi la watu.
Kwa vile mwanadamu anaongozwa na hulka, dhamiri na nafsi, hutengeneza hali ya mazoea ya kufanya jambo fulani katika maisha yake. Tabia ambayo inamwezesha kuwa na moyo wa utu kwa wanadamu wenzake na uzalendo kwa nchi yake.
Au kushuku na kuhisi kuonewa na kuamua kujenga tabia ya chuki na kisasi kwa mwanadamu mwenzake, uchochezi na usaliti kwa nchi yake. Mambo kama haya pindi yanapotokea, wananchi hawana budi kuchukua tahadhari. Kinga ni bora kuliko tiba.
Watu wema hawatangulizi uamuzi kutenda jambo, kwa sababu uamuzi ni hitimisho la jambo jema au baya. Jambo la msingi na la maana ni kutanguliza ushauri ambao ni rai au maoni na kutafakari linalo dhamiriwa lina mafaa au maafa.
Jambo lenye manufaa kwa mtu au watu hupewa kipaumbele na kutekelezwa kwa haraka. Na jambo lenye maafa husitishwa au huachwa ili kunusuru masilahi ya wananchi. Katika utaratibu kama huu utaifa na umataifa huonekana. Visasi na chuki kati ya wananchi havipati nafasi.
Dunia ni ileile tangu iumbwe na Mwenyezi Mungu. Lakini imepotezewa sifa yake ya kuhifadhi mazingira bora na kutunza hewa safi kwa ajili ya afya na uhai wa viumbe, kutokana na mwanadamu kutumia akili na elimu yake, uamuzi wake na matendo yake kuvuruga.
Leo dunia imejaa majanga ya joto kali, vimbunga aina aina na mafuriko ya hapa na pale, kutokana na visa vya mwandamu. Mwanadamu anazidi kuchafua na kuharibu anga, hewa na ardhi. Hali ambayo inatishia uhai wa viumbe vyote kutoweka. Dunia inalia, wanadamu wanacheka kwa sababu uamuzi umetangulia kabla ya ushauri.
Wanadamu wanajiamini wao ndio bora kuliko viumbe vingine. Wao wana nguvu na uwezo wa kubadili dunia kutoka katika hali safi na utulivu kwenda hali chafu yenye moto, majivu na jangwa. Mwanadamu anasema eti dunia ni uwanja wa fujo na kila mwenye ngoma au vitimbi acheze. Hapana.
Akili na elimu yao wanadamu inawatekenya na kuwapa midadi kuanzisha fujo na mifarakano ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni, kupitia milango ya haki na utawala bora chini ya misingi ya demokrasia. Vyama vingi vya siasa vya kidemokrasia vina lengo la utawala bora na sheria, siyo fujo na kuvunja sheria.
Wanadamu hawa wamo katika kila fani yenye kuleta maendeleo ya taifa. Miongoni mwao ni wanasiasa na watawala. Makundi haya kila siku yanazozana vikali kiuchumi na kisiasa, hata wakati mwingine kushutumiana na kudharauliana katika sera za uchumi na elimu, na katika kanuni za uongozi na utawala.
Tanzania ni sehemu ya dunia na Watanzania ni miongoni mwa wanadamu, ambao sasa nao wanajitumbukiza ndani ya lindi la uchafuzi wa mazingira ya kisiasa ya uongozi na kujenga tabia ya kiburi, ubabe, uchongezi na uchochezi ili wao wenyewe kuwasha moto wa vita. Sikia kauli zao mitaani.
Taifa huru lenye wananchi huru kama Tanzania linajengwa na wananchi wenye moyo, utu na uzalendo. Ni haki na wajibu wetu kuwasikiliza kwa utuvu viongozi wetu. Kusema si hoja, hoja ni vitendo. Ni kiongozi yupi anasema na anatenda. Kauli na matendo yana uhai wa maendeleo tuyatakayo?
Watanzania tukumbuke si busara tu itumike. Hata uungwana na ustaarabu utumike kwanza pamoja na ushauri kwa kina na utulivu kabla ya kuchukua uamuzi kutenda mambo ya kitaifa. Lazima tuseme tunahitaji uongozi bora si bora uongozi. Ushauri kwanza.