Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeendelea kutekeleza ahadi ya kuzima laini zote za simua mbazo hazijasajiliwa kwa kutumia alama za vidole.
Kwa mujibu wa Mamlaka hiyo, hadi Februari 12, mwaka huu jumla ya laini za simu 7,316,445 zilikuwa zimezimwa baada ya wamiliki wake kushindwa kuzisajili kwa kutumia alama za vidole na kitambulisho cha taifa.
Mwaka jana Serikali iliziagiza kampuni zote za simu za mikononi kuwasajili wateja wake kwa kutumia alama za vidole na kitambulisho cha taifa na ikapangwa Disemba 31, 2019 kuwa mwisho wa kazi hiyo. Hata hivyo, kutokana na matatizo ya upatikanaji wa vitam bulisho vya Taifa, rais John Magufuli alirefusha zoezi hilo kwa siku 20.
Baada ya januari 20, TCRA ikaanza kufungia laini za simu ambazo zilikuwa hazijasajiliwa chini ya utartibu mpya.
TCRA inasema uzimaji wa laini hizo utakuwa kwa awamu na alioanza kuzimiwa ni watu ambao tayari wana vitambulisho vya taifa lakini wameshindwa kusajili laini zao za simu.
Tathmimi iliyofanywa na TCRA inaonyesha kuwa hadi Februari 12, mwaka huu jumla ya laini 32,948,073 za simu zilikuwa zimesajiliwa kwa kutumia utaratibu mpya. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 75.3 ya laini zote za simu nchini zinazokadiriwa kuwa kama milioni 40 hivi.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa TCRA Februari 12, inaeleza kuwa watumiaji 1,790,646 wamerudisha laini zao kwa kuzisajili kwa alama za vidole baada ya kufungiwa.
Baada ya watumiaji hao kurudisha laini hizo zilizokuwa zimezimwa, idadi ya laini zilizozimwa na watumiaji wake kushindwa kuzirudisha imebaki 5,525,799.
Afisa habari wa TCRA, Semu Mwakyanjala, amesema mpaka sasa kuna laini 10,829,442 ambazo hazijasajiliwa kwa utaratibu mpya lakini hazijazimwa kwa sababu usajili wake umefanyika kwa kutumia kitambulisho cha mpiga kura na Mzanzibar Mkaazi.
“Mpaka sasa uhakiki kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) unaendelea na utaratibu wa kuzifunga unatekelezwa,” anasema Mwakyanjala.
Naye, Fredrick Ntobi, Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano TCRA, anasema uzimaji wa laini za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole unatekelezwa kwa awamu.
Anasema kuwa kumekuwapo na sintofahamu kwa watu wasiofahamu utaratibu unaotumiwa na mamlaka hiyo kuhusu uzimaji wa laini huku wakidhani kwamba wanatekeleza zoezi hilo kwa kukurupuka.
“Walidhani tutazima laini zote kwa wakati mmoja. La hasha, sisi tulianza kwa kutumia vigezo vyetu tulivyojiwekea,” anasema Ntobi.
Anadokeza kuwa uzimaji wa laini ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole kwa awamu ya kwanza ulihusisha watu ambao wana vitambulisho vya taifa.
“Sisi tulichukulia kwamba hao watu wamefanya uzembe tukaanza nao, na wananchi wanatakiwa kuelewa kuwa hili zoezi ni endelevu,” anasema.
Aidha, ametoa wito kwa Watanzania ambao laini zao zimefungiwa lakini wanazitumia kwenye mitandao ya kijamii kwamba wanajidanganya kwani watakuwa wanatumia gharama kubwa kupata mawasiliano.
“Watu wanaojitapa kuwa tumewafungia laini bado wana uwezo wa kuingia Facebook, Instagram na Whatsapp wanatakiwa wajiulize kama wanaweza kupata huduma za kifedha katika simu zao?
“Hao nawafananisha na mtu anayeendesha gari lisilokuwa na mafuta, ni lazima atatumia nguvu kubwa, Mimi naona wanachotakiwa kufanya ni wao kusajili laini zao ili kuepuka usumbufu na kuingia gharama katika matumizi ya simu zao,” anasema.