Maisha binafsi ya Kanali Kabenga Nsa Kaisi yalijulikana kwa watu wachache sana, lakini maisha yake ya kikazi yalijulikana vizuri sana katika sehemu zote alizowahi kufanya kazi. Wanaomfahamu na waliowahi kukumbana naye kikazi wanamwelezea kwamba alikuwa ni ‘jembe’ la aina yake popote pale alipofanya kazi. Alikuwa na staili ya aina yake, alikuwa hacheki na mtu na wala hakutaka mfanyakazi yeyote yule amzoee!‌

Hata hivyo, nyuma ya ‘uso wa chuma’ aliojivika, Kanali Nsa Kaisi alikuwa mtu mwema sana, mkarimu sana, mcheshi sana na mwenye moyo wa huruma sana, mwepesi wa kutokwa ‌machozi ya uchungu akipokea taarifa za msiba ama hata shida za wapendwa wake. 

Kanali Kabenga Nsa Kaisi aliwahi kuwa Mwandishi wa Habari mahiri mwanzoni mwa Awamu ya Kwanza. Aliwahi kwenda masomoni Cuba na Israel na aliteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali akiwa Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa‌ Mkoa, Kamishina Wizara ya Mipango, na kadhalika. Tunaambiwa Kanali huko nyuma ndiye aliyebuni jina la Azimio la Arusha; alihusika kwenye mradi wa maji wa aina yake uliokuwa maarufu wa Ntomoko wilayani Kondoa; na kadhalika, na kadhalika. Kanali alikuwa hana mchezo kazini.  ‌

Yapo mengi aliyoyafanya Kanali wakati wa vipindi vya uongozi wake kama Mkuu wa Wilaya na Mkoa. Wananchi wa mikoa alikofanya kazi wanayo mengi ya kusimulia kuhusu utendaji wa aina yake wa Kanali Nsa Kaisi na ‘vituko’ vyake. Kwa mfano, alipokuwa Mkuu wa Mkoa aliwahi kususia hafla ya chakula kwa ajili ya waziri‌ iliyoandaliwa na watendaji wa Ofisi ya Mkoa kwa kuwa aliona ulikuwa ni ubadhirifu wa fedha za umma! 

Si nia yangu kuelezea wasifu wa Kanali huyu, lakini ninaweza nikazungumzia kidogo juu ya nilivyomfahamu‌ kibinafsi tangu mwaka 1985 nilipokutana naye kwa mara ya kwanza nikiwa mfanyakazi kwenye Ofisi ya Rais Mstaafu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kijijini Butiama. Wakati huo Kanali Nsa Kaisi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara. 

Habari tulizozipata tulipofika kijijini Butiama ni kwamba Mkuu wa Mkoa ni mchapakazi kweli kweli, hana mchezo, lakini tatizo ni kwamba alikuwa hana maisha nje ya kazi. Tukaambiwa hata nyumbani kwake hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kufika bila kupata idhini yake! 

Hata hivyo, kwa miaka niliyoishi na kufanya kazi Butiama na baada ya hapo, nilipata bahati ya kumfahamu Kanali Nsa Kaisi kwa kiasi fulani. 

Baada ya kufika Butiama, siku moja Kanali Kaisi alikuja Mwitongo nyumbani kwa Mwalimu, kuonana na Mwalimu Nyerere. Nilisalimiana naye na kujitambulisha kwake. Siku chache baadaye alinipigia simu akaniambia angependa nionane naye nyumbani kwake, alitaka nimuarifu ni lini nitaenda Musoma ili tuonane. Nilishangaa kidogo kutokana na taarifa tulizokuwa tumezipata kuhusu alivyokuwa akiishi. Nikajiuliza maswali ambayo sikupata majibu mpaka siku niliyoenda Musoma na kuonana naye. 

Siku hiyo, nilipofika nyumbani kwa Mkuu wa Mkoa, katika maongezi nikagundua kwamba Kanali alikuwa‌ ananifahamu na anaifahamu vizuri familia ya mume wangu marehemu Gwandumi Jacob Mwansasu. Akaniuliza: Je, unafahamu kwamba mimi ni baba mkwe wako? Akanijulisha kwamba baba mkwe wangu‌  ‌Mzee Jacob Mwamakula Mwansasu ni binamu yake kwenye ukoo wao. Mwisho, akaniambia kwa kuwa niko mbali na familia, nijisikie nina ndugu karibu.  ‌

Baada ya hapo, taratibu nilianza kuufahamu upande wa pili wa Kanali Kabenga Nsa Kaisi aliyeamua kujivika ‘uso wa chuma’ mbele ya wale wote aliokuwa akiwaongoza akiwa Mkuu wa Mkoa na hata watu wengine waliojaribu kutaka kumzoea. Lakini kumbe, Kanali alikuwa mtu mwema sana na mcha Mungu. 

Niliporudi Dar es Salaam na kuanza kufanya kazi na Msaidizi wa Kudumu wa Mwalimu Nyerere, Mama Joan Wicken‌, ‌nilibaini  ‌mapya kuhusu Kanali Kaisi. Kulikuwa na uhusiano wa karibu sana wa kirafiki uliokuwa umejengeka kati ya Mama Wicken na Kanali Kaisi kiasi kwamba siku Kanali akija ofisini kumsalimia Mama Wicken, waliketi ofisini kwa Mama Wicken na kuongea kwa muda mrefu. Wakati mwingine alimletea zawadi mbalimbali ikiwemo ya maua! Ilidhihirika wazi kwamba walikuwa marafiki wakubwa. 

Nilichoweza kugundua pia, kutokana na maelezo yake Kanali mwenyewe ni kwamba alikuwa akimuheshimu sana Mwalimu na kumchukulia kama baba yake. Ni wazi, hali hiyo ilitokana na historia ya utendaji kazi wa Kanali. 

Mwalimu Nyerere aliwapenda sana watu waadilifu na wachapa kazi. Kuna mengi aliyoyafanya Kanali Kaisi tangu ujana wake katika kuleta maendeleo ya taifa letu; mambo ambayo pengine hata hakuna anayeyazungumzia na ambayo yangestahili kuandikwa kwenye wasifu wake. Mwalimu Nyerere aliyajua hayo na kuthamini sana utendaji wa Kanali Kaisi hadi ukajengeka uhusiano wa karibu wa ‘Baba na Mwana’. 

Siku moja katika maongezi Kanali alinieleza kwamba tulipokuwa Musoma‌, ‌Mwalimu ambaye alikuwa akipenda sana kusoma vitabu, kila akipita Musoma, alikuwa akiingia nyumbani kwa Mkuu wa Mkoa na kwa uhuru kabisa alikuwa‌ akienda moja kwa moja kwenye chumba cha kulala cha Kanali ambako kulikuwa na vitabu vingi vya aina mbalimbali. Mwalimu alikuwa akichagua kitabu alichotaka kusoma na kuketi humo chumbani kusoma. Wakati mwingine aliazima vitabu kutoka kwenye hazina hiyo ya vitabu alivyokuwa navyo Kanali Kaisi. 

Si hivyo tu, Mama Maria Nyerere naye alikuwa ni mama kwa Kanali. Kila Mama Maria alipokwenda mjini Musoma hakuacha kupita nyumbani kwa Mkuu wa Mkoa Kanali Nsa Kaisi, na kujisikia yuko nyumbani sana. Uhusiano huo wa ‘Mama na Mwana’ uliendelea mpaka sasa.  ‌

Mwaka jana kabla ya sikukuu ya kuzaliwa Mama Maria Nyerere, Kanali Kaisi alinipigia simu kuniomba nimuulize Mama Maria angependa Kanali ampelekee zawadi gani kwenye sikukuu yake ya kuzaliwa. Niliwasiliana na Bhoke mjukuu wa Mwalimu anisaidie kumuuliza Mama Maria juu ya hilo. Mama akajibu kwamba angependa kupata mchele wa Kyela. Kanali Kaisi alihakikisha anampelekea mama yake gunia la mchele wa Kyela, bila shaka Mama Maria alifurahi sana kuupokea! 

Si hayo tu, Kanali Nsa Kaisi ana‌heshimika na anayo nafasi ya kipekee miongoni mwa wana familia wa Nyerere waliopo Butiama na kwingineko ambao walishuhudia uhusiano mwema ukijengeka baina yake na familia hiyo.  ‌

Binafsi, Kanali Nsa Kaisi aliichukua nafasi ya baba mkwe kikamilifu, amenisaidia katika mambo mengi. Wakati wote tuliendelea kuwasiliana na aliwahi kuniambia kwamba anataka kuandika kitabu kuhusu Mwalimu Nyerere. Cha kusikitisha sana ni kwamba sikuweza kuonana naye katika siku zake za mwisho. Nalijutia sana hilo.  ‌

Napenda sote Watanzania, ndugu jamaa na marafiki wa Kanali Kabenga Nsa Kaisi tumuombe Mwenyezi Mungu aipumuzishe roho ya ndugu yetu marehemu Kanali Nsa mahali pema Peponi. Amina. 

‌Mwandishi wa tanzia hii, Anna Julia Mwansasu‌, alikuwa Katibu Muhtasi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kwa sasa anaishi Dar es Salaam. Simu 0715 788209