Wahenga wana misemo mingi na moja ya misemo hiyo ni: “Mtoto wa nyoka ni nyoka.” Usemi huu umejidhihirisha wazi kwa mwanamuziki wa kizazi kipya, Banana Zorro, anayefanya muziki kama alivyo baba yake mzazi, Zahir Alli Zorro.

Zahir ni mmoja kati ya wanamuziki wakongwe aliyeingia kwenye tasnia ya muziki mwaka 1968 na hadi sasa anaendelea ‘kupeta’ kwenye tasnia hiyo.

Alifanikiwa kupata watoto wawili ambao ni Banana na dada yake, Mahunda, ambao wote wamegeuka kuwa wasanii mahiri wa muziki wa Bongo Fleva.

Wasifu

Banana alizaliwa mwaka 1983 mkoani Iringa, ambako baba yake alikuwa mwanamuziki katika bendi ya JKT Kimulimuli.

Baadaye wazazi wake walihamia jijini Dar es Salaam ambako Banana alijiunga na Shule ya Msingi Kurasini mwaka 1991 hadi 1997.

Mwaka 1998 alijiunga na Sekondari ya Mt. Mathew iliyopo Kongowe mkoani Pwani. Mwaka 2000 akahamia Metro Police hadi alipohitimu kidato cha nne mwaka 2001.

Alikoanzia muziki

Awali, Banana alikuwa akipenda kuiga kucheza staili za marehemu mwanamuziki kutoka nchini Marekani, Michael Jackson, kabla hajajiunga rasmi kwenye kuimba baada ya kuhitimu kidato cha nne.

Aliichora ramani yake ya muziki pindi alipokuwa kidato cha pili. Alikuwa akiitumikia bendi iliyofahamika kama Bilovem. Alipenyeza sauti yake kwenye wimbo wa bendi hiyo uitwao ‘Anakudanganya.’ Baada ya kufanya hivyo, muda mfupi baadaye, bendi hiyo ilikamilisha albamu iliyobebwa na wimbo huo.

Inafrica Band

Harakati rasmi za muziki kwa Banana zilianza mwaka 2001, baada ya kuhitimu masomo ya sekondari.

Alijiunga na bendi iliyofahamika kama Inafrica Band baada ya kuunganishwa na msanii mkongwe nchini, Bizman.

“Hapo tuliandaa albamu ya ‘Indege’. Hiyo ndiyo iliyoniwezesha kujifunza vyombo mbalimbali vya muziki,” anasema Banana.

Mwaka 2002, alishiriki shindano kubwa la kusaka vipaji lililojulikana kama Pop Idol na kupata daraja la pili, akaongeza umaarufu wake. Katika shindano hilo Banana aliibuka kidedea baada ya kuonyesha uwezo wa hali ya juu wa kuimba.

Albamu ya kwanza

Mkali huyo wa sauti anasema nguvu zake kwenye muziki zilichanua baada ya kujizolea umaarufu mkubwa kwenye mashindano ya Pop Idol. Alifanikiwa kuachia albamu yake ya kwanza iliyojulikana kama ‘Banana’. Ilishiba nyimbo kali kama ‘Mama’, ‘Wasiwasi’ na nyinginezo.

Moja kati ya matunda ya albamu hiyo aliyoitoa mwaka 2002 ni tuzo za Kilimanjaro 2003, kupitia kipengele cha Mwanamuziki Bora wa Kiume.

Milango ya shoo ikafunguka. Akaanza kufanya ziara mikoani akiwa ameambatana na wanamuziki wengine kama vile Q. Chief na Papii Kocha, ambaye ilikuwa wafanye naye wimbo wa pamoja. Lakini mpango huo ulishindikana baada ya Papii kuingia katika matatizo yaliyosababisha awekwe rumande na baadaye kufungwa.

Aikacha Inafrica Band

Mwaka 2005 Banana aliamua kuachana na Inafrica Band, akajikita katika muziki wa peke yake (solo artist), ambapo alifanikiwa kuingiza sokoni albamu yake ya pili iliyojulikana kama ‘Subra’.

Ndani ya albamu hiyo kulikuwa na vibao kama ‘Mapenzi Gani’, ‘Mama Kumbena’ na ‘Niko Radhi’ ambazo hadi leo bado zinafanya vizuri katika ulimwengu wa muziki ndani na nje ya Tanzania.

Kama ilivyokuwa katika albamu ya awali, ya pili nayo ilimuwezesha kujinyakulia tuzo mbili za Kilimanjaro Music Awards mwaka 2007.

Alishinda katika kipengele cha Mwimbaji Bora wa Kiume pamoja na Wimbo Bora wa R&B (Niko Radhi).

Kwa leo tuishie hapa na wiki ijayo tutazidi kuangalia safari ya kimuziki ya kijana huyu.