Utafiti uliofanywa na HakiElimu nchini umeonyesha kuwa ushiriki hafifu wa wazazi au walezi kuhamasisha watoto kufanya vizuri shuleni na uhusiano mbaya na walimu kuwa ni moja ya vyanzo vikubwa vya watoto wengi kufanya vibaya katika matokeo ya mitihani ya kitaifa.
Hayo yalibainishwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Dk. John Kalage, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuitambulisha ripoti ya utafiti wa sababu zinazochangia baadhi ya mikoa kufanya vizuri huku mikoa mingine ikifanya vibaya mfululizo katika mitihani ya darasa la saba.
Kalage anasema utafiti huo ulilenga kubaini mambo yanayosababisha baadhi ya mikoa kufanya vibaya na mingine kufanya vizuri.
“Sababu moja ambayo ilionekana kuwa nzito na ilisemwa na washiriki karibia katika kila shule wilayani na mkoani ni umuhimu wa wazazi kushiriki kwa karibu katika kusimamia elimu ya watoto wao. Shule zenye ufaulu wa juu zilihusishwa na wazazi ambao wanathamini elimu ya mtoto. Kwa mfano, ni asilimia 34 tu ya wanafunzi kutoka katika shule mojawapo kati ya ambazo hazifanyi vizuri waliosema kuwa wazazi au walezi wamekuwa wakiwahamasisha kusoma kwa juhudi, tofauti na asilimia 87 ya wenzao kutoka katika shule zinazofanya vizuri katika wilaya moja ambao walisema wazazi au walezi wamekuwa wakiwahamasisha watoto kusoma kwa bidii,” anasema Dk. Kalage.
Pamoja na ushiriki finyu wa wazazi au walezi katika elimu ya waoto wao, utafiti huo umebaini pia kuwa umbali mrefu kutoka nyumbani kwenda shuleni na kutoka shuleni kwenda makao makuu ya wilaya ni sababu nyingine inayoathiri ufaulu wa wanafunzi wengi.
Aidha, Dk. Kalage anazitaja sababu nyingine kuwa ni tofauti ya miundombinu ama mazingira kutoka mkoa mmoja hadi mwingine, kutokuwapatia motisha ama hamasa walimu na mbinu za ziada ili kuimarisha ufundishaji na kujifunza pamoja na kuwapo kwa changamoto katika masuala ya menejimenti.
Dk. Kalage anaitaja baadhi ya mikoa iliyoonekana kufanya vibaya katika matokeo ya wanafunzi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kuwa ni Singida, Dodoma, Mtwara, Mara, Tanga, Kigoma, Tabora na Manyara.
Aidha, baadhi ya mikoa inayoonekana kufanya vizuri ni pamoja na Arusha, Dar es Salaam, Geita, Iringa, Kilimanjaro na Kagera.
Dk. Kalage anabainisha kuwa kati ya sababu zinazofanya mikoa hiyo kufanya vizuri ni kuwapo kwa utawala na menejimenti nzuri katika ngazi ya shule na wilaya, mbinu za ziada kuimarisha kufundisha na kujifunza katika ngazi za mkoa na wilaya na ushiriki wa wazazi na uhusiano mzuri baina yao na walimu na motisha kwa walimu.
Dk. Kalage anasema ilifahamika kuwa, ukiachilia mbali matokeo ya darasa la saba, mikoa, wilaya na shule zina mahitaji sawa ya rasilimali za kufundishia na kujifunzia na miundombinu kama ilivyoainishwa katika ripoti kuu ya utafiti. Kwa mfano, kwa wastani Mkoa wa Geita, ambao ni moja kati ya mikoa inayofanya vizuri, una upungufu wa madarasa kwa asiliia 56 na madawati kwa asilimia 36. Pia, kwa wastani, Mkoa wa Singida ambao ni moja ya mikoa ambayo imekuwa haifanyi vizuri, una upungufu wa madarasa kwa aslimia 49 na upungufu wa madawati kwa aslimia 21.
“Katika utafiti huu, HakiElimu kwa kutumia ripoti ya matokeo ya mtihani wa taifa wa darasa la saba 2016 na 2017 tumechagua mikoa michache iliyofanya vizuri pamoja na michache iliyofanya vibaya kwa ajili ya kujifunza na kubaini matokeo yao ili iwe chachu kwa mikoa mingine kujitathmini na kutafuta mambo yanayosababisha matokeo mazuri, wastani au mabaya,” anasema Dk. Kalage.
Anasema anaamini kuwa utafiti huo utaongeza tija kwa mikoa ambayo ilikuwa inafanya vibaya kwa kujifunza kutoka mikoa inayofanya vizuri na kusababisha kila mkoa kufanya vizuri ili kuwa na uhakika wa kuwa na watoto wengi zaidi watakaofaulu na kuendelea na masomo kwa kuimarisha mbinu za kufundisha na kujifunza katika ngazi za mkoa na wilaya.
Anataja kuwa uchambuzi wa nyaraka za mkoa na wilaya unaonyesha kuwa shule mbili kati ya tatu zilizo na ufaulu mzuri wa kila mara katika matokeo ya darasa la saba zina mipango mizuri iliyo katika maandishi, ambayo inalenga katika kuimarisha ufaulu wa mtihani wa darasa la saba.
Mipango hiyo ni kama vile kuwazawadia walimu ambao wanafunzi wake wamepata alama ‘A’ katika matokeo ya mitihani ya darasa la saba. Zawadi hizo ni pamoja na fedha taslimu, jambo ambalo linaongeza motish ya walimu kufundisha. Pia kuna mipango inayoonyesha kuwa umakini unazingatiwa katika madarasa ya mtihani (darasa la nne na la saba) ili kuwasaidia wanafunzi kuwa na muda wa kujifunza kwa undani.
Anasema chini ya mipango hiyo, wanafunzi walio katika madarasa hayo hupatiwa muda zaidi wa kujikumbusha masomo.
“Utakuta mathalani masomo yanaanza saa moja kabla ya muda wa kawaida ukilinganisha na madarasa mengine. Pia, wanafunzi katika madarasa ya mtihani walihamasishwa kuhudhuria shule hata wakati wa mapumziko ya mwisho wa wiki na siku za sikukuu kwa ajili ya marudio ya masomo. Aidha, wanafunzi hawakupewa kazi za ziada shuleni,” anafafanua.
Anatanabaisha kuwa ufaulu umeongezeka katika mikoa hiyo kutokana na jitihada za kudhibiti utoro kupitia njia mbalimbali pamoja na faini kwa wanafunzi wasiohudhuria shuleni kwa zaidi ya siku tatu mfululizo bila sababu za msingi. Faini iliwekwa kwa kuzingatia makubaliano kati ya walimu, wazazi na wanafunzi na wakati mwingine iliwekwa na wazazi wenyewe.
“Ni matumaini yangu kwamba matokeo ya utafiti huu yatachochea mijadala kuhusiana na matokeo ya ujifunzaji kwa watoto wetu na namna bora ya kuboresha ufaulu ili kuinua elimu yetu,” anasema.
Kwa upande wake, Mshauri Mkuu wa utafiti huo, Dk. Richard Shukia, anasema utafiti umefanyika katika mikoa kumi na kuongeza kuwa matokeo ya utafiti huo yatachangia kuongeza ufaulu katika baadhi ya mikoa, hasa ile iliyofanya vibaya, iwapo itazingatia mapendekezo yaliyotolewa na masomo watakayojifunza kutoka kwa mikoa inayofanya vizuri.
Anataja kuwa muundo wa utafiti ulielekezwa kwa kutumia njia ya mchanganyiko ya utafiti, inayotumia njia zote za kiwango na ubora za kukusanya taarifa zilitumika ili kuimarisha uzito wa taarifa zinazoandaliwa.
Washiriki wa utafiti walikuwa maofisa wa elimu wa mikoa, wilaya; maofisa tathmini, walimu wakuu na wenyeviti wa kamati za shule kutoka katika mikoa iliyoshirikishwa katika utafiti huo.
Mikoa ilichaguliwa kulingana na matokeo ya darasa la saba kwa mwaka 2016 na 2017. Mikoa iliyokuwa na ufaulu mzuri ni pamoja na Geita, Iringa na Dar es Salaam, wakati yenye ufaulu wa wastani ni Mbeya, Mara na Pwani; na mwisho yenye ufaulu wa chini ni Songwe, Dodoma, Singida, na Mtwara.
Anasema utafiti ulilenga kuona kama kuna sababu mahususi ambazo hazifahamiki zinazosababisha baadhi ya mikoa kutofanya vizuri na mikoa mingine kufanya vizuri katika mtihani wa darasa la saba katika mazingira ambayo yanafanana.
Kwa mujibu wa Dk. Shukia, sababu ambazo zimebainishwa na ambazo zimetofautiana kati ya sehemu na sehemu ni pamoja na mikoa ambayo imekuwa inafaulu mfululizo ni ile yenye viongozi ambao wana ushirikiano, wanahamasisha umoja katika kufanya kazi na wanahusisha demokrasia katika uongozi ambayo uhusisha uamuzi unaohusu masuala ya elimu katika mikoa husika, wilaya na shule yanafanyika kwa kushirikiana na kutaja kuwa kwa baadhi ya shule ambazo zinafanya vizuri, wanafunzi wanafundishana wenyewe kwa wenyewe.
Hii inahusisha walimu kuchanganya wanafunzi katika makundi ya wanaofanya vizuri na wasiofanya vizuri; hususan katika madarasa yenye wanafunzi wengi kuliko idadi ya walimu wanaotakiwa.
Hata hivyo, kuna baadhi ya shule ambazo hutumia njia mbaya ili kuwafanya wanafunzi wafaulu au waonekane kuwa wamefauli.
Dk. Shukia anaweka wazi kuwa wakati wa mahojiano na washiriki kutoka katika moja ya wilaya zinazofanya vizuri, ilibainishwa kuwa baadhi ya mikoa, wilaya na shule zinazofanya vizuri, zilifanya udanganyifu ili kuhakikisha kuwa wanafunzi katika mikoa, wilaya na shule husika wanafaulu mtihani wa kumaliza darasa la saba.
“Kama ilivyoelezwa katika ripoti, maofisa wa elimu katika shule, wilaya na mikoa waliamua kufanya udanganyifu ili kuhakikisha shule, wilaya na mikoa yao inapata nafasi za juu katika matokeo,” anaeleza.
Ilielezwa kuwa maofisa elimu katika ngazi tofauti kwa kushirikiana na walimu wakuu wa shule na baadhi ya walimu walijibu au kufanya maswali ya mitihani na kuwapa majibu wanafunzi katika vyumba vya madarasa kabla ya mtihani.
Hata hivyo, bado kuna maswali ya kujiuliza kuhusu kuhusisha ufaulu mzuri na udanganyifu, kwani kunaweza kuhamasisha wengine kufanya vitendo hivi ambavyo havikubaliki.
Sababu hizi za tofauti zinaweza kuwa zimesababisha mwendelezo wa ufaulu mbovu katika matokeo ya darasa la saba, ikiwa ni pamoja na umbali mrefu kutoka nyumbani kwenda shuleni na makao makuu ya wilaya, ambapo inawanyima wanafunzi manufaa kutoka wilayani, ikiwamo pamoja na kufanyiwa udhibiti ubora.