Wiki iliyopita nimezungumzia hali ya kisiasa katika Jimbo la Lindi Mjini. Nimeeleza katika usuli kuwa hilo la Mama Salma Kikwete kudaiwa kulitaka jimbo hilo ni moja kati ya mambo niliyokutana nayo katika safari ndefu ya kilomita 4,500 niliyozunguka nchi nzima.
Katika wiki hiyo hiyo, kwanza niliongeza kilomita 900 kwa kusafiri kwenda na kurudi, kwa maana ya kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma kuhudhuria mkutano wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSPF, lakini pia ndani ya wiki hiyo baada ya kurejea Dar es Salaam, nimelala siku moja nikasafiri tena hadi hapa Singida.
Umbali kati ya Singida na Dar es Salaam ni kilomita 720, kwa maana hiyo kwenda na kurudi Singida ni kilomita 1,440. Zikijumlishwa na 4,500 za awali, nimesafiri wastani wa kilomita 6,840 ndani ya wiki tatu. Nimeona na kujifunza mengi katika ziara hii.
Nikiwa Mpanda mkoani Katavi, nilikuta askari wa usalama barabarani wakiongoza vijana waendesha pikipiki karibu 500. Nilipata mshtuko kidogo. Kundi lilikuwa kubwa. Nilihoji kuna nini. Nilipewa jibu kwamba Polisi mkoani Katavi wamejiwekea utaratibu wa kutoa mafunzo kwa waendesha Bodaboda na wanakutana nao angalau mara moja kila mwezi.
Nilipokwenda Bukoba, ambako biashara ya Bodaboda ilianzia hapa nchini kwa kuigiza Waganda kwani kwao huu ni usafiri wa siku nyingi, nilikuta Bodaboda wanaendesha pikipiki kwa ustaarabu wa ajabu. Niliuliza imekuwaje polisi hawapambani tena na Bodaboda Bukoba, nikapewa jibu.
Sitanii, jibu nililopewa lilinifurahisha. Miaka ya nyuma ilikuwa polisi wanapambana na Bodaboda Bukoba kwa kukamata pikipiki kwa maelfu, nilipouliza imekuwaje sasa hawawakamati, askari mmoja akaniambia. “Huyu Kamanda wa Polisi wa Mkoa aliyekuja ana akili sana.”
Nilihoji kivipi? Akasema: “Tangu alipofika, alisema si vyema kuendelea kufukuzana na Bodaboda badala ya polisi kufanya kazi ya kulinda usalama. Aliwaita Bodaboda wote, wakachaguana kwa sasa wana uongozi wao. Wametunga kanuni zao, na hata mtu akiendesha hovyo, wenyewe wanadhibitiana kwa kutoleana upepo, kufungiana kwa kuzuia anayeharibu taratibu asifike kijiweni, na sasa ajali zimepungua au kwisha kabisa.”
Nilipofika Dodoma, nako nikakuta sura ya aina yake. Kuna taa za barabarani siku hizi Dodoma. Bodaboda wa Dodoma wanasimama kwenye taa nyekundu, wanasubiri ziruhusu nao wanakwenda sawa na magari. Hali si tofauti kwa hapa Singida. Waendesha pikipiki, wanawasha ‘indicator’ wanasubiri hata mwendesha baiskeli apite ndipo wavuke barabara.
Kwa Mkoa wa Mbeya, nako nilikuta hali ni shwari. Kimsingi niseme katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Iringa, Mbeya, Rukwa, Kigoma, Kagera, Geita na Shinyanga nimejifunza jambo juu ya waendesha Bodaboda. Tena Singida polisi wamewapa mafunzo vijana hawa jinsi ya kutambua wahalifu na wanaendesha kwa kasi ya kiungwana.
Baada ya kuona uendeshaji huo kwa mikoani, nikakumbuka siku niliyokuwa Uturuki. Pikipiki ni usafiri unaotumiwa na Waturuki wengi. Sikupata kuona wanakatiza kwenye taa nyekundu. Ni usafiri wa heshima. Unakuta mke na mume wanakwenda harusini kwa kutumia pikipiki na wanafika salama.
Sitanii, kwa Dar es Salaam niseme wazi tu, maana mficha uchi hazai. Napata wasiwasi kuwa fujo wanazofanya Bodaboda ni ishara kuwa Suleiman Kova, Kamanda wa Kanda Maalum ya Kipolisi Dar es Salaam huenda kazi imemshinda. Inaelekea Kova anawaogopa Bodaboda.
Nimelazimika kusema hivyo kwa maana kuwa kwa Dar es Salaam, Bodaboda sasa ni jeshi jingine. Matrafiki wakati wanaongoza magari kwenye taa, wanafanya kazi ya kukwepa waendesha pikipiki. Bodaboda hawajali taa nyekundu, hawajali sheria yoyote ya barabarani. Aibu ya aina yake na ya mwaka.
Hata pale Makao Mkuu ya Polisi Dar es Salaam, baada ya barabara ya Samora kubadilishwa matumizi hadi leo Bodaboda wanaendesha kutoka Posta Baharini, wanapita Central Police, tena mbele ya maaskari, wanakwenda kinyume cha sheria ya njia moja.
Sitanii, napata masikitiko makubwa ninapoona Bodaboda wanapita mbele ya Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam kwa kuvunja sheria bila kuguswa. Barabara ya Nyerere kwa sasa kuanzia Mnazi Mmoja hadi taa za Kamata, wakiona kuna foleni ya magari upande wa kuelekea uwanja wa ndege wanaingia kulia.
Wanaendesha katika njia ya magari yanayotoka uwanja wa ndege hadi kwenye makutano ya Nyerere na Kawawa kutokea Mnazi Mmoja inapoanzia Barabara ya Bibi Titi. Narudia; waendesha Bodaboda Dar es Salaam hawaheshimu kabisa taa nyekundu wala uwepo wa trafiki barabarani.
Kibaya zaidi, kwa kupita njia zisizo sahihi wanagonga waenda kwa miguu, maaskari na magari, lakini hata kama makosa ni yao wanaungana na kushambulia aliyegongwa. Hapa katikati Kova alionesha nguvu ya soda kwa kujidai kuwa anafukuza pikipiki na bajaji katikati ya Jiji la Dar es Salaam, lakini leo ninavyoandika makala hii ni kichefuchefu. Kova ananifahamu kuwa siumi maneno.
Ingawa siku moja aliniambia yeye ni mtu mkubwa sana, niwe nawasiliana na wasaidizi wake badala ya kumpigia yeye simu, na kweli tangu wakati huo sijampigia tena simu, inawezekana amelewa madaraka. Kova kasi ya Tibaigana aliyoikuta sasa anaififisha.
Kabla ya Tibaigana, ‘Mzee wa Attachment’, Dar es Salaam ilikuwa haikaliki. Magari yalikuwa yanaibwa hovyo, baa zilikuwa zinavamiwa bila utaratibu, mauaji yalikuwa nje nje, lakini Said Mwema alipoteuliwa kuwa IGP na Tibaigana akashika Kanda Maalum ya Dar es Salaam nchi ikatulia.
Sitanii, kabla ya Tibaigana siku hizo benki zilikuwa zinavamiwa kama nzige waingiavyo shambani. Wanywaji walifika mahala wakajitenga na unywaji kwenye baa za ndani. Si kwa imani, ila ni kipindi hicho wakazi wengi wa Dar es Salaam walianza kwenda baa wakiwa wamevaa kaptula au suruali fupi.
Waliachana na suruali ndefu kwa kujiandaa kutimua mbio mara baa zikivamiwa. Ni kipindi hicho ambacho wenye nyumba wengi walianza kujijengea magereza kwa kuweka nondo nzito katika madirisha na milango wakijikinga na uvamizi. Baada ya safisha ya Tibaigana, wizi katika vituo vya mafuta, benki na majumbani ukakoma.
Kwa bahati mbaya, Kova amekabidhiwa Dar es Salaam sijui kwa sababu ya umri kuwa ‘ameishastaafu’ au kwa sababu ya woga tu kama binadamu, sasa anaturudisha nyuma. Bodaboda wanavunja sheria hadi mbele ya ofisi yake, wezi wamerudi kwa kasi ya kutisha jijini Dar es Salaam.
Ukienda Muhimbili, watu waliopata ulemavu kutokana na uvunjifu wa sheria wa Bodaboda idadi inatisha. Asilimia kubwa ya wizi unaofanyika Dar es Salaam, wanatumia pikipiki. Hivi Kova, kwa ukimya wake anakiri kuwa Bodaboda wana nguvu kuliko polisi wote na wamemshinda?
Sitanii, kama angekuwa hajanipa onyo kuwa nisimpigie simu yeye ni mtu mkubwa, ningethubutu kufanya hivyo, ila sasa nalazimika kumfikishia ujumbe huu kupitia gazetini. Kwamba wiki iliyopita nilipata taarifa kijana mweye kibanda cha M-Pesa pale Tabata Segerea alipigwa risasi na kufariki.
Siku mbili baada ya kumuua kijana huyo, kwa mara nyingine eneo hilo hilo majambazi wakiwa na waendesha Bodaboda walifika na Boxer wakapiga risasi juu na kupora tena fedha. Mfanyakazi wa Kampuni ya Mwananchi Communications amepigwa risasi mkononi akiwa karibu na ofisi yao pale Tabata Relini, akaporwa milioni mbili.
Hapa kati, liliibuka kundi la ‘Panya Road’, ambao ni wajomba wa ‘Mbwa Mwitu’. Kwa kuwa kundi hili liligusa wakubwa, hapa Kova alifanya kazi kama polisi. Leo najiuliza, kama Kova aliweza kudhibiti ‘Panya Road’, ameshindwaje kudhibiti Bodaboda wakafuata sheria za barabarani? Je, atawezaje kusimamia ngwe nzito ya Uchaguzi Mkuu ujao?
Wakati najiuliza maswali hayo, nikakumbuka tukio la karibuni. Profesa Ibrahim Lipumba alikuwa anakwenda Mbagala kusitisha maandamano ya wafuasi wake, lakini ukiangalia picha za kichapo alichopewa na vijana wa Kova, unakasikitika. Nikasikitika kwa maana ilitumika nguvu kubwa mno.
Nikajiuliza kama Kova anaweza kutumia nguvu kubwa kiasi hiki kumdhibiti Lipumba, anashindwa nini kutumia robo yake kuwadhibiti Bodaboda? Wakati najadiliana na marafiki zangu kuandika makala hii, wamenionya. Wakasema ukimwandika Kova ‘vibaya’, yatakukuta ya Absalom Kibanda.
Sitanii, nikajiuliza lipi baya? Kumwambia kuwa majambazi wanaua watu Dar es Salaam wakati anayo dhamana ya kulinda maisha yetu? Nikawaza na kuwazua. Kwamba kumwambia kuwa Bodaboda wanavunja sheria mbele ya ofisi yake ndiyo kumwandika vibaya?
Jibu nililopata ni kwamba tunahitaji kuwa na ujasiri wa kumwambia mfalme kuwa yuko uchi, badala ya kumsifia huku wapita njia wakimcheka. Hofu ninayopata; kama Kova ataendelea kuwapo madarakani na Uchaguzi Mkuu ukafika waendesha Bodaboda wakiwa na ‘uhuru’ wa kuvunja sheria za barabarani Dar es Salaam bila kukemewa, amani ya Tanzania itapotea kuanzia Dar es Salaam.
Bado naamini nafasi ipo. Kova anaweza kuiga walichofanya ma-RPC wa Kagera, Katavi, Singida, Mbeya na kwingineko. Kwamba atumie kila mbinu kuwafanya Bodaboda wajue kuwa hawako juu ya sheria. Kuvunja sheria kwa matarajio ya kuwa na kinga ya kundi, ni hatari kwa ustawi wa Taifa letu.
Kwa vyovyote iwavyo, Dar es Salaam haiwezi kuendelea na vurugu hii ya Bodaboda. Kampala nchini Uganda kuna Bodaboda nyingi kuliko Dar es Salaam, lakini Serikali inasimamia sheria, na Bodaboda wanafuata sheria. Kwa Uganda, Bodaboda kupita kwenye taa nyekundu wakimkamata anayeendesha inauzwa saa hiyo hiyo.
Dar es Salaam ikianzisha utaratibu huu, hatutawaona Bodaboda wakipita taa nyekundu wala kushuhudia ajali zisizokoma. Suluhisho la kudumu ni kufunga kamera za CCTV kwenye makutano ya barabara kuu kama Tazara. Atakayepita taa nyekundu, namba ikisomeka pikipiki yake inafuatwa nyumbani na kuuzwa mara moja.
Kova epuka aibu hii. Itisha kikao haraka na askari wako, mjadili uvunjifu wa sheria wa hawa Bodaboda. Unaweza kuamua kunipuuza, lakini nakuhakikishia tukiendelea na uvunjifu huu wa sheria kuelekea Uchaguzi Mkuu, Dar es Salaam haitakalika. Kama tunaweza kuziba ufa, kwa nini tusubiri kujenga ukuta? Mungu ibariki Tanzania.