Jiji la Arusha lililopo kaskazini mwa Tanzania limepata umaarufu mkubwa kutokana na kuwepo kwa vivutio vingi vya utalii na kuufanya mji huo kuitwa mji wa kitalii.
Vivutio hivyo ni pamoja na uwepo wa Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa ya Arusha, Mbuga ya Wanyama ya Tarangire, Hifadhi ya Taifa ya Manyara na nyinginezo.
Pamoja na vivutio hivyo, Jiji la Arusha limeendelea kuvutia watalii wengi kupitia msitu ambao upo katikati ya jiji hilo. Pamoja na kuliingizia taifa na halmashauri ya jiji fedha, pia msitu huo mkubwa wa kupendeza na kuvutia ujulikanao kwa jina la Themi Living Garden, pia hutumiwa na baadhi ya wakazi wa Arusha kujiingizia kipato.
Msitu huo unaokadiriwa kuwa na ukubwa wa ekari tatu, upo pembezoni mwa Barabara ya Old Moshi, umbali wa kilomita mbili kutoka ilipo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, ambapo pia Mto Themi, unaoanzia Mlima Meru umepita katikati ya msitu huo.
Msitu huo hutembelewa na watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kwa nia ya kujionea mandhari nzuri iliyopendezeshwa na miti mirefu, iliyotengeneza kivuli chenye giza kiasi lakini pia kuna huduma ya vyakula vya asili pamoja na michoro mbalimbali kutoka kwa wasanii wachoraji.
Mwenyekiti wa kikundi cha kina mama cha ‘The Liga Group’ wanaotoa huduma ya vyakula vya asili katika msitu huo, Juliana Msemeno, anasema walianzisha biashara hiyo mwaka 2014 na imewavutia wateja wengi, hasa watalii kutoka nje ya nchi wanaokuja kwa nia ya kutembelea vivutio vingine.
Anasema walianzisha biashara hiyo baada ya kupatiwa mafunzo, vifaa pamoja na ujenzi wa mabanda. Msaada huo waliupata kutoka kwa Taasisi ya OIKOS East Africa.
Kwa kuwa msitu huo ndio chanzo kikubwa cha mapato yao, Msemeno anasema wanakikundi wamekuwa mstari wa mbele katika kutunza mazingira kwa kuhakikisha hakuna ukataji miti unaofanyika ndani ya msitu huo. Aidha, wanahakikisha usafi unadumishwa, ikiwa ni pamoja na kudhibiti utupaji ovyo wa taka.
“Hapa wanaingia watu wengi, ingawa si wote wanakuja kwa ajili ya kula, wengine wanakuja kujisomea, maana ni sehemu tulivu na yenye usalama, wengine wanakuja kuangalia tu mazingira na wengine wanakuja kuangalia aina ya miti,” anasema Msemeno na kuongeza:
“Kama unavyoona hii michoro inaonyesha aina ya mti, unakuja kuna mtu hususan wageni kutoka nje wanakuja kwa ajili ya kujua aina ya miti. Lakini kikubwa ni eneo lenyewe limekuwa kivutio kwa sababu huwezi kujua kama kuna huduma ndani kutokana na kulivyo, kwa nje unaweza kujua ni msitu pekee.”
Huduma zinatolewa kwenye mabanda yasiyo ya kudumu yaliyotengenezwa kwa ustadi ili kutoathiri uoto wa asili, huku pia kukiwa na huduma nyingine za kijamii zenye viwango vinavyokidhi ubora wa afya.
Msemeno anasema kikundi hicho kipo chini ya Halmashauri ya Jiji la Arusha, ambapo lengo lake ni kuwainua kina mama wajane na wanaoshi maisha magumu. Kikundi kilianza na kina mama 200 lakini kwa sasa wapo tisa tu. Wengi wao wameacha kutokana na sababu mbalimbali.
“Unajua kitu kinapoanza wengi wao hawaoni kama ni fursa, wengi walijua tutapewa pesa mikononi. Kwa hiyo wakaanza kuacha mmoja mmoja, lakini sisi tuliobaki tunashukuru kwa sababu tulipewa mafunzo kwa muda wa miezi mitatu ya jinsi ya utunzaji wa mazingira, faida za vyakula asili na jinsi ya kulima mbogamboga za asili zisizokuwa na kemikali,” anasema Msemeno.
Anasema awali wenyeji hawakupokea huduma hiyo vizuri kwani walitamani kuwepo kwa vyakula mchanganyiko si vya asili pekee, lakini wageni wengi walipapenda na kuwafanya wenyeji nao kuona umuhimu wa kutumia vyakula vya asili.
Kwa upande wa afya, anasema hata wagonjwa wanaosumbuliwa na tatizo la sukari mwilini wamekuwa ni wateja wao wakubwa.
“Wapo wagonjwa wa kisukari ambao wanaagizwa na madaktari wao kula vyakula vya asili. Kwa kuwa hapa vinapatikana vyakula vya aina hiyo, basi wanakuja hapa,” anasema.
Kwa mujibu wa Msemeno, licha ya msitu huo kuwasaidia kukuza vipato vyao kiuchumi, lakini wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa miundombinu ya kutosha kama vile majengo na nishati ya umeme ambapo kama ingekuwepo ingewasaidia kuendesha biashara hiyo hadi nyakati za usiku.
“Kama tungepata mfadhili akatusaidia kujenga majengo ya kisasa ingesaidia kupanua wigo wa biashara yetu, kwani wateja wetu, hasa watalii kutoka nje, wao huwa wanatuuliza kwa nini hatutoi huduma hii usiku. Hivyo tunatamani ifike siku tuweze kutimiza lengo hilo,” anabainisha.
Baadhi ya watu waliozungumza na JAMHURI wametoa pongezi kwa watoa huduma ndani ya msitu huo kwani kupitia huduma zao wameweza kuutangaza msitu huo ndani na hata nje ya nchi bila kuathiri mazingira yaliyopo.
Wanasema wamekuwa wakifurahia aina ya vyakula vinavyopatikana katika msitu huo pamoja na mandhari ya kuvutia yaliyopo, kwani hali ya hewa ni baridi ya wastani kwa kipindi chote cha mwaka.
“Kama usipoambiwa ndani ya msitu huu kuna nini huwezi kujua, kwani kwa nje ni msitu mnene lakini ndani yake kuna mazingira mazuri na tulivu ya kupumzikia. Huduma zinazotolewa ni za kipekee, vyakula vya asili ambavyo kwa sasa vinapendwa sana na watu wengi,” anasema Shinu Sabastian.
Kwa upande wake, Thea Mollea, anasema: “Licha ya huduma zilizopo kuutangaza msitu huo lakini vyakula hivi vimekuwa mkombozi wa afya za watu wengi na mmojawapo ni mimi. Nilikuwa na uzito mkubwa kama kilo 120, lakini kwa sasa nina kilo 100. Hii ni baada ya kushauriwa na daktari wangu kula vyakula kama hivi, na isitoshe alinielekeza hadi ilipo hii sehemu.”
Raia kutoka nchini Italia aliyejitambulisha kwa jina moja la Chaser, ambaye anasema amekuja nchini kwa ajili ya kutalii, anasema: “Nimekuwa nikija hapa nchini mara kwa mara kwa ajili ya kutalii, lakini eneo hili nimelifahamu mwaka juzi, hivyo kila nikiwa hapa mjini huwa ninapata chakula cha mchana hapa, ni sehemu nzuri sana.”
Waongoza watalii wanasema wananchi wengi wametumia fursa ya utalii kujinufaisha kama ambavyo wanaoutumia msitu huo kujiingizia kipato.
Zakayo Mjema ni mmoja wa waongoza watalii ambaye anauzungumzia msitu huo kuwa ni moja ya sehemu zinazotumiwa na watalii kwa ajili ya kupata huduma za vyakula pamoja na kuona ama kununua michoro ya picha kutoka kwa wazawa ambao wanautumia msitu huo kama njia ya kuwaingizia kipato.
“Asilimia 75 ya vijana hapa Arusha wamejiajiri kwenye sekta ya utalii kama wapishi, walinzi, wafanyabiashara ndogondogo na kadhalika. Hawa wamekuwa wabunifu wakubwa kwani hauwezi kudhani kuwa kuna kitu hapa ndani ya msitu, lakini ukiingia utafurahia mazingira na huduma zilizopo,” anasema Mjema.
Ndani ya msitu huo kuna kikundi cha vijana wanaojishughulisha na masuala ya kuchora michoro mbalimbali tangu mwaka 2017, ambao wanasema bila kuwapo kwa msitu huo wasingekuwa na soko la uhakika la bidhaa zao.
Nasib Yahya, ambaye ni mwenyekiti wa kikundi hicho anasema bila utalii asingekuwa mchoraji kwani wateja wake ni watalii wanaofika katika msitu huo. Anawashauri vijana wengine waangalie fursa nyingine katika msitu huo zinazoweza kuwaingizia kipato.
“Vijana wengi hawajui kutafuta fursa, wanategemea kuajiriwa. Lakini kama wangefika hapa na kuona mandhari hii huenda wangeweza kubuni kitu ambacho kingewafaa, kwani wateja wanakuja wenyewe si wa kutafuta,” anasema Nasib.