MWANZA
NA MWANDISHI WETU
Chama cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania (UMATI) kimeingia katika mgororo wa umiliki wa nyumba ambayo kilikuwa kinaitumia kama kliniki ya matibabu wilayani Ilemela, mkoani Mwanza.
Ingawa UMATI inadai kuimiliki nyumba hiyo baada ya kuinunua kwa Sh milioni 95 mwaka 2008, mtu ambaye anadai kuwa mmiliki halali wa nyumba hiyo amewaondoa UMATI katika jengo hilo na kushikilia mali kadhaa za taasisi hiyo.
Wakati UMATI wakidai kuimiliki nyumba hiyo, mmiliki huyo ameshindwa kulieleza JAMHURI iwapo ana nyaraka za umiliki wa nyumba hiyo.
Mkurugenzi wa UMATI, Dk. Lugano Daimon, anadai kuwa waliinunua nyumba hiyo Disemba 2008, kwa Sh milioni 95 kutoka kwa mmiliki wake wa awali, Goodhope Hance Mkaro, ambaye alikuwa anahitaji fedha kwa ajili ya kulipa mkopo wa benki uliokuwa umechukuliwa na baba yake.
Dk. Daimon anasema wanashangazwa mtu huyo kurudi tena na kuwaondoa kwa nguvu katika nyumba hiyo kwa madai kuwa yeye ndiye anaimiliki.
Akifafanua, Dk. Daimon anaeleza kuwa Septemba 1, 1998, taasisi yake iliingia mkataba wa upangaji na mmiliki wa jengo hilo kwa ajili ya kuendesha kliniki.
Anasema baadaye UMATI iliinunua nyumba hiyo kutoka kwa Goodhope Hance Mkaro, ambaye alikuwa anatafuta fedha kwa ajili ya kulipa mkopo wa benki uliochukuliwa na baba yake, Godson Hans Rengere, mwaka 2006.
Rengere alikopa Sh milioni 45 kutoka Twiga Bancorp akiitumia nyumba hiyo kama dhamana.
“Kwa bahati mbaya, Godson Hans Rengere, hakuweza kulipa mkopo huo na benki ilidhamiria kuliuza jengo husika ili kufidia deni lake. Kabla ya hatua hiyo Benki ya Twiga Bancorp ilifungua shauri la madai Namba 57 la mwaka 2008 kwenye Baraza la Ardhi na Nyumba la Mwanza, dhidi ya Godson Hans Rengere na Goodhope Hans Mkaro. Baraza hilo liliamuru jengo hilo kuuzwa kwa kuwa wahusika walishindwa kulipa deni hilo,” anasema.
Anasema hapo ndipo Mkaro alianza kuzungumza nao kwa lengo la kuwauzia nyumba hiyo.
JAMHURI limeona nakala ya barua iliyoandikwa na Mkaro Mei 12, 2008 kwenda kwa Mkurugenzi Mtendaji wa UMATI, akiomba fedha za kulipa deni la Twiga Bancorp iliyokuwa inamdai Sh 41,242,694. Katika barua hiyo Mkaro alikubali kulipwa kwa awamu.
Twiga Bancorp kupitia barua yake ya Juni 17, 2008, yenye kumbukumbu namba TBCL/HO/H. 10/28 iliyosainiwa na Kaimu Meneja Mkuu, J. H. J. Matawalo, imekiri kumdai Godson Hans Rengere, Sh 46,440,272.07.
Juni 23, 2008 Mkaro aliandika barua nyingine kwenda UMATI akieleza kuwa yupo tayari kutiliana saini mkataba wa mauziano ya nyumba hiyo.
“Ni matumaini yangu kwamba pamoja na malipo ya deni la benki, ofisi yako itafikiria kunilipa baki ya jumla ya fedha za mkataba huu mapema iwezekanavyo,” imeeleza sehemu ya barua hiyo ya Mkaro.
Dk. Daimon anasema UMATI ilikubali kununua jengo hilo kwa Sh milioni 95 kupitia mkataba wa mauzo namba 033060/100, ambapo sehemu ya fedha hizo zingetumika kulipa mkopo wa benki na kiasi kilichosalia kitalipwa kwa Goodhope Hance Mkaro. Anasema UMATI ilimaliza kulipa pesa zote Disemba 2008.
“Kwa maana hiyo hadi muda huo tayari tulikuwa tumekwisha kununua jengo hilo kwa kuingia makubaliano nje ya mahakama,” anabainisha Dk. Daimon.
Hata hivyo, miaka michache baadaye Mkaro akaanza kuidai UMATI kodi ya pango huku akijua kwamba tayari jengo lilikwisha kuuzwa kwa UMATI.
Notisi
Taarifa zinasema kuwa Machi 19, 2019, kupitia Kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart & Company Limited, Goodhope alitoa notisi ya siku saba kwa UMATI, akiitaka kuachia jengo hilo vinginevyo wataondolewa kwa nguvu.
Dk. Daimon anasema Aprili 2, mwaka jana ofisi hizo za UMATI zilivamiwa kwa nguvu na kundi la vijana walioharibu mali na nyingine kuibwa.
Anasema katika uvamizi huo ambao haukuwa na baraka za mahakama, jengo hilo lilifungwa na walinzi wapya wakawekwa ili kudhibiti uongozi wa UMATI. Magari yenye namba za usajili T 582 AVA na T 756 ABT mali ya UMATI inadaiwa yaliachwa ndani ya jengo hilo wakati likifungwa.
UMATI inaiomba serikali kuingilia kati suala hilo ili wapate haki yao, kwani wanakwamishwa kusaidia jamii kimatibabu.
“Uamuzi wa kufungua kesi ya madai na jinai ulifikiwa. Hivyo, kesi ya madai ilifunguliwa kwa shauri namba 02 la 2019, lililokuwa chini ya Jaji Mdemu katika Mahakama Kuu Mwanza.
“Kesi ya jinai ilipata pingamizi la kipolisi Kituo cha Kirumba. Baada ya ufuatiliaji kwa msaada wa Magna Attorney, tulikuja kugundua kuwa Goodhope Hance Mkaro hakuridhika na uamuzi wa baraza na akakata rufaa Mahakama Kuu, rufaa namba 68 ya mwaka 2016, ambapo rufaa yake ilitupiliwa mbali kwa uamuzi wa Jaji Matupa, Novemba 11,2016,” anasema Dk. Daimon na kuongeza:
“Hakuridhika tena na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, hivyo akakata rufaa namba 171 ya mwaka 2017, katika Mahakama ya Rufaa. Rufaa yake ilitupiliwa mbali kwa mara ya pili kwa kutokuwa na mashiko.” JAMHURI limeona nakala za hukumu za rufani hizo.
Dk. Daimon anasema Goodhope Hance Mkaro, akijua Mahakama ya Rufaa ilitupilia mbali shauri lake Machi 6, 2019, amevamia tena kwa nguvu jengo hilo Plot namba 111, Block ‘A’ lililopo kando ya Uwanja wa Furahisha, Kirumba bila uhalali wa kisheria.
Anasema kuwa uharibifu na usumbufu unaotokana na uvamizi huo unakadiriwa kufikia Sh milioni 631 na tayari suala hilo limeripotiwa katika kituo cha Polisi na kupewa namba MW/RB/5723/2019, dhidi ya Goodhope na Godson Hans Rengere.
Majibu
Alipotafutwa na kuulizwa kuhusiana na sakata hilo, Godson Rengere, alishindwa kuweka bayana ni nani mmiliki halali wa jengo hilo.
“Nipigie baada ya saa nne tutazungumza. Nipo safarini,” Rengere anaeleza kwa kifupi wakati alipoulizwa kuhusu mgogoro huo.
Baada ya saa nne kupita, alipotafutwa kwa mara nyingine akiombwa kuelezea umiliki wa nyumba hiyo, Rengere alitaka aulizwe mwanasheria wake.
Jitihada za kumpata Goodhope ili azungumzie pia suala hilo zinaendelea, kwani kila anapotafutwa kwenye simu yake ya kiganjani inaonekana haipo hewani.