Uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro umeshindwa kubaini kuwepo kwa hujuma zozote dhidi ya njia ya reli kati ya Moshi na Arusha.
Polisi walilazimika kufanya uchunguzi huo baada ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya, kusema hivi karibuni kuwa baadhi ya wafanyabiashara ya mabasi wamehujumu njia hiyo ya reli katika eneo la Sanya Stesheni, Wilaya ya Hai.
Januari 19, mwaka huu, Sabaya aliwataja wakurugenzi wa kampuni za Lim Safari na Machame Safari kuwa ni miongoni mwa wafanyabiashara wa mabasi ya abiria ambao wamekuwa wakiwatumia vijana kuhujumu miundombinu ya reli katika eneo hilo.
Aliagiza wafanyabiashara hao kujisalimisha mara moja katika Kituo cha Polisi Bomang’ombe kilichopo Wilaya ya Hai ili kusaidia vyombo vya usalama katika uchunguzi, agizo ambalo wafanyabiashara hao walilitekeleza.
“… ninazo taarifa kuwa kuna watu wameanza kuandaa magenge ya kihalifu na wanaofanya kazi hiyo ni wamiliki na wafanyabiashara ya mabasi. Kwa hiyo wao wameona njia yao ni kuwaletea usumbufu na wanahujumu miundombinu hii, wanaweka mawe, wanatindua kwenye udongo chini kabisa, wameanza utaratibu wa kulegeza nati, jambo ambalo ni hatari na uhujumu wa moja kwa moja.
“Kama waliua reli kipindi cha kwanza wanataka tena waje waue reli hii ambayo mnairudishia kwa mara ya pili kwenye uongozi huu wa Rais Magufuli … na ninatoa maelekezo yafuatayo, mtu anayeitwa Rodrick Emmanuel Uronu ambaye anamiliki mabasi ya Lim Safari, mtu wa kwanza; mtu wa pili anayeitwa Clemance Onasaa Mbowe, mmiliki wa mabasi ya Machame Safari yeye pamoja na wengine watatusaidia kuwapata watu wanaofanya hii kazi ya ibilisi,” ananukuliwa Sabaya.
Kutokana na taarifa hiyo ya Sabaya, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ilitembelea eneo linalodaiwa miundombinu yake kuhujumiwa na wafanyabiashara hao.
Hata hivyo, katika ukaguzi uliofanywa na kamati hiyo, ilishindwa kubaini aina yoyote ya hujuma katika eneo hilo.
Hilo lilithibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Salum Hamduni, alipozungumza na waandishi wa habari baada ya ziara hiyo ya kamati.
“Niwatoe hofu wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na Watanzania kwa ujumla kuwa hakuna miundombinu ya reli iliyoharibiwa wala kuhujumiwa. Tunaomba wananchi mtoe ushirikiano kwa Jeshi la Polisi juu ya taarifa kuhusiana na suala hili, ikiwa ni pamoja na kuendelea kulinda miundombinu ya reli,” anasema.
Kwa upande wao, wafanyabiashara waliotuhumiwa na mkuu wa wilaya kuwa wanahujumu njia hiyo ya reli wameshindwa kuzungumza na JAMHURI, hata baada ya Jeshi la Polisi kuwasafisha.
“Nani mwenzangu? Charles? Samahani Charles niko kwenye kikao kidogo, hebu nitafute baadaye tutazungumza,” alisema mmiliki wa mabasi ya Lim Safari huku mmilika wa mabasi ya Machame Safari akidai suala hilo amelifikisha kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Mapema mwaka jana, Rais Dk. John Magufuli, aliwatuma mawaziri wa Fedha, Dk. Phillip Mpango na Waziri wa Uwekezaji, Angela Kairuki, kwenda wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro kusaka ukweli juu ya malalamiko ya wawekezaji waliodai kuwekwa ndani na mkuu huyo wa wilaya.
Mbali na kuwekwa ndani kwa saa 48 kwa amri ya Sabaya, wawekezaji hao pia walilalamikia vitendo vya kudaiwa rushwa au kuwekwa katika mazingira ya kudaiwa rushwa.
Kutumwa kwa mawaziri hao na Rais Magufuli kulitokana na wawekezaji hao kumwandikia rais barua ya malalamiko wakilalamikia vitendo vya unyanyasaji wanavyofanyiwa na mkuu huyo wa wilaya.
Waziri Mpango alizungumza na waandishi wa habari na kutaja moja ya manyanyaso hayo ni mwekezaji katika shamba la kahawa la Kibo/Kikafu, Trevor Robert, ambaye ni raia wa Zimbabwe, kuwekwa ndani kwa saa 48 pamoja na kupokwa hati yake ya kusafiria.