DAR ES SALAAM





Rais Dk. John Magufuli na viongozi wengine wakiangalia mchoro wa Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere, moja ya miradi mikubwa ambayo inatekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano. 

Katika makala iliyopita tuliona baadhi ya maeneo ambayo nchi imepiga hatua kwa maendeleo lakini baadhi ya watu, hasa wanasiasa, wanadai kuwa hakijafanyika chochote nchini tangu Uhuru.

Lakini Waingereza wana msemo kuwa: “Seeing is believing”; yaani unaamini zaidi iwapo utakiona kitu kwa macho. 

Ninasema hili kwa vile sisi wafuasi wa Kristo tumeshuhudia ukweli wake kupitia yule Mtume Tomaso kule Yerusalemu baada tu ya ufufuko wa Bwana Yesu Kristo. Ninapenda ninukuu kidogo tu kuhusu kile kilichompata yule Mtume Tomaso.

Imeandikwa hivi: “Ikawa jioni ile siku ya kwanza ya juma, pale walipokuwepo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi, akaja Yesu akasimama katikati akawaambia ‘Amani kwenu’. Naye akisha kusema hayo akawaonyesha mikono yake na ubavu wake …” (Yon 20:19-20).

Kumbe wakati hayo yanatendeka mmoja wa wale thenashasa, Tomaso, aliyeitwa pacha, hakuweko pamoja nao alipokuja Yesu. Basi wale wanafunzi wengine wakamwambia: “Tumemwona Bwana”. “Akawaambia, mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, mimi sisadiki hata kidogo….” (Yoh. 20:24-25).

Basi baada ya siku nane wanafunzi wake walikuwemo ndani tena na Tomaso pamoja nao. Akaja Yesu, na milango imefungwa kisha akamwambia Tomaso: “Lete hapa kidole chako, nitazame mikono yangu; leta mkono wako unitie ubavuni mwangu wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye!” (Yoh 20:26-27)

Tunaambiwa: “Kuona ndiyo kuamini.” Na palepale yule Mtume Tomaso akajibu, akamwambia: “Bwana wangu na Mungu wangu.” (Yoh 20:28).

Ndiyo kusema Tomaso alijiona mtu tofauti sana na wenzake walipokuwa wakimweleza “tumemwona Bwana”, yeye alijibaraguza na kusema kuwa asipotia vidole vyake kwenye matobo ya misumari au asipotia mkono wake pale penye ubavu, hataamini chochote wanachosema wale wenzake.

Kumbe baada tu ya kuona ukweli, ninadhani alihofu sana kwa nini aliropoka ovyo namna ile ndiyo sababu kwa unyenyekevu mkubwa sasa akawa anajijutia na kujikuta kutamka maneno ya “Bwana wangu na Mungu wangu”. 

Hapo ndipo inakuja nguvu ya kuona ndiyo kuamini – ndiyo uthibitisho wa moyo. Kwa mtu yeyote asiyeamini, anafunguka macho yake baada tu ya kuona.

Rais pale Mwanza wkati wa maadhimisho ya sherehe za Uhuru alitoa hotuba nzuri sana yenye majumuisho ya maendeleo katika nchi yetu. Alieleza hali ilivyokuwa kabla ya Uhuru mwaka 1961, tulimopitia na hali ilivyo leo hii.

Baadhi ya uthibitisho aliowaeleza Watanzania ni kama pale alipotamka: “Tumefanya mengi ya kujiletea maendeleo katika awamu zote kwa miaka 58 ya Uhuru. Lakini msingi mkuu wa mafanikio yote ni amani, umoja na ushirikiano miongoni mwa Watanzania. Serikali imewahakikishia wananchi kuendelea kulinda na kudumisha amani hiyo”.

Kazi ya kuendeleza taifa si lelemama. Viongozi na waasisi wa taifa hili wamefanya mengi kwa mafanikio makubwa licha ya kuwa na changamoto nyingi. Ni jukumu letu kizazi cha sasa kuendeleza na kulinda mema yote yaliyoasisiwa na kusimamiwa na waasisi wetu.

Taifa limesomesha na kupata wataalamu, limeboresha na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji, limejenga viwanda vingi na linalenga kwenye kujitegemea, kama taifa huru.

Rais alitoa takwimu kulinganisha mwaka 1961 na mwaka 2019. Mathalani kwa upande wa afya alieleza wazi kuwa mwaka 1961 walikuwapo madaktari Watanganyika 12 tu, wakati leo hii tunao madaktari Watanzania 9,400. Wakati tulipopata Uhuru hospitali zilikuwa 98, sasa zipo hospitali 178, vituo vya afya vilikuwa 22 tu, leo hii vipo vituo 795, zahanati zilikuwa 975 tu, hivi sasa tunazo 6,285.

Umefanyika ujenzi wa barabara za lami na madaraja nchi nzima. Kwa upande wa elimu alisema shule za msingi zilikuwa 3,100 tu, leo hii zipo shule za msingi 17,379. Haya ni baadhi tu ya mambo makubwa ambayo nchi imeyafanya katika miaka 58 iliyopita.

Hapa ningependa nimfananishe Rais Magufuli na Mwalimu Nyerere. Baadhi yetu wazee tunakumbuka sherehe za mwaka 1971, miaka 10 baada ya Uhuru. Wakati ule Baba wa Taifa alituambia: “….pale Bagamoyo mwezi Disemba 1961 nilisema maneno watu wakafikiri yalikuwa ya kujigamba, nilipowaambia wakoloni tupeni muda wa miaka 10, kisha mtakuja kuona Watanganyika tutakavyokuwa tumeendelea. Nitawaalika muje muone haya ninayosema.”

Na kweli kabisa mwezi wa Disemba mwaka ule wa 1971 baadhi ya watawala wakoloni walialikwa na serikali na wakapelekwa katika mikoa (majimbo) na wilaya walipoondokea baada ya Uhuru.

Gavana Jenerali wa mwisho kutawala Tanganyika, Sir Richard Turnbull, naye alifika akawa mgeni wa Mwalimu hapo Ikulu. Basi, Mwalimu aliamua kumtembeza Sir Richard Turnbull Arusha iliyoitwa “Northern Province” na Mwanza iliyoitwa “Lake Province”.

Walitembezwa kabla ya siku ya kilele cha sherehe za Uhuru ili waone hali halisi ilivyo na kuwapa fursa wakoloni wale kuona yaliyotokea katika miaka 10 ya kujitawala. Mwaka 1971, Mwalimu na mgeni wake Sir Richard walitoka Arusha kwenda Mwanza ambako Mwalimu alipangiwa kufungua rasmi ile Hospitali ya Bugando Disemba 3, 1971.

Safari ya kutoka Arusha kwenda Mwanza ilifanyika kwa ndege ya JWTZ aina ya Caribou. Sir Richard akisimulia mshangao wake pale Bugando Mwanza jioni ya Disemba 3, 1971 alitamka hivi: “Tumefika pale airport Arusha asubuhi leo na mara tukaingia ndani ya ndege ile ya jeshi. Mimi nilimuuliza rais, mbona mapilot hawapo? Nikaona Nyerere anacheka na kuniambia; “huwaoni wale kule mbele?” Nikasema: “Those Africans” (wale Waafrika?). Rais alinitazama na kusema; ‘ngoja uone’. Hapo kweli nilifunika uso wangu kwa mikono na kujawa hofu.” Akaendelea:

“Basi ndege iliwashwa, tukaruka na tulipofika maeneo ya Serengeti yule pilot aliishusha ndege ile kidogo na kutuambia tuwaone wanyama. Hapo mimi nilijisikia kama ndege ile inaanguka, nikalia “oh my God” (Oh Mungu wangu), wenzangu walicheka sana. Tulipotua hapa Airport Mwanza nilisema “Julius”, “Well done!”. Nikamshika mkono yule rubani na kumwambia “Bravo”.

“Nimeona mambo mengi ya maendeleleo yenu hasa hili la Mwafrika kurusha ndege limenishangaza sana. “You have really achieved tremendous development in the past 10 years of your independence in this country” (mmepata maendeleo makubwa katika kipindi cha miaka 10 ya Uhuru wenu).

Hayo ni baadhi ya matamshi ya wakoloni mwaka ule 1971, miaka 10 baada ya kujitawala. Kule kumvulia kofia na kumsifia Mwalimu Nyerere alikoonyesha mkoloni gavana yule ni kukiri kuwa yametokea mabadiliko katika nchi waliyoitawala.

Nadhani lilikuwa jambo jema na la kistaarabu. Yule kapteni wa jeshi aliyerusha ile Caribou na mpaka mtawala aliposema walipotoka Tanganyika hapakuwa na Mwafrika hata mmoja mrusha ndege! Huyo alikuwa Kapteni Matiro wa JWTZ Airwing.

Leo hii mwaka 58 wa Uhuru wetu wapo hao kina Matiro (yaani marubani warusha ndege) wangapi? ATCL peke yake wako 94, ndege binafsi kama Coastal Air, TANZANAIR, Precision Air, JWTZ na Polisi, tunao warusha ndege chungu nzima. Huu si muujiza, bali ni uhalisia wa maendeleo yetu Watanzania.

Mbenna ni Brigedia Jenerali mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)

ITAENDELEA…