Jumapili Januari 26, 2020 waamini wa Kanisa Katoliki Tanzania, Kata ya Kitunda, Dar es Salaam wametabaruku Kanisa na Altare. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, ndiye aliyelitabaruku Kanisa hili lenye historia iliyotukuka.

Mwandishi Deodatus Balile, naye ameandika Kitabu cha Historia ya Parokia ya Roho Mtakatifu Kitunda, ambacho kinaeleza safari ya Ukristo kwa Kata ya Kitunda, Dar es Salaam. Makala hii, ni historia ya Kanisa la Kitunda kwa ufupi, kama ilivyotolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei, Dk. Donald Anthony Mwiturubani. Paroko wa Kirunda, Padri James Mweyunge, anatoa neno la shukrani pia. Endelea…

SHUKURANI

Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa Afya, Neema na Baraka tele alizowajalia Wana-Kitunda kuifikia siku hii ya Kutabaruku Kanisa letu jipya na Altare yake tulilolijenga kwa nguvu zetu wenyewe. Uzima aliotujalia Mungu ndiyo umetuwezesha kudhihirisha ukarimu wetu kwa kutenda mambo makubwa tunayoyashuhudia leo watu wa Mungu. Naamini kama tulivyojitoa na kukamilisha ujenzi wa Kanisa hili zuri, Mungu atatujalia na kuendelea kutubariki tuweze kukamilisha mengine mengi makubwa yaliyoko mbele yetu.

Kwa niaba ya Parokia yetu na Viongozi wake, napenda kumshukuru Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam kwa kukubali kulitabaruku Kanisa hili na Altare yake. Baba tunakuombea Mungu azidi kukupa moyo wa upendo na afya njema.

Kipekee tunamshukuru Mwadhama, Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu mstaafu, aliyeridhia na kuitangaza Parokia ya Roho Mtakatifu Kitunda kutoka Kigango na kuwa Parokia ambayo leo inamulika taa ya ukuaji wa imani kwa Kutabaruku Kanisa hili na Altare yake. Mungu azidi kukujazia rehema na afya njema.

Tunawashukuru wajenzi na wataalam mbalimbali walioshiriki katika ujenzi wa Kanisa hili. Mungu awabariki kwa majitoleo yenu.

Kipekee tunaishukuru Kamati Tendaji ya Parokia na Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi kwa moyo wao, majitoleo na mwongozo walioutoa muda wote bila kukata tamaa katika mkakati huu wa thamani kubwa wa ujenzi wa Kanisa hili. Tunaomba Mungu aendelee kuwabariki na kuwaneemesha katika yale yote mnayoyafanya kwa ajili ya kujenga ufalme wake bila kuchoka.

Mwisho, si kwa umuhimu, napenda kuwashukuru tena Wanaparokia wote kwa umoja, upendo, mshikamano, ushirikiano na moyo mkuu wa kujitolea mliouonyesha tangu tunaanza ujenzi, hadi leo tunapotabaruku Kanisa na Altare yake. Mimi kama Mchungaji wenu, mlinitia moyo, mlinifariji kwa majitoleo na mawazo yenu mazuri, kila mmoja kwa nafasi yake. Mungu azidi kuwabariki, kuwalinda na kuwaongezea pale mlipotoa wema wenu udumu daima.

Pd. James Mweyunge

Paroko

Parokia ya Roho Mtakatifu Kitunda

UTANGULIZI

Parokia ya Roho Mtakatifu Kitunda ilitangazwa rasmi kuwa Parokia tarehe 07/07/2010 na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo katika sherehe za Upadrisho zilizofanyika katika Parokia ya Kristo Mfalme, Tabata, Dar es Salaam. Kabla ya kutangazwa kuwa Parokia, Kitunda ilikuwa mojawapo ya vigango vinne vya Parokia ya Mt. Augustino Ukonga. Vigango hivi vilikuwa ni Roho Mtakatifu Kitunda; Magole; Mt. Monica Mazizini na Mt. Polycarp Mwanagati. Parokia ya Roho Mtakatifu Kitunda iko Kata ya Kitunda, Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es salaam. Parokia iko umbali wa takribani kilometa 4 kutoka Banana, jirani na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (JKNIA). Parokia ya Kitunda Mashariki inapakana na Parokia za Kizinga na Buza; Kusini: Parokia ya Kivule; Magharibi: Parokia ya Ukonga; Kaskazini: Parokia ya Kipawa. Kitunda ni moja ya Parokia 13 zinazounda Dekania ya Ukonga. Parokia nyingine za Dekania ya Ukonga ni; Ukonga, Pugu, Chanika, Mji Mpya Relini, Yombo Kiwalani, Yombo Dovya, Yombo Vituka, Buza, Kivule, Mwanagati, Chakenge (Parokia Teule) na Msongola (Parokia Teule). Parokia ya Kitunda ni mojawapo ya Parokia zipatazo 118 za Jimbo Kuu la Dar es salaam.

Mchakato wa kupata Parokia ya Roho Mtakafitu Kitunda uliwezeshwa na uamuzi wa waamini wa Parokia hii kujenga nyumba ya Mapadri Kitunda iliyoanza kujengwa mwaka 2007 na kukamilika 2009. Nyumba hii iligharimu Shilingi Milioni 100 hadi kukamilisha ujenzi wake. Fedha hizi zilitokana na michango ya waamini. Baada ya kukamilisha ujenzi huu, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam (wakati huo), Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alifuraishwa na moyo wa waamini kujituma hivyo akaahidi kuwa ndani ya muda mfupi Kigango cha Kitunda kingetangazwa kuwa Parokia. Mwaka uliofuata 2010, Mwadhama Kardinali Pengo aliitangaza Kitunda kuwa Parokia. Pia Kardinali Pengo alimtangaza Padri James Mweyunge kuwa Paroko wa kwanza wa Parokia mpya ya Kitunda.

Baada ya kutangazwa kuwa Parokia, waamini walianza mchakato wa kujenga Kanisa kubwa na la kisasa kwani Kanisa walilokuwa wanalitumia lilikuwa dogo lenye uwezo wa kuchukua waamini wachache tu, hivyo waamini wengi walikuwa wanasalia nje. Paroko Mweyunge alieleza nia yake ya kujenga Kanisa kubwa lenye uwezo wa kuchukua hadi watu 2,000, hivyo kazi ya kuandaa michoro na kupata vibali vya ujenzi ikaanza. Kanisa la Parokia ya Kitunda lilianza kujengwa Julai, 2012. Kwa nguvu za waamini wa Kitunda bila mfadhili kutoka sehemu yoyote, Waamini wamelijenga Kanisa hili kwa miaka 7 kwa utaratibu wa kuchangia ujenzi kila wiki. Hadi ujenzi wa Kanisa hili unakamilika limegharimu wastani wa Shilingi Bilioni 2.

Parokia ya Kitunda ilipoanzishwa ililirithi vigango viwili vya Magole na Mwanagati. Parokia ya Kitunda imevilea vigango hivi na imezaa Parokia mbili za Mt. Theresa wa Kalkuta Kivule (2016) na Mt. Veronica Mwanagati (Januari, 2019). Parokia ya Kitunda inao waamini wapatao 8,500 (Sensa ya Parokia 2016/2017).

HALI YA IMANI

Parokia hii imepata mafanikio makubwa kiimani tangu ilipoanzishwa. Parokia imekua kutoka Jumuiya moja enzi ikiwa Kigango hadi Jumuiya 52 kwa sasa. Tangu ikiwa Kigango hadi sasa imebatiza, imetoa Komunio, Kipaimara na imefungisha ndoa kama zinavyoonyesha takwimu za kuanzia mwaka 2011. Takwimu za kabla ya Mwaka 2011, zinabaki katika Parokia Mt. Agustino, Ukonga ilikozaliwa Parokia ya Kitunda. Takwimu zinaonyesha kuwa kuanzia mwaka 2011 hadi 2019 idadi ya waliopoata huduma za kiroho, yaani Ubatizo (4,275); Komunio (2,597) Kipaimara (3,047); Ndoa (525); Kupokelewa kutoka madhehebu mengine (61) kama ilivyochanganuliwa hapa chini.

MIITO YA KITUME (WATAWA)

Parokia ya Roho Mtakatifu Kitunda katika kipindi cha miaka 7 imefanikiwa kuzalisha miito. Parokia imepata Watawa watatu, ambao ni Mapadri wawili; Pd. James Wendelin Ngonyani, aliyepadirishwa July, 2016 kutoka Jumuiya ya Mt. Yohane XXIII na Pd. Ayubu Mwang’onda kutoka Jumuiya ya Roho Mtakatifu aliyepandirishwa Julai 03, 2014. Padri huyu ni wa Shirika la Salvatorian. Sista aliyeitikia wito kutoka Parokia ya Kitunda ni Sr. Filomena OSB. Aliweka Nadhiri za Kwanza Mwaka 2017. Chimbuko la Sista huyu ni Jumuiya ya Mt. Laurent Shahidi, ingawa kwa sasa wazazi wake wamehamia Chakenge, Parokia ya Mji Mpya Relini.

UTENDAJI WA VYAMA VYA KITUME

Hadi sasa Parokia ina vyama vya Kitume au Mashirika na Jumuiya za Kitume 9 ambazo ni; Utume wa Wanaume Katoliki Tanzania (UWAKA), Umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), Vijana Wafanyakazi Wakatoliki (VIWAWA), Utume wa Kwaya Katoliki Tanzania (UKWAKATA), Utoto Mtakatifu, Karismatiki Katoliki, Neokatekuminato, Legio Mariae na Kolping. Vyama hivi vimeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kufuata Mwongozo wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam katika kutangaza neno la Mungu. Vyama hivi vimeshiriki kwa mwavuli wa Parokia katika matamasha na safari mbalimbali za ngazi ya Dekania na Jimbo ikiwamo Hija Pungu, Visiga Seminari, Bagamoyo na Kituo cha Dada Wadogo Mbagala. Utoto Mtakatifu nao wameshiriki matukio ya kijimbo na kitaifa, ingawa ushiriki wao umekuwa si wa kuridhisha hivyo wazazi wanapaswa kuongeza nguvu kuimarisha imani. Makongamano na safari hizo, zimeimarisha na kukuza imani katika Parokia ya Kitunda.

MAPADRI WALIOHUDUMIA PAROKIA HADI SASA

Kabla ya kutangazwa kuwa Parokia, Mapadri kadhaa wamehudumia Kigango cha Kitunda kama inavyotajwa katika Kitabu cha Historia ya Parokia ya Kitunda. Tangu Kitunda imetangazwa kuwa Parokia, Mapadri walioihudumia ni:-

Paroko: Pd. James Mweyunge

Maparoko Wasaidizi:

Pd. Maximillian Wambura

Pd. Israel Slaa

Pd. Dismas Kimboi

Pd. Kalikawe Bigirwamungu

Pd. Paul Njoka

Pd. Urbanus Riziki Ngowi

VIONGOZI WA KAMATI TENDAJI HALMASHAURI YA WALEI TANGU JUMUIYA, KIGANGO HADI PAROKIA 1995 HADI 2019

JUMUIYA:

1995 – 1998:

Aloyce Paul Lyimo/

Mwl. Andrew Phiri – Mwenyekiti

Triphonia Komba – 

Makamu Mwenyekiti

Denis Aloyce Paul Lyimo – Katibu

Natalia Aloyce Lyimo – Mhazini

KIGANGO:

1998 – 2001:

Mwl. Andrew Phiri – Mwenyekiti

Marry Kimario – 

Makamu Mwenyekiti

Ambrosina Alphonce Mwailafu – 

Katibu

Charles Nyamuhisi – 

Katibu Msaidizi

Georgina Kasansa – Mhazini

2001 – 2004:

Mwl. Andrew Phiri – Mwenyekiti

Kayusi Tebuye – 

Makamu Mwenyekiti

Christopher Juma – Katibu

Felista Njali – Katibu Msaidizi

Magreth Maregesi – Mhazini

2004 – 2007:

David Moshy – Mwenyekiti

Baltazar Massawe – 

Makamu Mwenyekiti

Christopher Juma – Katibu

Felista Njali – Katibu Msaidizi

Victor Kabeya, baadaye 

Dk. Daudi Chacha – Mhazini

2007 – 2010:

Syliveter Mchaka – Mwenyekiti

Mzee Archard Rugaimukamu – 

Makamu Mwenyekiti

Simon Nguka – Katibu

Catherine Msira – Katibu Msaidizi

Joseph Mabusi – Mhazini

Jan. 2010 – Agt. 2010:

Eng. Justin Mulebya – Mwenyekiti

Mary Ngowi – 

Makamu Mwenyekiti

Augustino Komba – Katibu

Sandrika Mikongoti – 

Katibu Msaidizi

Joseph Mabusi – Mhazini

Aug. 2010 – 2013:

Syliveter Mchaka – Mwenyekiti

Eng. Justin Mulebya – 

Makamu Mwenyekiti

Simon Nguka – Katibu

Kelvina Mwingira – 

Katibu Msaidizi

Francisca Muro – Mhazini

2013 – 2016:

Dk. Daudi Chacha – Mwenyekiti

Aristides Rwegamba – 

Makamu Mwenyekiti

Simon Nguka – Katibu

Magreth Maregesi – 

Katibu Msaidizi

Francisca Muro – Mhazini

2016 – 2019:

Dk. Daudi Chacha – Mwenyekiti

Eng. Justin Mulebya – 

Makamu Mwenyekiti

Simon Nguka – Katibu

Oscar Andrea – Katibu Msaidizi

Joseph Mabusi – Mhazini

VIONGOZI WA KAMATI ZA UJENZI

NYUMBA YA MAPADRI:

Mzee Joseph Mallya; na

David Moshy

JENGO LA KANISA: 

Dk. Daudi Chacha; Simon Dollogo 

na Mzee Sylivester Mchaka

CHANGAMOTO ZINAZOIKUMBA PAROKIA

Mojawapo ya Changamoto zinazoikabili Parokia yetu ni Utume wa Wanaume Katoliki Tanzania (UWAKA), ambao ukiachia kuwa na mahudhurio hafifu katika ngazi ya Jumuiya, utendaji wao katika utume si wa kuridhisha. Mara kadhaa ushiriki wao katika matukio mbalimbali ya utume kama vile hija, umekuwa ni hafifu. Bado panahitajika mbinu za kufaa ili kuwapa hamasa Wanaume watambue nafasi yao katika utume ndani ya Kanisa.

Changamoto nyingine ni ya Viwawa ambao mara kadhaa ushiriki wao ndani ya Jumuiya zetu umekuwa ni wa kusuasua mno. Pengine kutokana na ukweli kuwa siku za Jumamosi vijana wengi wanashiriki mazoezi ya viungo asubuhi maarufu kama “jogging”, huenda haya yakawa ni maeneo yanayowameza vijana hata kutoshiriki ibada za Jumuiya.

Dk. Donald Anthony Mwiturubani 

MWENYEKITI – HALMASHAURI YA WALEI

PAROKIA YA KITUNDA

JANUARI 26, 2020