Ndugu Rais na wanao wapinzani karibuni mezani kwangu huku Mbagala kijijini. Chini ya mwembe huu panakumbusha mahali alipozaliwa Yesu Kristu, kwa imani ya Wakristu, mkombozi wa dunia. Alizaliwa ndani ya zizi la ng’ombe. Mwenyezi Mungu ayabariki malango yake yule mwanamwema aliyeniwezesha kukanyaga mahali pale patakatifu! Huu ndiyo mwembe alioufanya Bwana. Chini ya mwembe huu ndipo kilipoandikwa kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu. Kitabu ambacho kimetumiwa na wasomi wengi ndani ya nchi na nje ya nchi yetu kupata shahada zao za juu kabisa!

Ni kitabu hiki ambacho kiliwafanya wabobezi wa vitabu huko duniani kunialika katika maonyesho ya vitabu makubwa duniani ya Frankfurt, Ujerumani na baadaye maonyesho ya vitabu ya Afrika yaliyofanyika Cape Town, Afrika Kusini.

Lilifanyika kongamano kubwa katika Chuo cha Dar es Salaam ambapo washiriki wake walikuwa maprofesa na wasomi mbalimbali wa elimu ya juu kutoka katika nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini na sehemu nyingine. Kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu au kwa Kiingereza, The People’s Schoolmaster kilikuwa moja kati ya mazungumzo yao. Kama mwandishi nilialikwa, nami kwa mara ya kwanza nilipanda jukwaani katika Ukumbi wa Nkrumah na kuuhubiria umati ule mkubwa wa wasomi waliobobea! Kwa hili, sifa na utukufu zimrudie Muumba wangu. Mwanamwema Profesa Eliya, muandaaji, na vijana wako wasomi Yohani Wakota, Yunus na wenzao wote, malango yenu yabarikiwe sana! Kitengo cha Literature UDSM Bwana akiinue.

Ndugu Rais na wapinzani karibuni hapa chini ya mwembe huu, kwa kuwa hapa ndipo iliasisiwa MwalimuForum! Wanawema kwa uzalendo wao wa kuipenda nchi yao na wananchi wenzao, Juvenalis Ngowi, Namelock Sokoine, Edward Madenge, Baraka kutoka Zanzibar walikaa chini ya mwembe huu na kunyambua hadidu za rejea kutoka katika maandiko ya kitabu hiki.

Hadidu ambazo zimeingizwa katika Tume maarufu ya Kenya – maarufu kama BBI – Building Bridges Initiative na sasa zinahubiriwa kama Injili kila kona ya Kenya! Naamini, kwa uwezo wake Muumba, amani ya kweli ya nchi yetu iko chini ya mwembe huu.

Wanawema tunashuhudia uhasama mkubwa kati ya watawala na wapinzani. Wamekosa baraka za Mungu. Hakuna mtetezi wa wanyonge kati yao. Wote wamejaa uchu na uroho wa madaraka. Wasiyonayo wanayataka kwa liwalo na liwe wakati walionayo wamejiapiza hakuna kuyaachia, liwalo na liwe! Wamekengeuka!

Abarikiwe mwanamwema, Mwanisawa wa Ilambila, Kalambo – Sumbawanga kunijulisha kuwa makala hizi zinabandikwa kwenye kuta mbalimbali za baa na sehemu zingine za kimaendeleo ili zisomwe na watu wengi. Nawaombea baraka za Mungu watoto wake kwa upendo mkubwa kwangu japo hawanifahamu. Wakue wakiipenda nchi yao na Mungu wao na Watanzania wote kama wanavyonipenda mimi! Wajue hakuna wa kuwakomboa bali wao wenyewe! Wasiogope wawezao kuua mwili, bali yule awezaye kuua mwili na roho.

Ndugu Rais, jukumu la kwanza na la muhimu kuliko yote la serikali yoyote ya watu ni kulinda uhai wa watu wake na kuhakikisha usalama wao na mali zao. Unyama ukitendeka katika nchi, wa kwanza kuelekezwa kidole na wananchi ni serikali yao.

Hata hapa kwetu, ilipozama meli ya Mv Bukoba, vidole vyote vilielekezwa kwa serikali. Sasa kusema aliyekuwa anaendesha meli hakuwa Rais ni utetezi usiofaa. Inawezekana ulikuwa ni uzembe wa mtu mfulani lakini nchi ni Rais, serikali lazima ikubali lawama.

Wanawema watu wa serikali wanapowaambia wananchi kuwa kuna watu wasiojulikana katika nchi, ambao wanaendesha vitendo vya kinyama kuua watu, kuwapoteza, kuwateka na kuwatesa na wengine kuwashambulia kwa risasi, eti na serikali yao nayo haiwajui; labda ni kwa kutokujua au kwa uelewa wao mdogo kuwa wanaipotezea serikali uhalali na sababu ya kuwapo kwake.

Mahali popote panapolindwa pakitokea hitilafu ya kutia shaka, wa kwanza kuelekezewa vidole ni walinzi. Serikali ndiyo mlinzi mkuu wa wananchi katika nchi yoyote. Yanapotokea madhila kama haya, wananchi kama walivyo wanadamu wengine wote wakiinyoshea vidole serikali, ajabu yake inatoka wapi? Wasipomnyoshea baba yao kwa kumlilia, wamnyoshee nani? Sisemi mimi lakini walisema, mahakamani, mwizi hujishika mwenyewe.

Ndugu Rais, ninachosema ni kwamba kwa hapa tulipofikia hakuna chochote kitakachoiacha nchi hii na watu wake salama zaidi ya maridhiano. Yatupasa kama taifa tukae chini tuzungumze. Anayejiona hawezekaniki, alaaniwe na sisi wote asituletee machafuko katika nchi.

Ndiyo maana, baba naomba kama itawapendeza njooni tukae chini ya mwembe huu alioufanya Bwana tuyazungumze. Baba kwa ubinadamu wetu haiwezekani uwaongoze watu wako kwa muda wote huu wasiwe na lolote la kukuambia; au wewe la kuwaambia katika mfumo wa kero.

Ndugu Rais, ninayewakaribisha katika maridhiano, tangu kuzaliwa kwangu mpaka ninafikia umri huu sijawahi kuwa rais wa nchi. Ila ninachojua ni kwamba nikipewa fursa ya kuwaongoza marais hata wote, nitawaongoza vema kabisa. 

Nilikuwa sijawahi kuendesha pikipiki. Nilipofikiri sawasawa nikajua kuwa unatakiwa ujue ‘kubalance’ yale matairi mawili usianguke na kujua wakati gani unatakiwa kubadili gia. Sasa kama ninaweza kuendesha baiskeli vema na sasa ninaendesha mkweche wangu ambao ni ‘manual’, nitashindwaje kuendesha pikipiki? Nikawasha pikipiki nikaendesha mpaka nyumbani kwangu kwa mara ya kwanza tangu kuzaliwa bila kufundishwa na mtu.

Ukiweza kufikiri sawasawa hakuna kazi ngumu duniani. Kazi yoyote unayoifanya, hasa kama umeifanya kwa kitambo, haipaswi kuwa ngumu. Ukiona ni ngumu, jua unavyoifanya sivyo! Unaikosea! Kama ni ukuli, watazame makuli wenzako. Kama ni udaktari, watazame madaktari wenzako. 

Ingekuwa ni kwa amri yao, Robert Mugabe na wengine wangefia katika urais. Hata baada ya miaka zaidi ya 20 Nyerere hakuacha urais kwa sababu ya ugumu. Kazi ya uongozi inataka nguvu ya ufahamu na uelewa zaidi kuliko nguvu za misuli yetu iliyoko katika mikono au miguu yetu.

Baba, karibu hapa mwembeni tuliondoe hili wingu jeusi lililoifunika nchi yetu. Njoo baba ukae na wanao chini ya mwembe huu ambao Mwenyezi Mungu kwa kuwapenda waja wake amewashushia tunu ambayo sasa inawastawisha watu wa mataifa. Chini ya mwembe huu hamtakuwa tena baba na wanae, bali wana mliotoka katika udongo mmoja wa mama yenu, Tanzania.