Januari 9, mwaka huu Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) lilitangaza matokeo ya mitihani mitatu ya kitaifa iliyofanyika mwaka jana. 

Baraza la Mitihani lilitangaza kwa pamoja matokeo ya mtihani wa kujipima wa darasa la nne, kidato cha pili na ile ya kidato cha nne. Wakati akitangaza matokeo hayo, Katibu Mkuu wa Baraza hilo, Dk. Charles Msonde, alisema ufaulu kwa kila darasa unaendelea kupanda na kuongezeka ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Akitoa mfano, Dk. Msonde alisema kwenye mtihani wa kujipima wa darasa la nne, pamekuwa na ongezeko la asilimia 26.21 la idadi ya wanafunzi wanaofaulu na kuwa na sifa ya kuendelea na darasa la tano kutoka wanafunzi 1,213,132 mwaka 2018 hadi 1,531,120 mwaka huu.

Katika matokeo ya kidato cha pili, napo pana ongezeko lililofikia asilimia 90.04 ya watahiniwa waliofanya vizuri kwenye mtihani huo na wanaoendelea na kidato cha tatu, huku kidato cha nne ufaulu ukiongezeka kwa asilimia 1.38 kutoka asilimia 79.27 mwaka 2018 hadi asilimia 80.65 mwaka huu.

Lakini, licha ya ufaulu huu kuongezeka kwa kila eneo na mwaka, lipo jambo la kutafakari katika matokeo haya. Jambo moja ambalo limekwisha kuanza kuzoeleka miongoni mwa wananchi kwa sababu limeanza kuota mizizi ni matokeo ya shule nyingi za umma (za serikali) na wanafunzi wake kutofanya vizuri, ikilinganishwa na shule za binafsi (private schools).

Shule nyingi za umma kwenye matokeo hayo zimeendelea kuwa wasindikizaji nyuma ya shule za binafsi zinazoonekana kutawala kwenye madaraja yote ya juu ya ufaulu. Hali hii haijionyeshi kwenye matokeo ya mwaka huu tu, ni hali ambayo imekuwepo kwa miaka kadhaa sasa.

Shule za umma zimeendelea kupotea kwenye ushindani wa shule kumi bora na hata wanafunzi wake kuingia anga hizo, huku pia idadi kubwa ya shule zinazoongoza kufanya vibaya na kushika mikia zikiwa ni za umma.

Mfano tu kwa matokeo ya mwaka huu kuanzia yale ya darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne, shule za umma na wanafunzi wake wamekosekana kabisa katika orodha ya shule kumi bora huku shule nyingi za umma zikijazana kwenye nafasi za chini kabisa.

Shule 10 zilizofanya vizuri kuanzia darasa la nne mpaka kidato cha nne zote ni shule binafsi huku wanafunzi walioingia 10 bora pia kuanzia kwa wa jumla, wasichana kwa wavulana wakiwa ni kutokea pia shule binafsi.

Kupitia matokeo haya na ya miaka ya hivi karibuni, inaonekana wazi kabisa jinsi shule za binafsi zinavyoongeza pengo kati yake na shule za umma katika suala la ufaulu.

Yaani hata shule nyingi za umma zilizokuwa zikifanya vizuri na kushika nafasi za juu kwenye mitihani ya kitaifa miaka ya nyuma, zimefifia katika miaka ya hivi karibuni. Hivi sasa shule hizo hazisikiki tena, ukiacha zile zifa zake za miaka ya nyuma.

Shule kubwa, kongwe na za mfano kama Mzumbe, Ndanda, Bwiru, Ilboru, Songea Boys na Girls, Kilakala, Tosamaganga, Mtwara Tech, Arusha Tech, Mkwawa, Msalato na nyingine nyingi zilizokuwa zinatamba vilivyo miaka ya nyuma, siku hizi hazionekani tena katika orodha ya shule kumi bora kwa ufaulu.

Shule za umma zinakwama wapi?

Hili linaweza kuwa eneo la kwanza kabisa kulitafakari juu ya matokeo haya ya mitihani ya kitaifa kwa shule za umma. Tukumbuke shule hizi ndizo zimekuwa zikichukua idadi kubwa sana ya Watanzania ukilinganisha na shule za binafsi, kwani si wazazi wengi wa Kitanzania wana uwezo wa kuwapeleka watoto wao kwenye shule za binafsi ambazo tunajua gharama zake kidogo zinakuwa juu. Kwa hiyo tatizo lolote kwa shule za umma ni tatizo kwa taifa zima, kwani huko ndiko kuliko na Watanzania wengi.

Mkwamo wa shule nyingi za umma unaweza kuangaliwa kwa kugusia maeneo machache kati ya mengi katika mpangilio wa shule zenyewe. Je, miundombinu ya kusomea na kujifunzia kwa shule zetu za umma ikoje? Hapa tunaangalia vitabu, maabara, madarasa na mabweni kama yapo ya kutosha ama la.

Baada ya hapo tujiulize, je, miundombinu iliyopo inajitosheleza? Hamasa ya wanafunzi kujifunza kwa shule za umma ikoje? Hamasa inayotokana na uwepo wa mazingira rafiki na wezeshi kwa mwanafunzi kujifunza na mengine mengi.

Tafakuri ya mkwamo huu wa shule zetu za umma lazima ihusishe pia mijadala ya wadau mbalimbali ikiongozwa na serikali, kujadili namna ya kuondoka katika hali hii. Wapi panalega kwenye shule za serikali na kusababisha shule zetu kushindwa kufanya vizuri katika mitihani?

Tuna walimu wenye umahiri mkubwa wa kufundisha? Je, wapo wa kutosha? Je, kuna hamasa miongoni mwa wanafunzi kujifunza? Hayo na mengine mengi ni msingi wa kujua zinapokwama shule nyingi za umma na kusababisha kupigwa mweleka na shule za binafsi. Tuendelee kutafakari.

Bwanku ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dodoma na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, kiuchumi, kimaendeleo na kijamii. 0657475347