Diwani wa Viti Maalumu (Chadema), Jasimin Meena, anatuhumiwa kughushi nyaraka zilizomwezesha kujipatia

mkopo wa Sh milioni 3.3 kutoka taasisi moja ya fedha ijulikanayo kwa jina la Heritage Financing, Tawi la Moshi.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo JAMHURI linazo, diwani huyo alighushi nyaraka kuonyesha kuwa Neema Mwendo mkazi wa Kijiji cha Shiri Njoro, kilichopo Kata ya Mnadani, Wilaya ya Hai, amekubali kumdhamini na yuko tayari mali zake ziuzwe endapo diwani huyo atashindwa kurejesha mkopo huo.

“Nawapa mamlaka wana kikundi… Heritage Financing na mawakala wake kwamba tukishindwa kulipa mkopo hata rejesho la wiki moja, mali hizo ziuzwe kufidia mkopo wote, riba pamoja na gharama zote za ufuatiliaji,” inasomeka sehemu ya hati hiyo ya dhamana.

Hata hivyo, akizungumza na JAMHURI nyumbani kwake katika Kitongoji cha Kitifu Juu, Neema Mwendo anasema

nyaraka zote zilitotumiwa na diwani huyo zikionyesha jina lake, saini yake na alama ya dole gumba ni za kughushi.

Katika maombi hayo ya mkopo, diwani huyo ameambatanisha na kile kinachodaiwa ni hati ya mauziano ya kiwanja kilichopo eneo la Mailisita, Kitongoji cha Kitifu Juu, Kata ya Mnadani ya Februari 20, mwaka 1990.

Hati hiyo ya kughushi inaonyesha kuwa, Neema Mwendo, alinunua eneo lenye ukubwa wa robo tatu ya ekari kwa Sh

milioni 12 kutoka kwa mtu aliyetajwa kwa jina la Samson Joram Kweka.

Hata hivyo, Neema anaendelea kudai kuwa hata nyaraka hizo nazo ni za kughushi. Akifafanua, Neema anasema mwaka 1990 Kata ya Mnadani ilikuwa ikijulikana kwa jina la Kata ya Machame Kusini, pia yeye alikuwa akijulikana kwa jina la Neema Saidi Urassa, kabla ya kubadilisha jina mwaka 1996 na kuitwa Neema Idd Mwendo baada ya kuolewa.

“Alikuja hapa akaniomba nimdhamini anachukua mkopo wa Sh milioni moja. Kwa vile ni mtu ninayemfahamu

sikuwa na shaka naye hasa ikizingatiwa kuwa yeye ni kiongozi ndani ya jamii. Akaniomba nimpe picha yangu, nikampa wakati anatoka ndani akaomba tupige picha ya pamoja nje ya nyumba yetu kama mdhamini wake na kweli tulipiga,” anasema.

Diwani huyo alitumia nyaraka hizo za kughushi kujipatia mkopo wa kutoka Haritage Finacing Tawi la Moshi.

Neema ambaye ni mjane na mjasiriamali anasema hakujua kama picha hiyo ingetumiwa kutengeneza nyaraka feki kuonyesha ametoa nyumba ya familia kama dhamana kwa diwani huyo.

Ameliambia JAMHURI kuwa mwaka 1990 unaodaiwa alinunua kiwanja, hakuwa ameolewa na baada ya kuolewa mwaka 1996 ndiyo akaingia kwenye nyumba hiyo na kwamba eneo hilo ni la urithi na hajawahi kulinunua yeye.

“Mimi Samson Jerom Kweka nikiwa na akili zangu timamu bila kushawishiwa na mtu yeyote, nimeamua kumuuzia kiwanja changu ndugu Neema Idd Mwendo, kiwanja kipo katika Kijiji cha Shiri Njoro, Kitongoji cha 

Kitifu Juu, chenye ukubwa wa robo tatu eka,” inasomeka hati hiyo ya kughushi.

Hata hivyo, licha ya kuahidi kukutana na mwandishi kwa ajili ya kutoa ufafanuzi wa tuhuma hizo, diwani huyo

amekuwa akipiga chenga na hata anapopigiwa simu amekuwa akiahidi kuwasiliana na mwandishi baada ya nusu saa, kisha kunyamaza bila kupiga simu.

“Msg nimeiona mpendwa, niko hospitali kwa sasa, naomba nikitoka nikutafute ili nitoe majibu,” unasomeka moja ya ujumbe wa majibu ya diwani huyo baada ya kutafutwa muda mrefu na mwandishi.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, James Manyama, anasema tuhuma hizo zimefikishwa ndani ya Jeshi la Polisi na jalada la uchunguzi wa tuhuma za kughushi nyaraka zinazomkabili diwani huyo limekwisha kufunguliwa.

Nyaraka hizo zinaacha maswali mengi, kwani katika mwaka ambao unatajwa kuwa mauziano yalifanyika, hakukuwa na kompyuta za kupiga chapa kama ambavyo nyaraka hizo zilivyo.

Aidha, katika mwaka huo haiyumkini kwa thamani ya ardhi katika eneo hilo kuwa kubwa kiasi hicho.

Mbali na hayo, kwa mwonekano wa haraka karatasi hizo hazionyeshi kuwa ziliandikwa mwaka unaotajwa.