Zoezi la usajili wa laini za simu kwa kutumia alama za vidole na Kitambulisho cha Taifa limeibua uzembe uliofanywa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA). 

Kwa kiasi kikubwa watu wengi wameshindwa kusajili laini zao za simu kwa wakati kutokana na kutokuwa na Kitambulisho cha Taifa.

Tangu zoezi la kusajili laini za simu lilipoanza miezi mingi iliyopita, ilijidhihirisha kuwa NIDA ni tatizo, kwani watu wengi walikwama kutokana na kutokuwa na vitambulisho hivyo na NIDA haikuonekana kuchukua hatua mahususi kukabiliana na tatizo hilo.

Wapo watu ambao walikwisha kukamilisha taratibu za kupata vitambulisho, lakini ni zaidi ya miezi minane sasa hawajapata vitambulisho hivyo.

Ikafika mahali hata NIDA wenyewe wakaliona hilo. Wakaanza kutoa namba badala ya vitambulisho ili kuwawezesha watu kusajili laini zao. Lakini hilo nalo likaonekana jambo zito kwa NIDA, kwani imefikia hatua sasa hata upatikanaji wa namba ni mgumu.

Ilifika wakati hata Rais Dk. John Magufuli akalazimika kuingilia kati suala hilo na kumuamuru bosi wa NIDA kwenda Morogoro kutoa vitambulisho kwa watu waliokuwa wanavihitaji. Kwa sababu suala hilo liliagizwa na rais, kweli bosi wa NIDA akaenda Morogoro kutoa vitambulisho lakini kasi ya kutoa vitambulisho ikaishia hapohapo Morogoro.

Wakati zoezi la usajili wa laini za simu likikaribia mwisho kulingana na tarehe zilizopangwa awali, Rais Magufuli baada ya kusikia kilio cha mamilioni ya Watanzania ambao walikwama kusajili laini zao kutokana na kutopatiwa vitambulisho vya taifa, aliongeza siku 20. Lakini hilo nalo linaonekana halikusaidia, kwani wengi bado wamekwama kutokana na sababu hiyo ya kutokuwa na vitambulisho.

Wakati zoezi la kutoa vitambulisho vya taifa lilipoanza, NIDA iliwahakikishia Watanzania kuwa ina kila rasilimali zinazohitajika kuhakikisha kuwa kila anayestahili kupata kitambulisho anakipata bila usumbufu. 

Ni miaka kadhaa sasa imepita lakini inaonekana kuwa idadi ya waliopata vitambulisho hailingani na malengo ambayo yalikuwa yamewekwa awali. Tunaamini kuwa kama NIDA ingekuwa imefanya kazi yake ipasavyo, tusingeona hivi sasa mamilioni ya watu wakishindwa kusajili laini zao kwa sababu tu hawana vitambulisho.

Kinachoshangaza ni kuwa hata ulipobadilishwa utaratibu na kuanza kutumia namba badala ya kitambulisho halisi, lakini hilo nalo linaonekana kuishinda NIDA, kwa sababu bado watu wengi wameshindwa kupatiwa hata hizo namba.

Ni wakati sasa wa NIDA kubadilika na kuifanya kazi yao kwa umakini. Sasa hivi ilipaswa kila mtu anayestahili kupata kitambulisho awe amepatiwa, inakuwaje hata namba zimekuwa shida kupatikana?