Ndugu Rais, wewe ndiye tuliyepewa uwe baba yetu sisi wote hapa nchini kwa wakati huu. Lakini baadhi yetu labda kwa kusikilizwa sana wanajiona wewe ni baba yao zaidi. Wajue wewe ni baba wa wote.
Tulikuwa pamoja sana kabla hujawa baba. Unawapenda Watanzania wote. Kwa unyenyekevu mkubwa ukilihutubia taifa letu, uliwaambia Watanzania kuwa: “Sitaki kutawala nchi ya watu waliojaa machozi”.
Watu wako walikuamini na ndiyo maana mpaka sasa bado wanakuona wewe ni mtatuzi mkubwa wa kero zao, ni wewe baba yao! Wape angalau matumaini ili waweze kuiona kesho yao kuwa ni bora zaidi kuliko leo.
Hivi karibuni kupitia vyombo vya habari Watanzania walimuona Mtanzania mwenzao kule Mwanza Kanda ya Ziwa akiwa makaburini.
Baba mtu mzima alikuwa akibubujikwa machozi mbele ya kaburi ambalo kumbe ndimo alimzika mwanaye. Alilia sana huku akisema kwa sauti: “Mwanangu umekwenda, sawa, hayo ni mapenzi ya Mungu! Lakini hili deni uliloniachia, mimi baba yako maskini nitalilipaje?”
Huyu mzee alikuwa akimuuguza mwanaye huyo katika hospitali mojawapo hukohuko Mwanza. Madaktari walijitahidi kumtibu kwa kila hali, lakini hatimaye yule mtoto alifariki dunia. Katika kutaka kuondoka hospitalini hapo ili aende akamhifadhi marehemu mwanaye aliambiwa kuna malipo atatakiwa kulipa kwanza ndipo akabidhiwe mwili wa mwanaye. Wanaita kikombozi!
Bili ilikuwa kubwa sana kwa huyu maskini kuweza kulipa. Hivyo walikubaliana kuwa watamkopesha maiti ya mwanaye akaihifadhi. Lakini akisha kuzika atafute fedha akalipe lile deni. Hivyo pamoja na kwamba alikuwa akilia sana juu ya kaburi la marehemu mwanaye, lakini uchungu ulikuwa unaongezeka kwa kujua kuwa hana mahali pa kuzipata fedha za kuilipa hospitali deni kwa kumkopesha mwili wa marehemu mwanaye!
Alikuwako baba mwingine ambaye yeye ilimlazimu kufanya kibarua cha kupasua mawe ili ajipatie fedha naye akalipe deni la hospitali baada ya kukopeshwa mwili wa mpendwa wake aliyefia hospitalini hapo baada ya kuuguzwa kwa muda mrefu. Gharama za kukomboa mwili zikawa kubwa sana. Akakubaliwa aupokee mwili wa mpendwa wake kwa mkopo.
Matukio haya ni mengi nchi nzima lakini yanaumiza sana. Kuwaambia waathirika hawa kuwa nchi yao ni tajiri sana ni kuwaongezea makali ya uchungu, kwa kuwa ni sawa na kuwachoma katika kidonda kwa msumari wa moto. Fedha ni nyingi sana na maskini hawa wanaziona zinavyotumika; lakini zinanunua nini kuwatatulia kero zao? Hakuna ajuaye!
Wanaona wanaletewa viberiti vya chuma badala yake ambavyo haviwasaidii kwa lolote. Inauma sana. Maskini na wanyonge wa nchi hii wamekata tamaa. Hawamwoni wa kuwakomboa atatokea wapi. Baba watupie jicho la huruma hawa watu wa Mungu.
Wakati Muhadhama Polycarp Kardinali Pengo anatoka hospitalini Muhimbili alikokuwa amelazwa, siku hiyohiyo walinijia wanawema na kunililia wakisema: “Mwalimu Mkuu, tulikuja na rufaa ya baba yetu kutoka Mwanza ili auguzwe na kutibiwa na hospitali kubwa zaidi ya Muhimbili. Tumeuguza lakini bahati mbaya kwa mapenzi ya Mungu, baba yetu amefariki dunia. Hospitali imetutaka tulipe mamilioni ya fedha ili tupatiwe mwili wa baba yetu tukauhifadhi. Tunakujulisha wewe sauti ya wasio na sauti kuwa sisi ni maskini sana, hivyo tumeamua kurudi kwetu Mwanza. Mwili wa mpendwa baba yetu tumewaachia wao wataufanya watakavyo. Nyumbani tukifika tutazika nguo zake, Mungu atatusikia.’’ Nilichowaambia ni kuwa mimi pia kama nyinyi sina cha kuwasaidia, lakini nawaahidi kuwa nitalia pamoja na ninyi.
Baba Muhadhama Polycarp Kardinali Pengo, ulipolazwa Muhimbili uliombewa na watu wengi, tena wa dini mbalimbali. Kutokana na mahubiri yako uliyoyatoa katika ukumbi wa Mwalimu Nyerere yalionyesha kuwa kuna baadhi ya wenye mamlaka makubwa katika nchi hii ambao wewe ukisema wanakusikia. Tumia hiyo nafasi ya pekee uwaombe wakubwa hao wawatupie jicho la huruma maskini na wanyonge hawa wa nchi hii.
Watambue kuwa Roma haikujengwa kwa siku moja. Wananchi wanaumia. Miradi mikubwa uliyoisifia wananchi pia wanapongeza. Wasihi kama itawapendeza waahirishe japo mradi mmoja tu. Fedha hizo kwa hakika zitaondoa kero nyingi kama si zote zinazowakabili maskini na wanyonge wa nchi hii.
Wakati kukiwa na wanafunzi wengi waliotakiwa kuanza darasa la kwanza na waliofaulu kuingia kidato cha kwanza lakini wameshindwa kujiunga kutokana na uhaba wa madarasa, inasikitisha sana kumsikia Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, akisema fedha kiasi cha Sh bilioni 240.95 zilizotolewa kama msaada na Mfuko wa Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE) zitasaidia kutatua tatizo hilo. Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo, alisema: “Ni fedha itakayosaidia kutekeleza mahitaji ya sera, ikiwemo ujenzi wa madarasa, vyoo na mahitaji ya walimu kulingana na idadi ya wanafunzi.”
Wako waliyoyasoma yale maandiko kwa kuyarudiarudia lakini wakabaki hawaelewi kitu. Yaani serikali ya watu iliyopeleka bajeti ya Wizara ya Elimu bungeni ikapitishwa bila kupunguzwa, inashindwaje kununua madawati tu?
Hata kuchimba vyoo tu? Lakini haiingii akilini nchi tajiri kama inavyohubiriwa kila asubuhi kukosa fedha za kuongeza vyumba vya madarasa. Si kujenga shule nzima kumbuka! Tunajenga reli na kununua ndege, hao watalaamu wetu wenyewe tunaotarajia waje watuendeshee hayo makubwa tunayoyafanya si ndio hawa tunaoshindwa kuwajengea vyumba vya madarasa sasa?
Wako wanaoulizana, hii ina maana kwamba bila msaada wa hawa Wazungu ambao wengine wanawaita mabeberu, elimu ya watoto wetu waliokosa madarasa ndiyo ingekuwa imefika mwisho? Au tunataka kwanza tujenge matreni yenyewe ndiyo tukimaliza, tujenge madarasa ya kuwafundishia wataalamu wa kuja kutuendeshea? Watatucheka watu!
Ni vema sasa tukajipanga kutafuta majibu sahihi. Maridhiano ni kwa faida yetu. Kutegemea hila kama tulivyofanya kule mitaani, ni kujipumbaza wenyewe.
Maandiko yanasema: ‘Kiingiacho kwa hila, kitaondoka kwa hila’. Walioingia kwa hila huko mitaani na vijijini maisha yao ni ya kujutia. Watu wasicheke wakipita, ‘Wanawacheka wao.’ Watu wasinune wakipita, ‘wanawanunia wao.’ Jamani! Kila akutazamaye anakukumbusha kisasi! Genge la kununua mahitaji ni moja. Msikiti na kanisa ni pamoja. Wanaishi katika maumivu makali ya moyo. Wanajutia uhuni uliotendeka!