Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) imefichua ufujaji wa fedha zinazotengwa na makandarasi kwa ajili ya kutoa elimu juu ya maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa jamii inayozunguka maeneo yao ya miradi.
Fedha hizo hutengwa na makandarasi kutoka kwenye ukadiriaji wa miradi (BOQ) na hutumika kutoa elimu kuanzia kwa wafanyakazi wanaohudumu kwenye miradi hiyo na kwa jamii inayozunguka maeneo ya miradi, ukiwa ni mkakati wa serikali wa kupunguza maambukizi ya virusi vinavyosababisha ugonjwa huo.
Hata hivyo, pamoja na nia hiyo nzuri ya serikali, Takukuru imebaini kuwa fedha hizo hazitumiki kwa malengo yaliyokusudiwa na wakati mwingine fungu hilo halitengwi zaidi ya makandarasi hao kuweka alama nyekundu ya mapambano dhidi ya ukimwi kwenye kila bango la mradi.
Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Holle Makungu, anasema timu ya ufuatiliaji wa miradi ya taasisi hiyo ilifanya ufuatiliaji katika kipindi cha Oktoba, Novemba na Disemba mwaka jana na kubaini kuwapo kwa ubadhirifu wa fedha hizo.
Anasema kwa mujibu wa uchunguzi wao, miradi mingi imewekewa kiwango cha kati ya Sh 500,000 hadi Sh milioni moja kutegemea na ukubwa wa mradi kwa ajili ya mapambano dhidi ya ukimwi, lakini kifungu hicho hakitumiki kama ilivyokusudiwa kwa makandarasi wengi.
Anasema fedha hizo zinapaswa kutumika katika kuhakikisha wataalamu wa afya na waelimishaji rika wanafika kwenye maeneo ya miradi na kutoa elimu sahihi ya namna bora ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Elimu hiyo kwa wafanyakazi wa miradi hiyo pamoja na jamii inayozunguka maeneo ya miradi ni katika kuwawezesha kupima afya zao na kujitambua, ikiwa ni pamoja na kuelimishwa namna bora ya kuwahudumia wanaoonekana wamekwisha kuathiriwa na virusi hivyo vya ukimwi.
Kutokana na udanganyifu huo, Takukuru imewakumbusha makandarasi kuwa wanachokifanya kuhusiana na fedha hizo ni kinyume cha sheria na kuonya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya mkandarasi atakayebainika kutumia fedha hizo kinyume cha makusudio.
Katika hatua nyingine, Takukuru imebaini kuwepo kwa ufujaji wa Sh milioni 24.6 zilizotengwa kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya Shule ya Msingi Meserani, iliyopo Wilaya ya Same.
Taarifa ya Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro kwa kipindi cha miezi mitatu ya Oktoba, Novemba na Disemba mwaka jana, inabainisha kuwa fedha hizo ni sehemu ya Sh milioni 137 kutoka kwa wafadhili kupitia mfuko wa Student Africa Canada ambazo zilipitishwa kwenye akaunti ya mtu binafsi.
Makungu anasema katika taarifa yake kuwa fedha hizo zimefujwa na wahusika kisha kuandaa na kutengeneza taarifa ya benki (bank statement) ya uongo wakieleza kuwa fedha hizo zilikuwa zimekatwa na TRA kama Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), huku wakifahamu kuwa jambo hilo si kweli.
“Ukaguzi wetu umebaini kuwa nyumba mbili za walimu, majengo mawili ya vyumba vinne vya madarasa pamoja na ofisi ya walimu yaliyopangwa kukarabatiwa vimefanyiwa ukarabati lakini jengo la vyumba viwili vya madarasa lililotakiwa kujengwa halikujengwa,” anasema.
Katika hatua nyingine, Makungu anasema katika kipindi hicho cha miezi mitatu, Takukuru imeweza kupokea taarifa 110 na kati ya hizo taarifa 73 zilionekana kuwa ni makosa ya rushwa huku taarifa 37 zikiwa hazina uhusiano na makosa ya rushwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Serikali za Mitaa zimeendelea kulalamikiwa na wananchi kwani taasisi hiyo imepokea taarifa 22 za rushwa kuhusiana na taasisi hizo.
Aidha, taarifa 16 zilihusu uchaguzi, taarifa 15 zililalamikia sekta binafsi, ardhi kulikuwa na malalamiko saba, vyama vya ushirika malalamiko sita, maji malalamiko sita pia, ujenzi malalamiko matano, misitu malalamiko manne, mabaraza ya ardhi malalamiko manne, Hifadhi ya jamii malalamiko matatu kama ilivyo kwa idara ya afya; Tanesco malalamiko mawili, huku TRA na Mahakama zikiwa na lalamiko moja kila moja.