Umekisia kisa cha Bi Juliana Kant Nyitambe, mkazi wa mkoani Mara na mwalimu mstaafu wa Shule ya Msingi Kotwo iliyopo wilayani Rorya ambaye alikopeshwa Sh 1,000,000 na kulipishwa kwa lazima Sh 39,000,000? 

Wakati anakopa aliambiwa riba ya mkopo huo ni asilimia 50, hivyo alitakiwa kulipa Sh 1,500,000 lakini kutokana na utapeli, akajikuta akilipishwa Sh 39,000,000! Fedha hizo zilikuwa ni malipo ya mafao yake baada ya kustaafu kazi serikalini.

Kisa hiki kilianza pale Bi Nyitambe alipokuwa anasubiri mafao yake. Baada ya kuitumikia serikali hadi anafikisha umri wa miaka 60, Bi Nyitambe alistaafu rasmi Disemba 30, 2018 lakini hakupewa mafao yake mara baada ya kustaafu. 

Alilazimika kusubiri, wakati akisubiri mafao hayo alipata shida ya dharura ambayo ilihitaji fedha kuitatua. Ndipo akamfuata mtu ambaye anaweza kumkopesha.

Akakutana na Matiko Tubeti, mkazi wa Wilaya ya Tarime ambaye alikubali kumkopesha Sh 1,000,000 kwa riba ya asilimia 50. Pamoja na sharti hilo, Bi Nyitambe alitakiwa pia amkabidhi mkopeshaji kadi yake ya benki pamoja na namba ya siri ya kadi hiyo kama dhamana. Kwa kuwa alikuwa na shida, akakubaliana na masharti hayo. Ilikuwa Agosti mwaka jana, takriban mwaka mmoja baada ya Bi Nyitambe kustaafu.

Kwa bahati nzuri, malipo yake ya kustaafu yalifanyika na fedha zikaingizwa kwenye akaunti yake mwezi Disemba mwaka jana.

Hapo ndipo sakata likapamba moto, kwani mkopeshaji alikomba fedha zote kutoka kwenye  akaunti ya mwalimu huyo mstaafu. Mkopeshaji aliweza kufanya hivyo kwa sababu alikuwa na kadi ya benki na namba yake ya siri. Akakomba Sh 39,000,000 zote kutoka kwenye akaunti ya Bi Nyitambe kwa maelezo kuwa ni malipo ya deni lake. Malipo hayo yanaonyesha kuwa riba ilikuwa ni asilimia 3,750.

Bi Nyitambe alifanikiwa kurejeshewa fedha zake zote lakini hilo lilitokea baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuingilia kati. Lakini tatizo lililomkuta Bi Nyitambe linawakuta wastaafu wengi na watu wengine wa kawaida ambao huibiwa fedha zao za mafao na za biashara na wakopeshaji matapeli ambao huwawekea masharti ya ajabu wanapowapa mikopo.

Inafahamika wazi kuwa suala la mtu kukopa ni la kawaida katika jamii ambayo watu wengi hawana uwezo wa kujitosheleza kwa mahitaji yao yote kila wakati. Mtu huchukua mkopo ili aweze kukidhi mahitaji yake kwa wakati uliopo, akiwa na uhakika kuwa baadaye atapata fedha za kurejesha mkopo huo.

Wakati mwingine mtu hulazimika kuchukua mkopo kutokana na matatizo anayokumbana nayo lakini wengine huchukua mikopo kama sehemu ya mipango yao ya biashara. Lakini ni vema kwa kila anayechukua mkopo kuwa na uhakika wa mambo kadhaa ili mkopo huo usilete matatizo kwake.

Kwanza, anayechukua mkopo ni lazima awe na mpango mzuri wa matumizi ya mkopo huo. Hii inamaanisha kuwa mtu asichukue tu mkopo kwa lengo la kupata fedha kwa ajili ya kula raha. Kama ni kwa ajili ya kutatua tatizo fulani, basi mkopo huo utumike kwa ajili hiyo. Kama ni mipango ya kibiashara, ni vema kuhakikisha kuwa fedha zitakazopatikana kupitia mkopo zinatumika vizuri katika biashara ili biashara hiyo iweze kulipa mkopo huo baadaye.

Tukirudi kwenye sakata la Bi Nyitambe, alilazimika kuchukua mkopo kwa sababu ya matatizo ya kijamii aliyokuwa anakabiliana nayo. Wakati huo alikuwa na uhakika kuwa atapokea fedha zake za mafao, hivyo atakuwa na uwezo wa kurejesha mkopo huo. 

Lakini jambo ambalo hakulitilia maanani ni masharti aliyopewa. Inawezekana kuwa hakuwa na wasi wasi kwa masharti hayo, kwa sababu hakuhisi kuwa anaweza kutapeliwa kiasi hicho. Ni pale fedha zake zote zilizpochukuliwa na mkopeshaji ndipo akalazimika kuripoti suala hilo katika vyombo vya dola.

Mkuu wa Takukuru mkoani Mara, Alex Kuhanda, anasema walipopata malalamiko kutoka kwa Bi Nyitambe, walifahamu fika kuwa kilichofanyika hapo ni utapeli, kwa sababu mtu hauwezi kukopeshwa Sh 1,000,000 halafu baada ya miezi michache tu deni lifikie Sh 39,000,000.

Anasema, hivyo walilazimika kumtafuta Tubeti na kumhoji. Walipomhoji walibaini kuwa hakuwa na msingi wowote wa yeye kuchukua fedha hizo zote za Bi Nyitambe, hivyo wakamlazimisha azirejeshe kabla hatua nyingine hazijachukuliwa dhidi yake.

Tubeti alirejesha fedha hizo kwa awamu. Awamu ya kwanza alirejesha Sh 15,000,000 Disemba 12 na Disemba 31 alikakamilisha kiasi cha Sh 24,000,000. Lakini mtu huyo hivi sasa anakabiliwa na tuhuma nyingine, ikiwamo kuendesha shughuli za mikopo bila ya kuwa na leseni za kufanya shughuli hiyo na kuifanya shughuli hiyo bila kufuata taratibu zilizowekwa kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na sakata hilo hivi karibuni, Kuhanda, amewatahadharisha wananchi kuhusiana na uwepo wa watu hao wanaokopesha wenzao kitapeli.

Kuchelewesha mafao

Janga hili halijatokea mkoani Mara pekee. Kuna mikoa mingine ambayo wastaafu na watu wengine wameshakumbwa na tatizo kama hili. Kwa kawaida, matapeli hawa wa mikopo huwalenga watumishi wa umma, hasa wale ambao muda wao wa utumishi umekwisha na wanasubiri mafao yao. 

Kwa sababu inachukua muda mrefu kulipwa mafao hayo, na kwa wakati huo wanakuwa hawana kipato cha uhakika, mara nyingi watu hawa hupatwa na matatizo yanayohitaji fedha kuyatatua.

Kwa upande mwingine, watumishi wa umma nao wanakuwa na mahitaji makubwa ambayo wakati mwingine huzidi vipato vyao vya mwezi, hivyo kuhitaji fedha za ziada ili kutatua matatizo hayo. Wanakimbilia kwenye mikopo wakiamini kuwa wanaweza kutumia mishahara yao kurejesha mikopo wanayochukua.

Wastaafu wengi hukumbwa na tatizo hili wakati wakisubiri mafao yao. Bi Veronica Kunenge, ambaye alistaafu kazi ya ualimu mwaka 2014 wakati akifundisha Shule ya Msingi Azimio, ameliambia JAMHURI kuwa baadhi ya wastaafu wanapitia kipindi kigumu kidogo wakati wakisubiri malipo ya mafao yao.

“Katika hali kama hiyo si jambo la ajabu kwa mstaafu anayesubiri malipo yake akatafuta mkopo ili kutatua shida zinazomkabili. Kumbuka kuwa wakati huo mtu huyu anakuwa hana kipato rasmi,” anafafanua.

Anasema malipo ya mafao yanachelewa kwa sababu kadhaa, ikiwamo kuchelewa kwa wataasfu kuwasilisha nyaraka ambazo hutumika kuandaa malipo hayo. Lakini pia wapo wengine ambao huomba kustaafu kwa hiari na wakati huo taasisi husika zinaweza kuwa hazijaandaa nyaraka zinazohitajika kwa ajili ya kuchakata madai hayo ya mafao.

“Wakati ninasubiri mafao yangu nilipata changamoto ya malipo ya ada ya mtoto ikanilazimu nitafute njia mbadala ya kujikwamua katika hili na uhitaji ulikuwa wa haraka. Nilisita kwenda kwenye taasisi za fedha kwa kuhofia kuchelewa kupata mkopo, hivyo nikaenda kukopa kwa mtu ambaye amesajiliwa na kuweza kukopa.

“Lakini baadaye nikapata kipeperushi cha Benki ya Posta, yaani TPB kinachoeleza suala la mikopo kwa wastaafu. Nikafuatilia kwenda kujua utaratibu wao, nikapewa maelezo kwa kina, hivyo nikapata mwanga na nikafanya uamuzi, nikajiunga na kuchukua mkopo bila tatizo mpaka leo hii mimi ni mteja wa benki hiyo,” anasema Bi Kunenge.

Anasema kila mstaafu ana nafasi ya kujiunga na taasisi za fedha ambazo zina mipango ya kuwakopesha wastaafu, lakini wengi hawalijui hilo.

Naye Meneja TPB Mkoa wa Mara, Hagai Gilbert, anasema kipindi cha kusubiri mafao kinaweza kuwa kifupi ama kirefu kulingana na mchakato.

Gilbert anasema ni jambo la bahati mbaya kuwa wastaafu wengi huamini kuwa taasisi za fedha zina masharti magumu ya kutoa mikopo, yanayomfanya mstaafu ashindwe kukopa kama vile kuwa na dhamana ya mali isiyohamishika.

“Kwa upande wa wastaafu, TPB tunahitaji barua ya kustaafu na kitambulisho cha uraia. Ni vema wastaafu wakayafahamu mambo haya na wanapokuja kwetu tunawaelewesha na wakihitaji mikopo wanapata kwa urahisi, kwa kutimiza masharti hayo nafuu,” anabainisha.

Tahadhari

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, ameipongeza Takukuru kwa kumbaini tapeli huyo wa mikopo na kumchukulia hatua. Amewataka wananchi kutosita kuripoti matukio kama hayo kwenye vyombo vya dola ili haki zao zisichukuliwe na matapeli wachache.

“Hatutamfumbia macho mtu yeyote anayetaka kuwaumiza wanyonge kwa manufaa yake binafsi. Lazima sheria ichukue mkondo wake na wahusika wawajibishwe,” anasema.

Kwa upande wake, Kuhanda, anaiomba Benki Kuu, kwa kuwa ndiyo yenye dhamana ya kuweka uwiano wa riba za mikopo katika taasisi za fedha, kuingilia kati ili kuondoa adha kama hii inayowapata wakopaji.

Lakini pia Kuhanda anaiomba Wizara ya Viwanda na Biashara, ambayo ina dhamana ya kuwasajili watoa mikopo, walitumie tukio hilo kufanya marekebisho yatakayohakikisha kuwa eneo hilo halitumiwi na matapeli kuwadhulumu wanyonge.

“Kwa sehemu kubwa mikopo ya aina hii imekuwa ikijitokeza mara baada ya mtu kuacha kupokea mshahara baada ya kustaafu. Hivyo, ni vema kipindi cha kusubiri mafao kiwe kifupi ili kuwaepusha wastaafu kupata uwezekano wa kuangukia kwa matapeli kama hawa,” anasema.