Wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma imetajwa kama moja ya maeneo nchini ambayo bado yanakabiliwa na matatizo ya ukatili wa kijinsia.
Takwimu zilizotolewa hivi karibuni zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2016 na mwaka jana, matukio 313 ya ukatili wa kijinsia yakiwamo ya kingono yalitokea wilayani humo na kuriporiwa. Kwa kuwa matukio mengi kuhusiana na ukatili wa kijinsia hayaripotiwi, basi inaaminika kuwa idadi ya matukio hayo wilayani humo ni kubwa kuliko takwimu rasmi zinavyoonyesha.
Taarifa kutoka Jeshi la Polisi wilayani Kakonko zinasema katika kipindi hicho wanawake 55 walibakwa. Kati ya hao, wanawake 11 walibakwa mwaka 2016, wanawake 16 mwaka 2017, mwaka 2018 yakaripotiwa matukio 19 ya ubakaji na mwaka jana wanawake tisa wameingiliwa kingono bila ya ridhaa yao.
Ukatili huo unajiri wakati Umoja wa Mataifa (UN) umeweka mkazo kuwa ifikapo mwaka 2030, nchi wanachama ziwe zimekomesha dhuluma zote dhidi ya wanawake.
Taarifa ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kakonko, S.F. Njau, kupitia Dawati la Jinsia na Watoto, inasema kesi nyingi kuhusu ukatili wa kijinsia zilizoripotiwa zinahusu mashambulio.
Ofisa wa Polisi wa wilaya hiyo Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto, Getruda Bahisha, anasema katika taarifa hiyo kuwa matukio mengi ya ukatili na unyanyasaji yanatokea ndani ya familia.
Akifafanua, anasema: “Kwa mwaka 2016 yaliripotiwa matukio18, mwaka 2017 matukio 20,
mwaka 2018 yaliripotiwa 28 na mpaka robo ya tatu ya mwaka 2019 tumekwisha kupokea malalamiko 16.”
Taarifa hizi zilitolewa wakati wa mdahalo wa kupiga vita ukatili wa kijinsia, ulioandaliwa na Shirika la Kivulini, ambalo ni moja ya mashirika yaliyojikita kupigana dhidi ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.
Mdahalo huo uliokuwa sehemu ya maadhimisho ya Siku 16 za kupiga vita ukatili wa kijinsia, ulifanyika katika Kijiji cha Kasanda, Wilaya ya Kakonko, mkoani Kigoma.
Kivulini, lenye makao yake jijini Mwanza na mshirika wake UN Women, wamekuwa mstari wa mbele kupinga dhuluma dhidi ya wanawake na wasichana. Moja kati ya mikakati wanayoitumia katika vita hiyo ni kutoa elimu kwa jamii na viongozi tofauti.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Polisi, katika kipindi hicho cha miaka mitatu, wanafunzi 31 katika wilaya hiyo nao wamepewa ujauzito, watano nao wakikatishwa masomo baada ya kuozeshwa na wengine sita inaripotiwa kuwa wamewekwa vimada na wanaume.
Ripoti inabainisha pia kuwa katika kipindi hicho familia 19 zimetelekezwa, mashambulio 175 yakiwamo 48 ya kudhuru mwili yameripotiwa, watoto wawili wametupwa na wengine wanane kuibwa katika mazingira ya kutatanisha.
Mahakamani
Jeshi la Polisi Kakonko limethibitisha kuwa, kati ya matukio 313 yaliyoripotiwa mwaka 2016 hadi 2019, kesi 189 zilifunguliwa mahakamani. Kati ya hizo, kesi 97 zilipata mafanikio kwa watuhumiwa wa vitendo hivyo kukutwa na hatia na kuhukumiwa adhabu mbalimbali zikiwemo vifungo gerezani. Kesi 15 bado zinaendelea mahakamani.
Hata hivyo, jumla ya kesi 77 zimekwama mahakamani kutokana na sababu mbalimbali, kubwa ikiwa ni mashahidi kutohudhuria wakati kesi zinapopangwa kusikilizwa. Cha kushangaza ni kuwa wakati mwingine hata waathirika wenyewe wanakosa kuhudhuria kesi zao!
Imebainika kuwa kushindwa kujitokeza kwa waathirika ili kutoa ushahidi kwenye kesi zinazowahusu kunatokana na njama zinazofanywa na watuhumiwa kwa kuwatorosha mashahidi hao ili kesi dhidi yao zikwame kwa kukosa ushahidi.
Sababu nyingine zilizothibitishwa kukwama kwa kesi hizo ni jamaa, marafiki na familia kukubali kupokea malipo kutoka kwa watuhumiwa, ikiwa kama fidia ya vitendo hivyo vya kikatili.
“Sababu nyingine ya kukwama kwa kesi hizi ni jamii kushindwa kutoa ushirikiano kwa kuhofia kutengwa katika jamii. Pia kesi hizo zinadhaminika mahakamani, hivyo baadhi ya watuhumiwa hutoroka baada ya kupewa dhamana na mahakama,” anaeleza Bahisha.
Wakati kesi 77 zikikwama kutokana na sababu zilizoainishwa hapo juu, kwa upande mwingine kesi 41 zilifungwa na polisi kwa sababu mbalimbali, ikiwamo ushahidi kutojitosheleza na baadhi ya waathirika kuamua ‘kuwasamehe’ watuhumiwa bila kujali madhara.
Bahisha anasema jamii inapaswa kubadilika kuhusiana na suala hili, kwa sababu ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa watoto ni uhalifu kama ulivyo uhalifu mwingine. Pia vitendo hivyo ni ukiukwaji wa haki za binadamu na ni uvunjaji wa sheria za nchi.
Changamoto hizo zinaonyesha kuwa elimu bado inahitajika zaidi ili kuihamasisha jamii kuacha kufanya ukatili. Aidha, jamii inapaswa kuelimishwa ili iweze kutoa ushirikiano unaotakiwa katika kukomesha vitendo hivi kama kwa kutoa taarifa pale vitendo hivi vinapotokea na kushirikiana na mamlaka husika katika kesi zinazofunguliwa dhidi ya watuhumiwa.
“Watoto zaidi ya 2,000 wa shule mbalimbali wamepatiwa elimu hiyo,” Getruda anasema katika taarifa aliyoitoa huku akitoa wito kwa jamii kuimarisha ushirikiano na polisi na asasi nyingine za serikali na kiraia zilizojikita kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika jamii.
Athari
Ofisa Miradi wa Shirika la Kivulini, Eunic Mayengela, anaeleza kuwa Mkoa wa Kigoma una kiwango cha asilimia 61 ya ukatili wa kijinsia na kufanya kuwa mmoja wa mikoa ambayo tatizo hilo ni sugu. Pamoja na mambo mengine, anasema vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto vinafifisha maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Anasema kitendo cha waathirika na watu wengine kushindwa kuonyesha ushirikiano na vyombo vya dola, kama vile kushindwa kwenda mahakamani kutoa ushahidi, kunawafanya watu hao nao kuwa wameshiriki kuirudisha jamii nyuma kimaendeleo.
Kwa mujibu wa Shirika la Kivulini, kiwango hicho cha ukatili mkoani Kigoma ni lazima kidhibitiwe hadi kufikia sifuri, lakini hilo halitatokea iwapo jamii haitashiriki kikamilifu katika mapambano hayo.
“Mfano, juzi tu mtoto mdogo wa miaka saba ameripotiwa kubakwa na kijana wa miaka 27. Tukio ambalo limegundulika siku nyingi baada ya ukatili huo kufanywa. Hebu fikiria, mtoto huyu mdogo ameingiliwa kingono, madhara yake yatadumu katika maisha yake yote. Hii ni athari kiasi gani? Unakuta mwanamke anapigwa na kupata ulemavu wa maisha. Sasa tunapaswa kusema hapana,” anasema.
Ofisa huyo wa Shirika la Kivulini anasema ukatili wa kimwili unaendana na vipigo, ukatili wa kiuchumi, kingono na kisaikolojia. Vitendo hivyo vyote vinaharibu maendeleo ya jamii na taifa zima, hivyo vinapaswa kukomeshwa.
Anatoa wito kwa Watanzania wakiwamo wakazi wa Mkoa wa Kigoma, hasa Wilaya ya Kakonko, kujitokeza mahakamani kwenda kutoa ushahidi dhidi ya wahalifu wa masuala ya ukatili ili wachukuliwe hatua zinazostahili.
“Ukiwa wewe ndiye umefanyiwa ukatili wa aina yoyote kama vile kupigwa, kubakwa, kunyimwa fursa za kufanya biashara, kutukanwa matusi ya nguoni, kubakwa au kulawitiwa, toa taarifa polisi. Kesi nyingi zinakwama mahakamani kwa sababu ya kukosa ushahidi. Mwananchi yeyote una wajibu kwenda kutoa ushahidi mahakamani ili aliyefanya ukatili aweze kufungwa na hatimaye kukomesha hii hali,” anasisitiza Mayengela.
Mashirika ya kiraia
Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Hoseah Ndagala, anayataka mashirika ya kiraia na serikali kuongeza ushirikiano katika kutoa elimu kwa jamii, kwani inaonekana ndiyo njia muafaka na ya ufanisi ya kukabiliana na tatizo hilo.
Anasema elimu zaidi inahitajika ili kutokomeza vitendo vya ukatili na hilo litawezekana tu iwapo wadau vikiwamo vyombo vya habari, watashirikiana kuhimiza usawa wa kijinsia ili lengo hilo litimie kabla ya mwaka 2030.
Kanali Ndagala anasema vyombo vya dola vina wajibu wa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watu wanaotuhumiwa kufanya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Anataja chanzo kikuu cha ukatili wa kijinsia kuwa ni umaskini katika jamii husika. Hivyo, anasema kuwa kuhimiza watu kufanya kazi kwa jitihada ili kujinasua na utegemezi kiuchumi ndiyo siri ya mafanikio katika kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
“Lakini, ninyi wasichana ni chanzo mojawapo. Mnasema nitumie hela na ya kutolea, oooh! Mara bodaboda, chipsi… mara unanunuliwa simu, ukija kushituka mimba hiyo. Ninyi ni hazina ya taifa. Kataeni na muwe mstari wa mbele kupinga unyanyaswaji na utegemezi,” anasema mkuu huyo wa wilaya.
Pamoja na mambo mengine, anasisitiza umuhimu wa waathirika wa ukatili, jamii na majirani wa watu wanaotendewa unyama huo kwenda mahakamani kutoa ushahidi.
Kauli za wananchi
Jacqueline Petro, mkazi wa Kakonko mkoani Kigoma, anaeleza kuwa wanawake wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa kijinsia, jambo linalowaumiza katika nafsi na kuwakwaza katika jitihada zao za kujiletea maendeleo.
Anasema manyanyaso wanayoyapata yanawanyima amani, hivyo analiomba Jeshi la Polisi na watendaji katika taasisi nyingine za serikali na binafsi kuimarisha ulinzi kwa wanawake wanaonyanyaswa. Anazitaka taasisi hizo pia kuongeza bidii katika ukamataji wa watuhuiwa na kuwafikisha mahakamani ili haki itendeke.
“Wanawake nao wanawatendea ukatili watoto wadogo. Wanawatuma sokoni kwenda kuuza vitumbua na vibalagala,” anasema Emmanuel Makoko, mkazi wa Wilaya ya Kakonko.
Kauli hiyo iliwaibua wanafunzi waliokuwa katika mdahalo huo ambao wanaeleza kuwa kina baba ndio wanaowatuma kwenda sokoni kuuza vitumbua, huku wengine wakisema mama zao ndio huwapa kazi hiyo.