Kuongezeka kwa joto kunazidi kuleta hali ya tishio kutokana na moto mkubwa unaowaka katika maeneo mengi nchini Australia.

Watabiri wa hali ya hewa wameonya kuwa ongezeko hilo la joto litaongeza ukame katika maeneo mengi, hivyo kutoa mwanya kwa moto kusambaa zaidi.

Taarifa zilizopatikana mwishoni mwa wiki zinaeleza kuwa moto huo umeanza kusambaa kuelekea kwenye maeneo yenye watu wengi, kiasi kwamba jeshi nchini humo limelazimika kutumia nyenzo zake kuanza kuwaokoa watu, hasa watalii waliokwama kwenye maeneo ambayo yamezingirwa na moto mkali.

Tayari zaidi ya watu kumi wameripotiwa kufariki dunia wiki iliyopita kutokana na moto huo huku makumi wengine wakiwa hawajulikani walipo katika maeneo ya Victoria. Makumi ya maelfu ya watu katika maeneo ya Victoria nao wameanza kuyakimbia makazi yao baada ya kuonywa kuwa mamlaka zinaweza kushindwa kuzuia moto kufika katika maeneo yao.

Idara ya Zimamoto ilionya mwishoni mwa wiki kuwa moto ungesambaa hadi maeneo ya Blue Mountains, kaskazini mashariki mwa Penrith. 

“Katika pwani ya kusini, moto mkali kutoka eneo la Bega hadi kusini mwa Rasi ya Batemans unaweza kusambaa maeneo mengine mengi zaidi,” taarifa inaeleza.

Pia, moto huo unaweza kusambaa kutoka Rasi ya Batemans kuelekea kaskazini hadi maeneo ya Rasi ya Jervis, kwani ulikuwa katika maeneo ya Snowy Mountains ambako kuna mazingira ya kuwezesha moto kusambaa.

Mbuga kadhaa za wanyama, ikiwemo Royal National Park, na maeneo yenye makambi katika eneo la Sydney yamefungwa kutokana na tishio la moto.

Waziri Mkuu, Gladys Berejiklian, ambaye ametangaza hali ya hatari hadi Alhamisi ijayo, anasema maeneo ya kaskazini, kusini na magharibi yamo katika tishio kubwa la moto, kwani joto litapanda na akasisitiza kuwa ni lazima watu na taasisi husika wajiandae kwa hali hiyo.

“Kama unakabiliana na hali isiyo nzuri na unahitaji msaada, tafadhali nenda kwenye vituo vya uokoaji,” anasema.

Kamishna Msaidizi wa Zimamoto huko NSW, Rob Rogers, alionya kuwa moto unaweza kusambaa kwa kasi kutokana na hali ya hewa.

“Kwa bahati mbaya tunaweza kupoteza nyumba lakini tutafurahi na tutajiona wenye bahati iwapo hakuna mtu atakayefariki dunia,” anabainisha.

Zaidi ya wazimamoto 3,000 walipangwa kwenda kupambana na moto huo huko NSW Jumamosi, wakati wazimamoto wengine 500 watawekwa kwenye maeneo maalumu. “Tupo tayari kukabiliana na hali yoyote itakayojitokeza,” anabainisha.





Boti ya Jeshi la Maji Australia ikitumika kuwahamisha watalii ambao maeneo yao yamezingirwa na moto.