Maandamano ya vurugu yaliyotokea wiki iliyopita katika Ubalozi wa Marekani jijini Baghdad ni tukio la hivi karibuni ambalo zinazisogeza Marekani na Iran kwenye vita kamili, wachunguzi wa mambo wanaeleza.

Maandamano hayo ni mwendelezo wa vurugu zilizoanza baada ya kuondolewa madarakani na kuuawa kwa kiongozi wa zamani wa Iraq, Sadam Hussein, mwaka 2003.

Kuibuka kwa kundi la waasi ambao wamechukua uongozi serikalini nchini Iraq nako kumechangia kuongezeka kwa uhasama huku serikali ya Rais Donald Trump ikipiga kampeni za kutaka kuiwekea Iran vikwazo kamili vya kiuchumi.

Wiki iliyopita Trump aliituhumu Iran kwa kuandaa njama kuvamiwa kwa Ubalozi wa Marekani jijini Baghdad na akasema kuwa ataamua jinsi ya kujibu shambulio hilo.

Maandamano hayo yalifuatia shambulio la mabomu la Marekani dhidi ya kundi la Kata’b Hezbollah linaloendesha shughuli zake kutokea Iraq, ambalo linashutumiwa na Marekani kuwa ndilo limekuwa likishambulia vikosi vya Marekani nchini Iraq kwa kutumia maroketi.

Zaidi ya askari 20 wa kundi hilo waliripotiwa kuuawa katika shambulio lililofanywa na Marekani, hivyo kusababisha maandamano hayo kwenye ubalozi.

Uwezo wa waandamanaji kuvunja ukuta wa nje na kufanikiwa kuingia kwenye eneo la ndani ambako waliwasha moto ni kitendo kinachoonyesha jinsi vikosi vya usalama vya Iraq vilivyotoa ushirikiano kwa waandamanaji hao.

Serikali ya Iraq imekasirishwa pia na mashambulizi ya Marekani dhidi ya wapiganaji walio ndani ya nchi hiyo, ikisema kuwa shambulio hilo limeifanya serikali kuwa na wakati mgumu kukabiliana na wapiganaji hao.

Waziri Mkuu wa Iraq, Adel Abdul Mahdi, alitangaza siku tatu za maombolezo kutokana na mashambulizi ya Marekani ambayo alisema kuwa yanatia hasira.

Idadi ya taasisi zinazoiunga mkono Marekani nchini Iraq imezidi kupungua na vituo vya Marekani na ubalozi wake nchini Iraq vimegeuka kuwa maeneo ambayo Wairaq wanaweza kuonyesha hasira zao.

Kataib Hezbollah ametishia kuzidi kuuandama ubalozi huo kwa kuhakikisha waandamanaji wanalindwa wakati wakiungana na wenzao wanaoiunga mkono Iran.

Richard Haas, Rais wa Baraza la Mahusiano ya Kimataifa, alituma ujumbe kwa njia ya twitter akisema: “Vurugu zinazoungwa mkono na Iran zilizoibuka Baghdad ni jibu kwa vita ya vikwazo vya kiuchumi inayoanzishwa na Marekani.”