Waziri Mkuu wa Israel anayekabiliwa na mashitaka mahakamani, Benjamin Nentanyahu, ameliomba Bunge kumpa kinga ya kutoshitakiwa katika kesi tatu za rushwa zinazomkabili.

Hii ni hatua ambayo haijawahi kuchukuliwa na kiongozi yeyote wa Israel na wanaharakati wameipinga wakisema inazuia usawa mbele ya sheria.

Hatua hiyo ya kuomba kinga ni tukio la hivi karibuni katika siasa za Israel ambazo zimesababisha serikali kushindwa kufanya kazi vizuri.

Akijulikana kwa mikakati yake ya kujinasua kwenye migogoro ya kisiasa, hatua ya Netanyahu kuzuia mashitaka dhidi yake kwa kuomba kinga ya Bunge kunaonyesha udhaifu wake, jambo ambalo linaweza kusababisha akaishia gerezani.

Hatua hiyo pia inatishia kuzidi kuligawa taifa hilo na kurefusha mgogoro wa kisiasa ambao umeiacha Israel bila serikali inayofanya kazi sawasawa kwa takriban mwaka mmoja sasa.

Netanyahu aliwasilisha ombi hilo la kinga saa tatu kabla ya kwisha kwa muda uliowekwa. Hatua hiyo inaweza kuchelewesha kwa miezi kadhaa kesi za jinai zinazomkabili, ambaye anakabiliwa na uchaguzi mkuu katika kipindi cha miezi miwili ijayo, ukiwa ni uchaguzi wa tatu kufanyika nchini humo katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja uliopita.

Iwapo ombi lake hilo litakubaliwa, kinga hiyo inaweza kumfanya asifikishwe mahakamani katika kipindi ambacho bado ataendelea kuwa mbunge.

Novemba mwaka jana mwendesha mashitaka aliwasilisha mahakamani mashitaka ya rushwa, ubadhirifu na matumizi mabaya ya ofisi dhidi ya Netanyahu ambaye ameyakanusha.

Tangu wakati huo hakuchukua hatua yoyote na watu wengi wakasubiri atachukua hatua gani kujilinda dhidi yake. Wachunguzi wa mambo wanasema Netanyahu alihofia kuwa hatua ya kuomba kinga ya Bunge ingeweza kuhatarisha ushindi wake katika uchaguzi ujao.

Katika hatua ya kupoza joto la kisiasa, Netanyahu mwenyewe amekielezea kitendo cha kuomba kinga kama ni jambo dogo na la kawaida. Akizungumza kupitia televisheni, alisisitiza kuwa hiyo ilikuwa ni mbinu ya muda tu ambayo inadumu hadi kipindi chake cha ubunge kitakapokoma.