Licha ya vikwazo inavyowekewa na Marekani, Kampuni ya vifaa vya kielektroniki ya Huawei ya China imepata mafanikio makubwa katika biashara zake mwaka uliopita.

Taarifa kutoka ndani ya kampuni hiyo ambayo inajulikana kwa kutengeneza simu za mkononi, mapato yake yamekua huku ikizidi kusaini mikataba ya teknolojia ya 5G.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa kampuni hiyo inabidi ikabiliane na vikwazo kadhaa mwaka huu wa 2020, ikiwamo kufungiwa katika masoko yake makubwa na kuzuiwa kutumia ‘application’ za Google Android.

Kwa upande mwingine, kampuni hiyo inabidi ikabiliane na wimbi la kesi inayomkabili Mkuu wake wa kitengo cha fedha, Meng Wanzhou.

Marekani inaishutumu Huawei kuwa ni hatari kwa usalama wa nchi na imezuiwa kuuza bidhaa na hisa zake katika nchi hiyo.

Hata hivyo, licha ya vikwazo hivyo, hesabu za awali zilizotolewa na kampuni hiyo zinaonyesha kuwa mapato yake yangefikia yuan bilioni 850 (sawa na dola bilioni 121.66 za Marekani) kwa mwaka 2019, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18 kwa mwaka, ingawa ni chini ya makadirio ya kampuni hiyo kwa mwaka husika.

Changamoto 2020

Ingawa Huawei imekwisha kusaini mikataba na nchi kadhaa kuhusiana na teknolojia ya 5G, lakini inaweza kuzuiwa kuingia katika masoko mengine ambayo yangeweza kuipatia fedha nyingi kupitia teknolojia hiyo mpya.

Wakati Australia na Japan zimeizuia Kampuni ya Huawei kuanzisha mtandao wa 5G katika nchi hizo, baadhi ya nchi bado zinafikiria iwapo ziiruhusu kampuni hiyo au la.

Ujerumani na Uingereza ni kati ya nchi ambazo hazijafanya uamuzi huo na inatarajiwa kuwa uamuzi wowote utakaochukuliwa na nchi hizo utatazamwa kwa karibu na nchi nyingine.

Rais Donald Trump wa Marekani anadaiwa kuzishinikiza nchi washirika kutoiruhusu Huawei kuanzisha teknolojia ya 5G katika nchi zao, akidai kuwa kampuni hiyo ni hatari kwa usalama wa nchi hizo, kwani vifaa na teknolojia yake inaweza kutumika kuzichunguza nchi hizo.