Ndugu Rais, inauma sana kuanza andiko la kwanza katika mwaka mpya kwa habari ya kuomboleza! Niwe mkweli, zaidi ya kumwona na kumsoma katika vyombo vya habari kuhusu mashitaka tata dhidi yake, Erick Kabendera simfahamu. Nadhani naye ni hivyohivyo, hanifahamu!
Mama yangu mpendwa ninajua ananisubiri kule juu kwa baba alikotangulia miaka mingi iliyopita, lakini uchungu wa kumkosa hapa duniani hautakuja kukoma mpaka pumzi yangu ya mwisho itakapoutoka mwili wangu!
Wako wenzetu ambao wamejaliwa kuendelea kuishi na mama zao hadi leo wakiwa katika afya njema kama waliwazaa jana! Na wako wengine ambao uhai wa mama zao kiafya unaning’inia juu ya uzi mwembamba.
Mama zao watakapowatoka ndipo watakapoujua uchungu wa kumkosa mama ambao wengine na sasa ni pamoja na Erick, tutaendelea kuumia kwa miaka yetu iliyobakia!
Mama yetu alitusihi kuwa hawezi kuishi bila Erick kwa sababu ndiye alikuwa tegemeo lake kuu, lakini kilio chake kilitua juu ya mioyo migumu mithili ya mawe! Maneno ya mpendwa mama yetu yametimia, naye ametutoka! Najaribu kuufikiria ukubwa wa uchungu aliokuwa nao mpendwa mama yetu wakati anaitoa roho yake kumkabidhi Muumba wake dhidi ya watu waliokuwa wamemshikilia mwanae, Wakongo wanasema: ‘Siitiki!’ Kwetu zamani lilikuwako neno, ‘laana’. Lingekuwa bado lipo na huku, kati yao angepona nani?
Kabla hajafikwa na mauti mama yetu aliomba akisema: “Ni mkubwa lakini cheo chake cha urais hakimzuii kuwa mtoto wa mtu, ana wazazi na anawalea. Kwa hiyo ninamwomba baba huyo anionee huruma, sina mwingine wa kunisaidia! Bila Erick siwezi kuishi. Mkubwa anihurumie, anihurumie, anisaidie, anisaidie!” Tunageuka nchi ya watu waliojaa machozi!
Fedha inakuwaje mpaka inatakata? Ni msamiati mpya sawa na watu wasiojulikana ubunifu mkubwa wa Awamu ya Tano bila kujua kuwa hakuna kitu kitakachobaki kuwa siri milele!
Julius Kambarage Nyerere ndiye alikuwa kinaya wangu katika maisha yangu. Mtu huyu alizisoma sana tawala za Afrika Magharibi za wakati ule. Kutokana na hilo alijitengenezea Kawawa wake! Rais Julius Kambarage Nyerere kamwe asingekwenda mwenyewe kuwaambia wananchi wa Ubungo waliovunjiwa nyumba zao kuwa hatawalipa fidia! Kisiasa huko ni kujinyonga mwenyewe mpaka kufa!
Ole wake mtu yule aliyemuingiza baba katika kundi la kuonekana vibaya siku zote. Kufanya jambo lenyewe lionekane ni la kitoto zaidi wakamtengenezea na washangiliaji waliofanana na wenzetu wanaokodiwa kwenda kulia katika msiba ambao si wao!
Rais Julius Kambarage Nyerere aliitawala nchi hii bila kuwa na hata chembe ya hofu kifuani mwake! Alisema wa kunidhuru labda atokee mwendawazimu! Alikuwa mtu wa haki! Nafsi ya mtu ikimkumbusha uovu autendao ndiyo huujaza moyo wake hofu! Ni hofu ndiyo humfanya mtu kuiona hata kazi ya Mungu kuwa ngumu! Kama rubani aendeshaye dege la mizigo kubwa kuliko yote duniani haoni ugumu katika kazi yake, basi katika kufanya kazi yako unaikosea.
Yawezekana waliokuwa wanatuambia kuwa nchi yetu ni maskini lengo lao lilikuwa wanapotuibia tusilalamike, si hatuna kitu, tunaibiwa nini? Yawezekana pia na watakaokuja kutuambia kuwa nchi yetu ni tajiri sana nao watataka wanapotawanya mali zetu ovyo ovyo pia tusilalamike, si tunazo nyingi, kuna ubaya gani? Lakini sasa wakati wa kuyaweka sawa umefika.
Huu ni mwaka alioufanya Bwana kwa wanaomkiri bila unafiki kuyaweka juu ya meza yote yanayotatiza katika nchi. Viongozi wa dini katika mahubiri yao ya siku ya Noeli wamebainisha pasipo kuacha shaka kuwa katika kipindi chote hiki cha miaka minne yetu tuliyoimaliza nchi na wananchi walitawaliwa na hofu. Wabobezi wa fikra wanasema katika hofu hakuna maendeleo.
Mwanamwema kaniandikia: “Mwalimu Mkuu, tumemaliza vyuo, na sasa tunapuyanga tu mitaani.” Tunawaonyesha ‘trela’ ya yale tunayotamani kuyafanya, lakini hayo si maendeleo ni kupuyanga!
Maskini na wanyonge mlioko katika nchi hii wekeni katika fahamu zenu kuwa mnakwenda katika Uchaguzi Mkuu huku viongozi wenu, kwa maana ya watawala na wa upinzani, wakiwa katika mzozo mkubwa.
Wanachogombania ni madaraka ili wawatawale. Walio katika madaraka hawako radhi kuyaachia na wanayoyataka hawako radhi safari hii kuyakosa. Na wote wamejiapisha kuwa liwalo na liwe!
Lakini katika hao wote, watawala na wapinzani, eleweni kuwa hakuna hata mmoja kati yao aliyeyatanguliza masilahi ya nyinyi wananchi maskini na wanyonge! Hivyo msiende katika uchaguzi kwa lengo la kumchagua mtu fulani ili awe rais.
Mchagueni mtu aliye tayari kuirudishia nchi hii uhuru wake wa kuwapata viongozi wake kwa amani, kwa uhuru na kwa haki sasa na siku zote zijazo!
Nchi hii ni kubwa kuliko hao wote. Rais Uhuru Kenyatta anasema hakuna anayeweza kuiongoza nchi salama akitumia kichwa chake peke yake! Akitokea mweye mawazo kama hayo miongoni mwetu, tumuogope kama ukoma! Hatufai!
Mchagueni mtu atakayewarudishia nchi katika hali yake ile ya mwanzo.
Mwenge wa Uhuru ulioasisiwa na Baba wa Taifa ili uulinde uhuru wenu, sasa umepoteza sababu ya kuwapo kwake. Mwanamwema kaniambia ni kwa sababu ya kumcha Mungu sana ndiko kulikomfanya Nyerere awashe mwenge utakaoizunguka nchi ili kuwapa matumaini wananchi kuwa wako huru.
Katika makanisa yote ziko taa za umeme zinazowaka sana lakini hata ikiwa mchana inawashwa mishumaa ili ilete nuru ya uhuru wa kweli katika vifua vya waumini! Leo Mwenge wa Uhuru umepangiwa kazi ya TAKUKURU. Si kazi ya Mwenge wanawema kuzindua miradi! Mwenge uliasisiwa ulinde uhuru wa watu wetu ili wasije wakatokea wasiojulikana wa kuwateka, kuwatesa na hata kuwapoteza!
Baadhi ya viongozi wetu hawana uwezo tena wa kufikiri kwa undani. Wanawasherehesha wananchi siku ya Uhuru wa nchi ya Tanganyika huku wakiwapeperushia bendera ya nchi nyingine tofauti kabisa, nchi ya Tanzania ambayo yenyewe ilizaliwa ikiwa huru.
Watanzania, nyinyi ni wamoja watoto wa baba mmoja. Anayewahubiria ili mbaguane, jua la Mwenyezi Mungu limuwakie hadi utosini! Kaeni katika meza ya maridhiano kama wana wa familia moja muyaweke mezani yote yanayowatatiza! Yeyote asiyetaka maridhiano, nyinyi wote katika ujumla wenu mkataeni mtu huyo hata kabla ya Uchaguzi Mkuu! HAWAFAI!